Na Mahmoud Zubeiry |
YANGA jana, imeanza vibaya michuano ya Klabu Bingwa Afrika
Mashariki na Kati, baada ya kufungwa 2-0 na Atletico ya Burundi, Uwanja wa
Taifa, Dar es Salaam.
Mabao mawili ya Olivier Ndikumana katika dakika ya 81 na
90+3, yalitosha kuipa Atletico FC ushindi wa 2-0 dhidi ya mabingwa hao watetezi.
Yanga jana ilicheza ovyo na ilizidiwa katika kila idara-
angalau baada ya kufungwa bao la kwanza walijaribu kushambulia kwa mipira ya
pembeni, lakini walipopigwa la pili katika dakika ya tatu ya muda wa nyongeza
baada ya kutimu kwa dakika 90 za mchezo huo ‘walitepeta kabisa’.
Yanga ilikuwa ikicheza mechi ya pili chini ya kocha mpya,
Mbelgiji Tom Saintfiet, baada ya mechi ya awali ya kirafiki dhidi ya JKT Ruvu,
ambayo timu hiyo ilishinda 2-0.
Falsafa ya Tom anayeingia katika wiki ya pili tangu atue
Jangwani, ni kucheza soka ya utulivu, zaidi wakipaki basi- wakati umaarufu wa
Yanga kwa muda mrefu ni soka yao ya kasi na pasi ndefu, zaidi wakitumia
mashambulizi ya kutokea pembeni.
Na ndiyo maana mawinga wengi bora na maarufu nchini walicheza
Yanga, hii ni tangu enzi za akina Awadh Gessan, Leonard Chitete, Abubakar Salum
‘Sure Boy’, Sanifu Lazaro ‘Tingisha’, Edibilly Lunyamila, Ephraim Makoye,
Mrisho Ngassa na wengineo.
Yanga wapo kwenye kipindi cha mpito kuelekea katika
mabadiliko ya mfumo wa uchezaji, ambao ukifanikiwa utakuwa bora zaidi na wenye
tija.
Yanga wanatoka uwanjani kinyonge |
Mtakatifu Tom anampongeza kocha wa Burundi |
Atletico wanashangilia ushindi |
Mechi ya kwanza kwa asilimia kama 40, Yanga walifanikiwa
kuumudu mfumo mpya, lakini jana walichemsha ile mbaya.
Wachezaji wengi wa Yanga jana hawakuwa vizuri, walikuwa
hawafikishi pasi, walikuwa wanapokonywa mipira kwa urahisi, mtu kama Jerry
Tegete hata mipira ilikuwa haiwezi kutulia miguuni mwake.
Alikuwa anaanguka ovyo hadi akatolewa kumpisha Said
Bahanuzi. Hata Bahanuzi alipoingia naye pia alicheza chini ya kiwango. Angalau alipoingia
Nizar Khalfan kasi ya mashambulizi iliongezeka.
Kwa kweli, jana wachezaji wa Yanga waliwasononesha mashabiki
wao- lakini kwa waumini wa soka, wanajua wakati mwingine hutokea hayo hata
Ulaya- ndio maana Manchester United ilifungwa sita, mwisho wa msimu ikalingana kwa
pointi na mabingwa Manchester City.
Kila kitu kilikataa Yanga jana na nilijiuliza maswali mengi-
pamoja na kwamba natambua timu za Burundi zina hulka ya kucheza soka safi ya
kuvutia, tangu enzi zile za utawala wa Inter Star na Vital’O, baadaye Prince
Louis na sasa Atletico.
Nilijiuliza; au kwa sababu Yanga haikuwa kambini? Maana yake
tatizo kubwa la wachezaji wa Kitanzania ni kutojitambua, mtu anayeweza kuingiza
mwanamke kambini na kulewa, akiwa nyumbani kwake inakuwaje? Si sherehe ya
mitungi na mikasi?
Nilijiuliza, labda wachezaji walipewa mazoezi magumu siku
moja kabla ya mechi- au ulikuwa uchovu wa kawaida walioamka nao wengi miongoni
mwao? Sikupata majibu.
Lakini kitu ambacho naweza kuwaambia wana Yanga, wawe na
subira. Tena sana. Matokeo kama ya jana na hali ya mchezo kwa ujumla ilivyokuwa
kocha na benchi lake zima la ufundi wameona na naamini wanakwenda kuyafanyia
kazi.
Desturi moja nisiyoipenda ya wana Yanga ni kukosa subira kwa
wachezaji wao na makocha- hii lazima waepukane nayo. Wakithubutu kuanza kuzomea
timu kwa sasa au kocha, litakuwa kosa kubwa ambalo litavuruga mustakabali mzuri
wa timu unaotayarishwa.
Kocha atachanganyikiwa na wachezaji kadhalika. Viongozi pia
watachanganyikiwa. Itakuwa hatari. Kocha akichanganyikiwa ni mbaya zaidi, kwa
sababu anaweza kufikiria mbinu mbadala ya kuwafurahisha mashabiki- labda
ataamua timu irudi kucheza soka ile ile ya Kuala Lumper, Malaysia matokeo yake
Yanga wataendelea kuwa vibonde kwenye mashindano ya Afrika.
Huu mfumo ambao Tom anautumia kwa sasa, anataka wachezaji
wauzoee vema, ili siku Yanga wanacheza na TP Mazembe, Al Ahly, Esperance au
Enyimba mwaka 2014 washinde kwa staili ya kupaki basi na kushambulia kwa
kushitukiza.
Na ni lazima autumie katika kila mechi ili uzoeleke vema. Narudia
kuwaambia wana Yanga, wawe na subira. Hata Rome, haikujengwa siku moja. Wasalam!
0 comments:
Post a Comment