Kikosi kipya Yanga |
Na Princess Asia
YANGA imerejea. Yanga imeamua kushiriki michuano ya Ujirani
Mwema, inayoandaliwa na Chama cha Soka Zanzibar (ZFA), imeelezwa.
Ofisa Habari wa Yanga, Louis Sendeu ameiambia BIN
ZUBEIRY asubuhi hii kwamba, wameamua kurejea kwenye michuano hiyo,
baada ya kusikia wapinzani wao wa jadi, Simba wanatamba wamewakimbia.
Awali, Yanga ambao ni washindi wa Medali ya Shaba ya Ligi Kuu
ya Bara walijitoa, kwa sababu ya kuhofia wachezaji wake kuumia kabla ya kuanza
Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame.
“Mara nyingi tunapokwenda kwenye michuano ya Zanzibar,
wachezaji wetu huumia, hivyo tunahofia hilo lisijitokeze tena wakati tuna wiki
mbili tu kabla ya kuanza kutetea Kombe la Kagame,” alisema wiki iliyopita,
Ofisa Habari wa Yanga, Louis Sendeu akitoa tamko la klabu hiyo kujitoa.
Lakini leo Sendeu amesema; “Tunaondoka mchana wa leo saa
sita kwenda kushiriki mashindano ya Ujirani Mwema, tumefanya hivyo ili
kuwaonyesha wapinzani wetu Simba kwamba hatuwaogopi na tunaomba sana tukutane
nao fainali,”alisema Sendeu.
Michuano hiyo inaanza rasmi leo, kwa mabingwa wa Tanzania
Bara, Simba SC kufungua dimba na mabingwa wa Zanzibar, Mafunzo kwenye Uwanja wa
Amaan, Zanzibar, wakati washindi wa Medali ya Fedha ya Ligi Kuu ya Bara, Azam
FC nao watacheza mechi yao ya ufunguzi dhidi ya timu ya taifa ya vijana chini
ya umri wa miaka 23 ya Zanzibar (U23) kwenye Uwanja huo huo wa Amaan.
Mechi kati ya Azam na U23, maarufu kama Karume Boys ndio
itatangulia na mechi ya Simba itafuatia usiku kwenye Uwanja huo huo.
Tayari Azam wapo visiwani Zanzibar tangu jana, wakati
Wekundu wa Msimbazi watapasua mawimbi mchana wa leo kuelekea visiwani humo.
Wakati michuano ya Ujirani Mwema ilianza jana visiwani
Zanzibar, Kombe la Kagame linatarajiwa kuanza Julai 14, Yanga ikifungua dimba
na Atletico ya Burundi.
Simba, Yanga na Azam zote zitacheza Kombe la Kagame pia.
0 comments:
Post a Comment