Spider Man |
MABINGWA watetezi wa Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati,
Kombe la Kagame, Yanga SC leo wanashuka Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam
kumenyana na timu ya Jeshi la Rwanda, APR katika Nusu Fainali ya pili ya
michuano hiyo kuanzia saa 10:00 jioni, mchezo ambao utatanguliwa na Nusu
Fainali ya kwanza kati ya AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na
Azam FC.
Yanga iliingia Nusu Fainali baada ya kuitoa Mafunzo ya
Zanzibar kwa penalti 5-3, kufuatia sare ya 1-1 ndani ya dakika 90, wakati APR
iliitoa URA ya Uganda kwa kuichapa mabao 2-1.
Nusu Fainali ya pili inayozikutanisha Azam FC iliyoitoa
Simba kwa kuichapa 3-1 na AS Vita iliyoitoa Atletico ya Burundi kwa kuichapa
2-1, itaanza saa 8:00 mchana Uwanja huo huo wa Taifa.
Azam na Vita nayo itakuwa
mechi tamu, kwa sababu timu zote zinacheza soka ya kuvutia na zina wachezaji
wenye vipaji- zaidi kila timu ina mshambuliaji anayewania ufungaji bora wa
michuano hii.
Azam kuna John Raphael Bocco ‘Adebayor’ mwenye mabao manne
akifungana na Hamisi Kiiza wa Yanga katika nafasi ya tatu, wakati Vita inaye
kinara wa mabao katika Kagame ya 2012, Etikiama Taddy mwenye mabao sita,
akifuatiwa na Said Bahanuzi ‘Spider Man’ wa Yanga mwenye mabao sita.
Akizungumzia mchezo dhidi ya APR, kocha wa Yanga, Tom
Saintefiet alisema kwamba utakuwa mgumu kwa sababu timu hizo zitakuwa
zinakutana mara ya pili, baada ya mechi ya awali ya kwenye Kundi lao, C ambayo
Yanga ilishinda 2-0.
“Utakuwa mchezo mgumu, APR ni timu nzuri, wanacheza kwa
ufundi, nguvu, lakini tunataka kushinda na tutakwenda kupigana ili
kushinda,”alisema Tom.
John Bocco 'Adebayor' |
Hata hivyo, Mbelgiji huyo alisema katika mchezo wa leo
atawakosa kipa wake namba moja Yaw Berko na kiungo Nizar Khalfan ambao wote ni
majeruhi.
Mtakatifu Tom alisema kutokana na kucheza mechi mfululizo,
wachezaji wengi wa Yanga wanalalamika maumivu, ila wako tayari kucheza na wana
nia na dhamira ya kutetea Kombe.
Safu ya ushambuliaji ya APR inaweza kuongozwa na wakali
wawili, Mrundi Suleiman Ndikumana na Olivier Karekezi ambao wote wana miili
mikubwa ni hatari kweli sambamba na kiungo mshambuliaji, Mganda Danny Wagaluka,
wakati Yanga bila shaka Said Bahanuzi na Hamisi Kiiza wataendelea kumpumzisha
kwenye benchi Jerry Tegete na Haruna Niyonzima ataongoza safu ya kiungo.
Kihistoria mechi kati ya Yanga na APR huwa ni kali na za
kusisimua tangu zianze kukutana mwaka 1996 katika Klabu Bingwa Afrika Mashariki
na Kati na mara nyingi watoto wa Jangwani ‘hutoshana nguvu’ na timu hiyo ya
jeshi la Rwanda.
Azam ikiwa na morali ya hali ya juu, safu yake ya kiungo inatarajiwa
kuongozwa na kiungo bora mzalendo kwa sasa Tanzania, Salum Abubakar ‘Sure Boy
Jr’ wakati kwenye ushambuliaji mfungaji bora wa Ligi Kuu, Adebayor wa Chamazi
atapewa dhamana.
