Na Mahmoud Zubeiry |
AKIIONGOZA kwa mara ya kwanza katika mechi, kocha Mbelgiji
Thom Saintfiet jana aliiwezesha Yanga, kushinda mabao 2-0 dhidi ya JKT Ruvu
katika mchezo wa kirafiki uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mabao ya Yanga yalifungwa na beki Nadir Haroub ‘Cannavaro’
dakika ya 18 kwa kichwa akiunganisha kona ya Juma Abdul, wakati la pili
lilifungwa na Mwanasoka Bora wa Uganda, Hamisi Kiiza ‘Diego’ dakika ya 72,
akiunganisha pasi ya nyota wa Rwanda, Haruna Niyonzima.
Katika mchezo huo, ilishuhudiwa mabadiliko ya kiuchezaji
kwenye kikosi cha Yanga, wakicheza soka ya utulivu, bila kukimbia ovyo kama
ilivyo ada yao, muda mwingi wakitulia kwenye eneo lao na kufanya mashambulizi
ya mipango.
Yanga ilitumia mshambuliaji mmoja tu kwenye mchezo huo,
Jerry Tegete huku viungo zaidi wakilundikwa uwanjani.
Baada ya mchezo huo, nilizungumza na kocha Thom na akasema
kwamba ameridhishwa na uchezaji wa timu na matokeo pia na anaamini taratibu
timu itazidi kuimarika hadi kwenye michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na
Kati, Kombe la Kagame.
Alisema baada ya mechi hiyo, atakuwa na vipindi vitatu zaidi
vya mazoezi kabla ya mechi ya ufunguzi wa Kombe la Kagame Jumamosi dhidi ya
Atletico ya Burundi.
Alisema atafanya siku moja moja kuanzia leo, kesho na
keshokutwa kabla ya kushusha timu uwanjani Jumamosi kukata utepe wa Kagame.
Yanga ndio mabingwa watetezi wa michuano hiyo, inayoshirikisha timu za Simba na
Azam pia katika orodha ya wenyeji.
Lakini, baada ya mechi hiyo minong’ono ilitawala juu ya namna
ambavyo Yanga walicheza- wakiwapa fursa wapinzani kuwa na mpira zaidi.
Ndiyo, ndivyo ilivyokuwa, muda mrefu Yanga walikuwa
wakiwaachia wapinzani mpira na wao kufanya kazi ya kuzuia, huku wakifanya
mashambulizi ya kushitukiza.
Mtakatifu Thom akifundisha |
SOKA NI TAALUMA
Soka ni mchezo, lakini ni taaluma ambayo makocha wanaenda
darasani na baada ya hapo wanafanya tathmini za kutafuta ubunifu ili kuweza
kumudu ushindani katika soka ya kisasa.
Tumeshuhudia michuano ya Kombe la Mataifa ya Ulaya hivi
karibuni, Euro 2012, Hispania wakiibuka mabingwa, baada ya kuifunga Italia 4-0
katika mchezo wa mwisho.
Lakini ukiirejea fainali ile kwa kina na kujiuliza kwa nini
Italia ilifungwa ‘kimdebwedo’ namna ile utagundua kitu kimoja tu, The Azzuri
walishindwa kujitofautisha na La Rojja mapema kabla ya mechi hiyo.
Kama Italia wangejitathmini kwa maana ya kila mchezaji na
timu na wakawatathmini wapinzani wao, basi wasingecheza walivyocheza hata
wakafungwa 4-0.
Italia walifunguka katika mchezo ule wakafakiria tangu
mwanzo kuwashambulia wapinzani, ambao wako vema kuliko wao kimchezo kwa tofauti
kubwa mno.
Hispania wazuri kuanzia namba moja hadi 11- kwa maana ya
safu ya ulinzi, kiungo na ushambuliaji, kwa ujumla La Rojja ni wazuri kama timu
kuliko Azzuri.
Hilo Italia hawakulitazama na ndiyo maana wakajaribu
kushindana uwezo na Hispania, matokeo yake wakapata kipigo kiliochoharibu ladha
ya fainali. Rejea Nusu Fainali na Fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu,
namna ambavyo Chelsea ikiongozwa na Roberto de Matteo, iliweza kwanza kuwavua
ubingwa Barcelona kabla ya kumbeba mwali kwa kuifunga Bayern Munich nyumbani
kwake.
Utagundua kwamba, soka ni taaluma ambayo inahitaji nidhamu
ya hali ya juu na kujitambua pia, tena dhidi ya mtu unayekwenda kukabiliana
naye na ndiyo maana katika dunia ya soka ya leo, hupaswi kumdharau mtu au timu
yoyote.
Tazama eneo la JKT, Yanga wachache kama hapa Nizar anapotaka kutoa krosi mbele ya wachezaji watatu |
NINI ANAFANYA MTAKATIFU THOM?
Wakati anasaini mkataba Yanga wiki iliyopita, alisema kwamba
falsafa yake ni ushindi, iwe bao 1-0 au 5-0, anachotaka ni ushindi tu. Hakutaka
kuzama ndani sana, na yeye mwenyewe akisema hataki kuwapa faida wapinzani wake
wajue mbinu zake mapema, lakini kwa weledi baada ya mechi ya jana wanaweza
kupata picha kamili kuhusu falsafa yake.
