Okwi |
Na Princess Asia
EMMANUEL Okwi, mshambuliaji wa Simba SC amepewa wiki mbili
zaidi za kuendelea na majaribio katika klabu ya FC Red Bull Salzburg ya Austria
yenye maskani yake Wals-Siezenheim, nchini humo na baada ya hapo ndipo majibu
yatatoka.
Katibu wa Simba Evodius Mtawala ameiambia BIN ZUBEIRY
jana usiku kwamba, Okwi ambaye tayari yuko huko kwa wiki moja, hadi
sasa anafanya vizuri ndio maana kapewa wiki mbili zaidi, ili kocha wa klabu
hiyo ajiridhishe zaidi na kiwango cha Mganda huyo.
Klabu hiyo inayotumia Uwanja wa Red Bull Arena, ikiwa zaidi
inafahamika kama SV Austria Salzburg kabla haijanunuliwa na kampuni ya Red Bull
mwaka 2005, imewahi kufika Fainali ya Kombe la UEFA mwaka 1994 na inacheza Ligi
Kuu ya Austria, iitwayo Bundesliga kama Ligi Kuu ya Ujerumani.
Timu hiyo ni kama timu ambayo Okwi, anachezea kwa sasa,
Simba SC, kwani nayo inavaa jezi za rangi ya nyeupe na nyekundu na imewahi kutwaa
taji la Bundesliga ya Austria mara saba na pia ilicheza Ligi ya Mabingwa Ulaya
msimu wa 1994–1995 kama Casino Salzburg, na kuwa timu pekee, ambayo haikufungwa
na mabingwa wa wakati huo, Ajax Amsterdam.
Awali, Okwi aliikosesha Simba Sh. Bilioni 2 kwa kukataa
kujiunga na klabu ya Mamelodi Sundown ya Afrika Kusini na kuamua kwenda Austria,
ambako inaelezwa klabu hiyo iko tayari kutoa Euro 600,000 akifuzu.
Awali Olando Pirates ya Afrika Kusini ilimuomba Okwi akafanye
majaribio huko kama angefuzu wangemsajili dau la dola 550,000 kabla ya kuibuka
kwa taarifa za kutakiwa Italia na klabu ya Parma.
Hata hivyo, Simba SC ilisema imeshindwa kumshawishi Okwi
kwenda kucheza Afrika Kusini kwa kuwa mwenyewe anataka kucheza Ulaya tu. Wakala
aliyeiunganisha Simba na Pirates akawasilisha ofa nyingine kutoka Mamelodi,
ambayo ni Euro 600,000 na kupanda hadi Sh. Bilioni 2, lakini bado mabingwa hao
wa Tanzania, walishindwa kumshawishi Okwi kwenda Ligi Kuu ya Afika Kusini
(PSL).
0 comments:
Post a Comment