Wachezaji wa Simba wakiwa wamemuinua juu Kaseja baada ya fainali ya Kombe la Urafiki wiki mbili zilizopita |
SIMBA SC jana imetolewa katika Klabu Bingwa ya soka Afrika
Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, baada ya kufungwa na Azam FC mabao 3-1,
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika Robo Fainali ya mwisho.
Na Mahmoud Zubeiry |
Mbaya wa Simba jana alikuwa John Raphael Bocco ‘Adebayor’ aliyefunga
mabao yote matatu, wakati bao la kufutia machozi la Simba lilifungwa na Shomary
Kapombe.
Japokuwa Bocco aliondoka na mpira jana, lakini nyota wa
mchezo alikuwa Salum Abubakar ‘Sure Boy Jr’, ambaye alitawala sehemu ya kiungo
na kuiongoza vema timu yake hata ikapata ushindi huo mnono.
Maneno mengi yameibuka baada ya matokeo hayo, jambo ambalo
ni kawaida kwa timu zetu hapa nchini, dosari na kasoro nyingi huzungumzwa baada
ya matokeo mabaya. Leo ndio wanasema timu mbovu na hata kocha Milovan Cirkovick
amesema timu yake haikuwa tayari kwa mashindano haya.
Najaribu kujiuliza, Simba imetolewa na Azam, timu ambayo
wiki mbili zilizopita ilikutana nayo kwenye fainali ya Kombe la Urafiki na
ikashinda kwa penalti 3-1, baada ya sare ya 2-2.
Wiki mbili zilizopita, Simba ilikuwa noma, ilikuwa inatisha
baada ya kuifunga Azam kwa matuta, lakini wiki mbili baadaye, Simba mbovu.
Jamani!
Umefika wakati sasa tuwe watu wa kujadili zaidi hali halisi,
kufanya tathmini ya kina ili kubaini makosa yetu, badala ya kupenda kuzungumza
kwa chuki, jazba na mazoea. Nimewasikia wachambuzi fulani wa radio moja nchini
wanazungumzia Simba- kwanza huwezi kujua pointi yao ni ipi. Mara kukosekana kwa
Emanuel Okwi kumepunguza makali ya Simba, ndiyo manaa hata Felix Sunzu amekuwa
hatishi sasa.
Jamani, hilo ni tatizo lililofanya Simba ipoteze mechi ya
jana? Watanzania tunapenda kukurupuka tunapotaka kusajili wachezaji bila
kufuatilia rekodi zao na ndiyo maana kuna wakati tunaingia mkenge kwa magarasa.
Sunzu katika mashindano haya ameonyesha hayuko sawa- amekosa
mabao ya wazi yasiyopungua 10. Sasa kwa nini uwadanganye wana Simba kukosekana
kwa Okwi kunamfanya hata Sunzu awe butu, wakati anapata nafasi akiwa yeye na
kipa anamdakisha, anapiga nje, anaanguka, au mpira unamgonga unaondoka.
Mimi nawaambia wachambuzi wa kibongo, wakumbuke mashindano
haya hata kwa ambao hawaendi mpirani, wanapata fursa ya kuona kupitia Super
Sport na Star TV- wamekuwa wakimuona Sunzu akipokea pasi za mwisho kama
alizokuwa akipewa na marehemu Patrick Mafisango, akipigiwa krosi kama ambazo
alikuwa akipigiwa na Okwi, lakini anaishia ‘kumbwelambwela’.
Lakini Sunzu tangu atue Simba, lini alikuwa mkali hata
akawanyima watu usingizi? Aliwafunga Yanga kwa penalti kwenye mechi ya Ngao
mwaka jana na kwenye Ligi Kuu, kiungo Mafisango alikuwa mfungaji bora wa timu
kwa mabao 10, sikumbuki yeye kama alifikisha hata matano.
Huyu ni mchezaji anayelipwa dola za Kimarekani 3,500,
takriban Sh.Milioni 5 kwa mwezi Simba SC na huwezi kupata jibu kwa nini
anamzidi maslahi Shomary Kapombe. Simba ilimsajili Sunzu baada ya kutupiwa
virago El Hilal kwa sababu alikuwa hafungi mabao.
Simba ilimsajili Sunzu kwa kukumbuka alikuwa mfungaji bora
wa Kombe la Challenge, au watuambie walimfuatilia wapi maendeleo yake baada ya
hapo, ikiwa klabu aliyokuwa anaitumikia iliamua kuachana naye kwa sababu
hafungi na sasa tushangae nini hafungi Simba?