Mimi nililifanyia kazi hilo mapema tu, baada ya kusaini
mkataba nilifuatilia mazoezi yake na nilimsikia kwa kina anawaelekeza nini
wachezaji wake.
Kwa muda mrefu asili ya soka ya Yanga imekuwa ni kukimbiza
mpira uwanjani, muda wote kushambulia na ndiyo maana aina ya wachezaji wengi wa
klabu hiyo ni wale wenye kasi.
Hata msimu huu, Yanga imesajili wachezaji wengi wenye
kukimbiza mpira, kwa maana ya wachezaji wenye kasi- na katika mechi ya awali ya
kujipima nguvu ya klabu hiyo dhidi ya Express ya Uganda, dakika zote 45 za
kwanza Watoto wa Jangwani Uwanja wote ulikuwa wao katika mechi hiyo
waliyoshinda 2-1.
Lakini siku ya kwanza kabisa baada ya Mtakatifu Thom kusaini
mkataba, nilimfuatilia uwanjani, miongoni mwa maneno niliyosikia akiwaambia
wachezaji wake ni kwamba hataki mchezo wa kukimbia kimbia, anataka soka ya
kutulia na hata katika mazoezi yake hatakuwa akiwakimbiza sana wachezaji zaidi
ya kuchezea mpira sana.
Nikamfuatilia tena siku mbili zilizofuata, anawafundisha
nini Yanga, nilichogundua ni kile nilichokiona jana- hataki kucheza kwa
kupoteza nguvu na pumzi nyingi bila faida. Anataka soka ya mipango.
Wachezaji wake wanatulia kwenye eneo lao wakati wapinzani
wana mpira, lakini wanawamulika vema wapinzani wao hao katika mienendo yao
wasivuke kwenye mipaka yao.
Unaweza kusema ni mchezo fulani maarufu kama wa kupaki basi,
ambao mfalme wake Jose Mourinho, kocha Mreno wa Real Madrid, lakini mwisho wa
siku katika soka ya kulipwa unaweza kuuita mfumo wa ushindi na ndiyo maana
Mtakatifu Thom anajiita muumini wa ushindi.
Rejea mechi ya jana ya Yanga na JKT, kweli kwa kiasi kikubwa
JKT waliachiwa fursa ya kuwa na mpira, lakini nani alifanya mashambulizi mengi?
Nani alipata mabao? Ukipata majibu ya hayo maswali mawili huwezi kuacha
kuukubali mfumo huu mpya wa Yanga chini ya Mtakatifu Thom.
Bado Yanga wanafanya idadi kubwa ya mashambulizi ya mipango, kama hivi jana na JKT Ruvu |
KWA NINI YANGA IJIHAMI KWA JKT?
Labda yanaweza kuibuka maswali, kwa nini Yanga icheze mfumo
huu kwa timu kama JKT Ruvu, ambayo ilimaliza Ligi Kuu katika nafasi ya nane,
timu ambayo huwezi kuiita ya ushindani katika ubingwa wa ligi hiyo, zaidi tu ya
kuwaita wasumbufu?
Kama Yanga wanacheza kwa kupaki basi katika mechi na JKT,
vipi wakikutana na timu kama Simba au Azam tu kwa mfano- au wakienda kwenye
michuano ya Afrika?
Ndiyo, haya ni maswali sahihi kabisa baada ya mechi ya jana.
Lakini kama nilivyosema hapo juu, soka ni taaluma, ambayo walimu pamoja na
kusomea darasani, mwisho wa siku katika kujiendeleza zaidi wanazama ndani
katika kufanya ubunifu ili kuweza kumudu ushindani wa soka ya leo.
Walimu wana malengo na mitazamo- na ambayo wanapaswa
kuyafanyia kazi kwa maana ya kuyajengea mazingira ya kufanya kazi. Ni kama
ndondi tu, bondia anajiandaa kupigana na bondia, lakini mazoezini anapigana na
begi tu.
Bondia namba mbili kwa ubora anajiandaa kupigana na bondia
bingwa, lakini mazoezini anapigana na bondia ambaye hayumo hata kwenye orodha
ya mabondia 10 bora. Na anapigana naye kwa namna ambavyo amepanga kwenda
kupigana na mpinzani wake siku ya siku.
Akili ya Thom haipo hapa kabisa; Ananaangali Afrika 2014 |
THOM ANATAZAMA MBALI
Mapema tu wakati anamaliza kusaini mkataba, Mtakatifu Thom
alisema sera yake ni ushindi na mataji. Mataji yatakuja kutokana na kazi ambayo
itafanywa na timu yake. Timu itafanya kazi baada ya kuandaliwa kuifanya hiyo
kazi.
Waandishi wa Habari tunapenda kutumia maneno maandalizi ya
zimamoto, au kutokuwa na dira wala mwelekeo katika habari au makala zetu,
lakini sina uhakika kama wengi huwa tunatumia maneno haya huku tukielewa maana
yake halisi.
