OGOPA JEZI NAMBA 11 YANGA; Said Bahanuzi akishangilia kwa staili ya kuonyesha jezi namba yake baada ya kufunga bao leo |
Na Prince Akbar
YANGA imeonyesha matumaini ya kutetea taji lake la Klabu
Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, baada ya kuifunga APR ya
Rwanda mabao 2-0, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam jioni hii.
Shujaa wa Yanga leo, alikuwa ni mshambuliaji mpya kutoka
Mtibwa Sugar ya Morogoro, Said Bahanuzi, aliyefunga mabao yote hayo, moja kila
kipindi.
Hadi mapumziko, tayari Yanga ilikuwa mbele kwa bao 1-0,
lililofungwa na Bahanuzi dakika ya 22, akiunganisha krosi ya Hamisi Kiiza.
Dakika ya 43, Bahanuzi alitupia tena mpira nyavuni, pasi ya
Kiiza, lakini refa Dennis Batte kutoka Uganda akakataa.
Kipindi cha pili, Yanga waliendelea kucheza kwa kuelewana na
kasi, wakilitia misukosuko muda wote lango la APR na dakika ya 67, beki mmoja
wa APR alikuwa anataka kumpiga chenga Bahanuzi kwenye eneo la hatari, lakini
mshambuliaji huyo akafanikiwa kuunasa mpira huo na kumtoka beki huyo kabla ya
kumchambua kipa Jean Claude Ndoli.
Lilikuwa bao tamu, ambalo liliwanua vitini mashabiki wa Yanga
na kuamini sasa wameshinda mechi.
Kocha Tom Saintfiet alimpumzisha Bahanuzi dakika ya 72 na
nafasi yake ikachukuliwa na Jerry Tegete, wakati Nizar Khalfan kabla ya hapo alimpisha
Juma Seif ‘Kijiko’.
Kwa ushindi huo, Yanga imemaliza mechi za Kundi C ikiwa
katika nafasi ya pili kwa pointi zake sita, mabao tisa ya kufunga, matatu ya
kufungwa, Bahanuzi akiwa amefunga manne kati ya hayo, akifuatiwa na Hamisi
Kiiza mwenye matatu, moja Stefano Mwasyika na lingine Nizar Khalfan.
Atletico ya Burundi inaendelea kuongoza Kundi C, kwa pointi
zake saba, baada ya kucheza mechi tatu, kushinda mbili na kutoa sare moja,
wakati APR ya Rwanda inashika nafasi ya tatau nayo imefuzu Robo Fainali, kwa
pointi zake nne, wakati Waw Salaam ambayo haina pointi na imeaga.
Katika mchezo huo, kikosi cha Yanga kilikuwa; Yaw Berko,
Juma Abdul, Oscar Joshua, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Athumani Iddi
‘Chuji’, Stefano Mwasyika, Haruna Niyonzima, Said Bahanuzi/Jerry Tegete, Hamisi
Kiiza na Nizar Khalfan/Juma Seif.
A.P.R.; Jean Claude Ndoli, Mbuyu Twite, Kabange Twite,
Mugiraneza Jean, Leonel St Preus, Johnson Bagoole, Iranzi Jean Claude, Ngabo
Albert, Tuyizere Donatien, Suleiman Ndikumana na Olivier Karekezi.
Nahodha Cannavaro akimpongeza kijana |
Kiiza akiwa amembeba juu Bahanuzi kumpongeza |
MKALI; Bahanuzi anakwenda kufunga la pili |
HATARI LAKINI SALAM; Kiiza alikosa bao la wazi hapa |
Daktari wa Yanga, Sufiani Juma akimtibu Bahanuzi baada ya kuumizwa na kipa wa APR, Jean Claude Ndoli |
MIPANGO YA KWENYE KONA; Wachezaji wa Yanga wakipiga mishemishe zao langoni mwa APR wakati wa kona |
0 comments:
Post a Comment