Silaha mpya za Yanga zikiwa zimeongezana, wa mbele Yondan, anayemfuatia Juma Abdul, Said bahanuzi na Barthez |
Na Prince Akbar
MABINGWA wa soka Afrika Mashariki na Kati, Yanga SC ya Dar
es Salaam leo wanashuka kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, kumenyana na JKT
Ruvu katika mchezo wa kirafiki, kujipima nguvu kabla ya kuanza kutetea taji
lake, Kombe la Kagame Jumamosi.
Mchezo huo utakaofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ni
ambao kocha mpya, Thom Saintfiet kutoka Ubelgiji aliuhitaji mno ili kutazama
mapungufu kikosini mwake, kabla ya kuanza kwa michuano hiyo.
Mchezo huu utakuwa kipimo kizuri kwa Yanga, kwa sababu JKT
Ruvu ni timu ya ushindani katika Ligi Kuu na msimu uliopita ilimaliza katika
nafasi ya nane kwa kujikusanyia pointi 32, sawa na Kagera Sugar iliyomaliza
nafasi ya saba.
Ruvu inayonolewa na mchezaji wa zamani wa Yanga, Charles Killinda
imekuwa ikitoa wachezaji wazuri wenye vipaji na kwa mfano msimu huu, mabingwa
hao wa Afrika Mashariki na Kati wamemsajili Frank Damayo kutoka timu hiyo ya
jeshi na msimu uliopita walimsajili Juma Seif ‘Kijiko’.
Wapinzani wao wa jadi, Simba nao wanaye kiungo Mwinyi Kazimoto,
waliyemtoa JKT Ruvu pia msimu uliopita, lakini ndani ya kikosi cha timu hiyo
kuna wakali wengine ambao leo wanatarajiwa kuipa changamoto nzuri Yanga kabla
ya kuanza kwa Kagame.
Mashabiki wa Yanga leo watarajie mapinduzi makubwa ya soka
katika klabu yao, kutoka ule mfumo wa kusukuma mashambulizi mfululizo hadi
kucheza soka ya utulivu ya pasi nyingi, tena timu ikitumia mshambuliaji mmoja
tu kwa falsafa ya ‘Mtakatifu Thom’ ambayo imekuwa ikifanyiwa kazi mazoezini
tangu mwalimu huyo aanze kazi siku tano zilizopita.
Aidha, kwa wana Yanga leo ni siku nyingine ya kuwashuhudia
wachezaji wao wapya waliosajiliwa kwa fedha nyingi, kama kipa Ally Mustafa ‘Barthez’,
beki Kelvin Yondan kutoka Simba, beki Juma Abdul kutoka Mtibwa Sugar, viungo
Frank Damayo, Nizar Khalfan aliyekuwa anacheza Marekani, Said Bahanuzi kutoka
Mtibwa Sugar na mshambuliaji Simon Msuva kutoka
Moro United.
Lakini pia wataendelea kuwaona kiungo Athumani Iddi ‘Chuji’
na mshambujliaji Jerry Tegete ‘waliozaliwa upya’. Haruna Hakizimana Fadhil ‘Niyonzima’
tayari amerejea na hapana shaka atapewa nafasi leo uwanjani na hivyo kuongeza
idadi ya mafundi kwenye kikosi cha Yanga.
Ni mamatarajio kwamba utakuwa mchezo mzuri na muhimu kwa klabu
hiyo, kabla ya kushuka dimbani Jumamosi kupepetana na Athletico ya Burundi.
0 comments:
Post a Comment