Sawa, maandalizi ya zimamoto maana yake maandalizi ya
kukurupuka badala ya kuwa na maandalizi ya muda mrefu.
Kutokuwa na dira wala mwelekeo ni kukosa malengo na njia za
kukufikisha pale ambako unaota kufika.
Kwa mfano Yanga leo, wanacheza Ligi Kuu ili wawe mabingwa na
wapate tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini wanajichezea tu ili
wakashiriki michuano hiyo mikubwa Afrika bila ya kuwa na maandalizi ya kucheza
michuano hiyo.
Mfumo ambao Yanga wanataka kucheza kwenye Ligi ya Mabingwa,
lazima waufanyie kazi mapema, wauzoee, wamudu na wakati ukifika wajue wanafanya
nini. Haya ni maandalizi.
Lakini ukija kwa upande wa dira na mwelekeo- Yanga
wanatakiwa wajue mapema aina ya wapinzani ambao watakwenda kukutana nao kwenye
michuano ya Afrika.
Soka yetu iko chini na wachezaji wetu wanazidiwa uwezo na
wachezaji wa nchi nyingine Afrika na ndiyo maana kila mwaka hatufiki mbali. Ila
kama tutajipanga kwa kutengeneza dira na mwelekeo, basi inawezekana kufanya
kile ambacho Chelsea walifanya dhidi ya Barcelona na Bayern.
Lazima tujitambue na tuwaheshimu wapinzani wetu- ili siku
tukienda kucheza nao, tucheze kwa adabu kwa lengo la la kutimiza azma ya
kushinda na kutwaa taji.
Thom hawaangalii JKT Ruvu na nina imani hawaaangalii Azam
kwa jinsi nilivyomsoma, bali anataka kuwatumia wote kumtengenezea timu ya
kushindana na TP Mazembe, Al Ahly, Esperance na vigogo wengine wa Afrika.
Anataka Yanga wazoee mfumo wa kucheza wakikutana na timu
bora Afrika. Thom anawafundisha soka Yanga.
SOKA NI MABAO; Hata Pele, mfalme wa soka duniani alisema siku nyingi...hapa Yanga wanashangilia bao |
YANGA WAWE WAVUMILIVU NA WENYE SUBIRA
Baada ya mechi kati ya Simba na Express iliyoisha kwa sare
ya bila kufungana wiki mbili zilizopita, nilifanya mahojiano na kocha wa
mabingwa hao wa Uganda, waliofungwa na Yanga 2-1 siku moja kabla- nikamuuliza
ipi timu nzuri kati ya hizo mbili za Tanzania.
Kocha huyo akasema Yanga wanatisha zaidi kwa sababu muda
wote wanashambulia tu na kasema mbele ya Simba, safu yake ya ulinzi ilikuwa
likizo. Lakini narejea miaka minne iliyopita, Yanga ikiwa chini ya Profesa
Dusan Savo Kondic, ililazimishwa sare na hawa hawa JKT, tena kocha akiwa yule yule
ambaye yupo hadi leo, Charles Killinda.
Killinda ni mchezaji wa zamani wa Yanga, na nilipofanya naye
mahojiano baada ya mechi, alisema Yanga lazima wabadilike, wajifunze kuchezea
mpira, haiwezekani muda wote wao wanashambulia tu.
Kwa kweli, mimi kama binadamu kwa wakati huo sikumuelewa
Killinda, ila haikuchukua muda mrefu kumuelewa- na kukubali kwamba, mfumo ambao
Yanga wamekuwa wakiutumia kwa muda mrefu ni wa ovyo.
Lakini kwa kujua kabisa mashabiki wa Yanga wamezoea kuwaona
wachezaji wao wakikimbiza uwanjani tangu enzi za akina Leonard Chitete na ndiyo
maana hadi leo wanamlilia Mrisho Ngassa na hawawezi kumsahau Edibily Lunyamila,
nasema umefika wakati wabadilike na wawe tayari kupokea mageuzi ya kiuchezaji
chini ya kocha wao mpya, Thom.
Nawasihi, mashabiki wa Yanga wakati Thom anaingia na timu
kwenye michuano ya Kombe la Kagame, wampe ushirikiano na wawe na subira. Najua
miongoni mwa mashabiki wa Yanga wapo mashabiki wa Chelsea na Mourinho- basi
wawe na subira.
Wawe na subira kwa sababu, Thom haangalii timu za Kagame
wala Ligi Kuu ya Bara, bali anafikiria Ligi ya Mabingwa Afrika 2014. Kwa uzoefu
wangu wa makocha wa kigeni, kuanzia ngazi ya klabu hadi timu ya taifa, ni
kwamba Thom ni kocha wa ukweli.
Anawapongeza marefa; yote furaha ya ushindi, angefungwa angekumbuka hili? |
Yanga wamvutie subira na wakubaliane na falsafa zake, na
wakiweza hivyo iko chini ya Mtakatifu Thom, watavunja rekodi za wapinzani wao
wa jadi, Simba kuwa timu yenye mafanikio zaidi katika michuano ya Afrika.
Naishia hapa wapendwa.
0 comments:
Post a Comment