Kuisaidia Simba ni kuzama ndani na kuangalia matatizo ya
msingi ya timu, kwa sababu huwezi kuwaambia watu eti Simba leo mbovu, wakati
wiki mbili zilizopita wachambuzi hao hao waliisifia Simba inatisha na Juma
Kaseja ni kipa bora na wakaitabiria kufanya vizuri kwenye Kagame.
Sasa nataka nieleze matatizo ya msingi ya Simba
yaliyowagharimu leo.
BEKI YA KUSHOTO;
Simba ilifanya kosa kumuacha Juma Jabu bila kusajili beki mwingine
mbadala hodari wa kushoto, kwani Paul Ngalema aliyesajiliwa badala yake
hajamvutia kocha Milovan na ndiyo maana jana akampanga Shomary Kapombe beki ya
kushoto.
Ikumbukwe Amir Maftah aliumia kidole baada ya mechi na AS
Vita na ikaelezwa hatacheza tena mashindano haya.
Kapombe asili yake ni kiungo na anaweza kuchezesha timu
vizuri akicheza kulia na hata katikati, ila amekuwa akitumiwa kama beki wa
kulia na kati na anacheza vizuri tu, lakini upande wa kushoto umemshinda.
Kama utaurejea vizuri mchezo wa jana, mipira mingi Azam
walikuwa wanapitishia upande wake.
UPANGAJI MBOVU WA KIKOSI:
Lino Masombo na Juma Nyosso wote ni mabeki wa aina moja na
lilikuwa kosa kubwa kuwapanga pamoja na hadi sasa bila shaka tumejiridhisha
Simba haina beki wa uhakika wa kati, au kocha anataiwa kuisuka upya safu kwa
kutumia wachezaji alionao kikosini ikibidi hata kumrejesha sentahafu Mussa
Mudde.
Sina neno Jonas Mkude, alicheza vizuri katika nafasi ya
kiungo mkabaji, pasi zake zilikuwa zinafika na mwanzoni alijitajidi na kupunguza
makali ya Kipre Michael Ballou hadi alipoumia na kutoka na nafasi yake
kuchukuliwa na Ramadhan Chombo ‘Redondo’.
Takriban mechi mbili au tatu, Mussa anamdhihirishia Milovan,
kwamba hawezi kucheza kama kiungo wa pembeni, lakini anandelea kumlazimisha na
hapo ndipo unapoweza kujiuliza viungo wa pembeni akina Kiggi Makassy, Salim
Kinje, Uhuru Suleiman na hata Christopher Edward walisajiliwa wa nini?
Sunzu, tangu mashindano yanaanza amekuwa akiboronga na bado
ameendelea kupewa nafasi kwenye kikosi cha kwanza na Danny Mrwanda yupo tena ni
huyu aliyeingia kwenye fainali ya Kombe la Urafiki akaenda kusababisha penalti
iliyofungwa na Mwinyi Kazimoto, wakati Simba ikiwa nyuma kwa mabao 2-1.
Kuna vitu vinaendelea ndani ya Simba kiasi kwamba inakuwa
vigumu kuamini kama ni matakwa ya kocha, au kuna nguvu za ziada kutoka kwa
wajuaji? Tumeona mara kadhaa Haruna Moshi ‘Boban’ huwa mzuri zaidi anapotokea
benchi na tumeona cheche za Abdallah Juma, lakini mambo mbona yanaenda kinyume
sasa?
Suala si kufungwa, bali ni kiwango duni cha timu- kwa sababu
kufungwa hata timu bora kama Barcelona hufungwa na timu za kawaida kama
Chelsea, bali inashitua kuona wachezaji ambao hawako vizuri wanalazimishwa
kucheza.
Lino Masombo kila mpira anaosha- hadi kuna wakati Boban
akamkaripia, jamani Simba hawachezi hivyo, Simba wanamtembeza nyoka chini- soka
ya kutungua maembe ina wenyewe hapa na wanafahamika.
Kote nilipoogelea ni katika kutanua mjadala tu, lakini hoja
yangu ya leo ni kwamba; wiki mbili zilizopita Simba ilikuwa inatisha, wiki mbili
baadaye Simba mbovu, jamani!
Simba tishio wiki mbili zilizopita |
MAFUNDI BENCHI; Kutoka kulia Kiemba, Kinje, Mrwanda, Obadia, Kiggi na Waziri Hamadi. Abdallah Juma, Paul Ngalema hawakuvaa kabisa. |
0 comments:
Post a Comment