Kikosi cha Yanga kilichoipiga APR 2-0 |
Na Prince Akbar
MABINGWA watetezi wa Klabu Bingwa ya soka Afrika Mashariki
na Kati, Kombe la Kagame, Yanga SC ya Dar es Salaam, leo wanashuka dimbani
kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, kumenyana na Mafunzo ya Zanzibar katika
hatua ya Robo Fainali ya michuano hiyo.
Kocha wa Yanga, Mbelgiji Tom Saintfiet katika mchezo wa leo,
atamkosa kiungo Nizar Khalfan ambaye anasumbuliwa na maradhi ya nyonga, wakati
hali ya kinara wa mabao wa timu hiyo, Said Bahanuzi ‘Spider Man’ hadi jana
haikuwa ya kumpa uhakika wa kucheza mechi hiyo.
Bahanuzi anasumbuliwa na maumivu ya mgongo, wakat kiungo
Nizar Khalfan yeye kwa asilimia 100 hatacheza kutokana na maumivu hayo ya
nyonga.
Saintfiet aliiambia BIN ZUBEIRY jana kwamba, Nizar
hatacheza kabisa, lakini wachezaji wengine watatu, Bahanuzi, kipa Yaw Berko anayesumbuliwa na goti, kiungo
Athumani Iddi ‘Chuji’ na Hamisi Kiiza wanaosumbuliwa na quadriceps wako kwenye
hatihati kucheza.
Mtakatifu Tom amesema kwamba, Daktari wa Yanga, Sufiani Juma
anaendelea kufuatilia kwa karibu hali za Bahanuzi, Kiiza, Berko na Chuji ili
kuhakikisha wanakuwa fiti kwa ajili ya mechi ya leo.
Amesema sababu ya wachezaji wake kuumia mara kwa mara ni
kutokana na kucheza mechi mfululizo na kulingana na kanuni za mashindano hayo,
hawezi kutumia wachezaji zaidi ya 20, hivyo hana namna nyingine zaidi ya
kupambana na hali hiyo.
Bahanuzi ndiye kinara wa mabao wa Yanga hivi sasa, hadi sasa
akiwa amekwishaifungia timu hiyo mabao manne, hivyo kuingia kwenye mbio za
kuwania kiatu cha dhahabu cha mashindano hayo, ambayo tayari kwenye kabati la
Yanga kuna mataji manne yamehifadhiwa.
Mshambuliaji huyo mpya kutoka Mtibwa Sugar ya Morogoro, Ijumaa
alikaribia kuondoka na mpira uwanjani, kama si refa Dennis Batte kutoka Uganda
kukataa bao lake moja siku ambayo alifunga mawili yaliyokubaliwa dhidi ya APR
ya Rwanda, Yanga ikishinda 2-0, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam jioni hii.
Katika mchezo huo, Kocha Tom alimpumzisha Bahanuzi dakika ya
72 na nafasi yake ikachukuliwa na Jerry Tegete, wakati Nizar Khalfan kabla ya
hapo alimpisha Juma Seif ‘Kijiko’.
Matatizo ya mgongo kwa Spider Man yalianzia kwenye mechi na APR |
Mchezo kati ya Yanga na Mafunzo, utaanza saa 10:00 jioni na
utatanguliwa na mechi nyingine ya Robo Fainali kati ya URA ya Uganda na APR ya
Rwanda, wakati kesho Atletico Olympique Sport ya Burundi itamenyana na AS Vita
ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) katika Robo ya Fainali ya tatu
mchana, kabla ya Azam FC na Simba SC, zote za Dar es Salaam, kuhitimisha awamu
ya Nane Bora ya michuano hiyo.
Michuano hii, iliyoanza Julai 14 na inatarajiwa kufikia
tamati Julai 28, inadhaminiwa na Azam na SuperSport Televisheni.
RATIBA ROBO FAINALI
Julai 23, 2012
URA vs APR (Saa 8:00 mchana)
Mafunzo vs Yanga (Saa 10:00 jioni)
Julai 24, July
Atletico vs AS Vita (Saa 8:00 mchana)
Azam vs Simba SC (Saa 10:000 jioni)
0 comments:
Post a Comment