BIN ZUBEIRY inazitakia kila la heri timu za Tanzania katika
hatua hii zishinde leo na kulihakikisha Kombe la Kagame kuendelea kuishi katika
Bandari Salama. Mungu ibariki Tanzania, zibariki Azam na Yanga. Amin.
JE WAJUA?
1.
Klabu ya Armee Patriotique Rwandaise, maarufu
kama A.P.R., ilianzishwa mwaka 1993 na inamilikiwa na Jeshi la Rwanda na katika
kipindi cha uhai wake, mafanikio yake makubwa ni kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya
Rwanda mara 12 (1995, 1996, 1999, 2000, 2001, 2003, 2005, 2006, 2007, 2009,
2010 na 2011), Kombe la Kagame mara mbili (2004 na 2007) na kufika Nusu Fainali
ya Kombe la Washindi mwaka 2003.
2.
Young Africans SC maarufu kama Yanga
iliyoanzishwa rasmi mwaka 1935, hadi sasa mafanikio yake makubwa ni kutwaa
ubingwa wa Ligi Kuu ya Bara mara 23, (1968, 1969, 1970, 1971, 1972, 1974, 1981,
1983, 1985, 1987, 1989, 1991, 1992, 1993, 1996, 1997, 1998, 2002, 2005, 2006,
2008, 2009 na 2011), Kombe la Kagame mara nne (1975, 1993, 1999 na 2011),
kufika Robo Fainali ya Klabu Bingwa Afrika mara tatu (1969, 1970 na 1998) na
Kombe la Washindi 1996.
3.
Wakati Yanga, kocha wake ni Mbelgiji Tom
Saintfiet, APR inafundishwa na kocha Mholanzi, Ernie Brandts- na wakati Yanga
Mwenyekiti wake ni mfanyabiashara milionea, Yussuf Manji, APR Mwenyekiti wake
ni mdogo wa rais wa Rwanda, Paul Kagame aitwaye Alex Kagame.
4.
Nembo ya Yanga ina alama ya Mwenge, ramani ya
Afrika na mpira- ikimaanisha kushiriki harakati za Uhuru wa Tanganyika, ambayo
baadaye iliungana na Zanzibar na kuwa Tanzania (Mwenge), timu halisi ya Afrika
(ramani) na timu ya mpira (mpira), wakati nembo ya APR ina alama ya mnyama
Simba na mpira- vikimaanisha, ni wafalme kama mnyama Simba porini (Simba) na
timu ya mpira (mpira).
5.
Wakati Yanga ambayo huvalia jezi za rangi ya
kijani na njano, ilishiriki michuano hii kwa mara ya kwanza mwaka 1975 na
kutwaa Kombe, APR ambao huvalia jezi za rangi nyeupe na nyeusi siku zote, mara
nyingi zikiwa za mistari ya punda milia, ilishiriki kwa mara ya kwanza michuano
hii mwaka 1996 na kushika nafasi ya pili, baada ya kufungwa 1-0 na Simba kwenye
fainali.
6.
Wakati wapinzani wa jadi wa Yanga, nchini
Tanzania ni Simba SC kwa APR wapinzani wao wa jadi Rwanda ni Rayon Sport.
Makocha; Ernest Brandy Mholanzi wa APR kulia na Tom Saintfiet Mbelgiji wa Yanga |
REKODI YA YANGA NA
APR KAGAME;
1996 Dar es Salaam;
Yanga 2-2 APR (Nusu Fainali, APR ilishinda kwa penalti 4-2)
2008 Dar es Salaam;
Yanga 2-2 APR (Kundi C)
2012 Dar es Salaam;
Yanga 2-0 APR (Kundi C, Julai 20)
2012 Dar es Salaam;
Yanga V APR (Nusu Fainali, Julai 26)
Mechi ya kwanza ambayo Yanga iliifunga APR 2-0 |
0 comments:
Post a Comment