Jerry Tegete anafunga dhidi ya Express; Lakini hama malengo, anajichezea tu |
JUZI niliandika kwa muhtasari kuhusu wachezaji wawili wa
Tanzania, Danny Davis Mrwanda na Nizar
Khalfan, ambao kwa hakika kutokana na kuonekana wachezaji wenye malengo,
wananifurahisha na nikasema kwamba wanafaa kuwa kioo cha wachezaji wengine wa
Tanzania.
Na Mahmoud Zubeiry |
Nilisema hawa jamaa ni wapiganaji, hawasiti kurudi nyuma
kujipanga upya, mara wanapopoteza nafasi.
Sasa Danny amesaini Simba, akitokea Hoang Anh Gia Lai,
aliyoichezea kwa msimu mmoja akitokea Dong Tam Long An, zote za Vietnam.
Ni huyu Danny ambaye mwaka 2004 alikwenda kufanya majaribio
katika klabu ya Yanga, lakini pamoja na kufanya vizuri, enzi hizo akiitwa
Okocha, akatemwa dakika za mwishoni, kocha wa Yanga wakati huo, Kenny Mwaisabula.
Danny alipotemwa Yanga dakika za mwishoni, akaenda Arusha
kujiunga na AFC ya huko na msimu wa 2005 alicheza soka baab kubwa, hata
akasajiliwa na Simba SC msimu uliofuata.
Alicheza Simba SC kwa mafanikio na msimu wake wa kwanza tu,
aliitwa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars.
Mwaka 2008, Danny alinunuliwa na klabu ya Tadhamon ya Kuwait
kwa pamoja na kiungo Nizar Khalfan. Mchongo waliupataje? Stars ilikwenda
ziarani Saudi Arabia na ikiwa huko ndipo soka yao ikamvutia kiongozi mmoja wa
klabu hiyo, akawanunua wote.
Lakini baada ya msimu mmoja, Danny hakuongezewa mkataba na
klabu hiyo, hivyo akarejea nyumbani na kujiunga tena na Simba SC. Hakurudi kama
amefika, au aliyekata tamaa, bali aliendelea na mikakati yake ya kutoka.
Alicheza Simba hadi 2010 alipopata ofa tena ya kwenda
Vietnam ambako amecheza hadi msimu huu anarudi. Sitaki kuamini Danny amekuja
kumalizia soka yake Simba SC. Naamini kama ilivyokuwa awali, amerudi kucheza
nyumbani, baada ya kumaliza mkataba Vietnam, huku akitafuta nafasi nchi nyingine.
Kuna kitu Danny alipost kwenye page yake ya facebook wiki
hii, kinachonifanya niamini huyu ni mchezaji anayejitambua na mwenye malengo. “U-superstar
huwa ni feki...hung'arisha tu ukiwa na market, open your mind bongo superstars,”
aliandika.
Kwa mtazamo huu, Danny anatembea akijua ana deni. Ana deni
la kuhakikisha anakuwa na soko wakati wote. Na kama ni hivyo, Danny hawezi
kubweteka, lazima atahakikisha siku zote anakuwa vema.
Kama mchezaji, Danny anatakiwa kuwa fiti wakati wote ili
acheze vizuri. Na kucheza vizuri ndiko kutamfanya aendelee kuwa supa star na
kupamba kurasa, kuanzia za blogs hadi magazeti. Kama mimi BIN ZUBEIRY, nafungua
moyo wangu. Nampenda sana Danny, wakati wote kama mchezaji wa Kitanzania kioo
cha wachezaji wengine. Nampenda Nizar Khalfan, ingawa sijamuelezea kwa undani
hapa, lakini naye ana fikra sawa na za Danny.
Amekatishiwa mkataba Marekani, karudi Yanga kujipanga upya,
kama tu alivyomaliza mkataba Kuwait, akarudi Moro United kujipanga. Maisha
ukiyaonea noma, yanakutoa nishai kweli kweli.
Nizar Khalfan |
Najua, kuna wachezaji walikwenda nje kucheza, ama wamekosa
timu au wametemwa, lakini wanaona noma kurudi nyumbani kujipanga upya. Danny na
Nizar hawana akili hiyo. Na watarudi tu juu.
Tatizo nini kwa wachezaji wetu?
Wachambuzi maarufu Tanzania wamekwishaandika sana na kila
mmoja amejaribu kuelezea kiini cha tatizo kwa mtazamo wake.
Baada ya kipindi kirefu cha kufuatilia kwa kina na kufanya uchunguzi,
nimegundua kwamba tatizo la wachezaji, kubwa ni kukosa malengo.
Wachezaji wetu wanakuwa na nia ya kufikia kucheza Simba au
Yanga pekee, hawana ndoto za zaidi ya hapo na ndio maana kuvuka hapo limekuwa
suala zito,
Katika maisha kila jambo linafanikiwa kutokana na malengo,
ambayo yanatimia kutokana na mipango.
Kama mchezaji atakuwa ndani ya mipango, kwa mfano akiwa timu
ya vijana U17, anasema kwanza anataka acheze hadi timu ya taifa ya wakubwa, awe
ana namba ya kudumu kwenye kikosi cha kwanza.
Lazima atapambana kuhakikisha anafikia malengo yake na kwa
sababu hiyo hawezi kubweteka hata kama atasajiliwa Simba au Yanga, atajua
lazima kila siku ana deni la kufikia malengo yake.
Hatua ya pili, kama atajiwekea malengo kwa mfano, anataka
kuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu, kuwa mchezaji bora, basi lazima atapambana hadi
atimize malengo yake. Atakuwa mshindani siku zote. Siku moja nilimuambia Jerry
Tegete, kwamba yeye hana malengo, ndio maana japo anajua kufunga, lakini
hajawahi kuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu.
Nimekuwa nikimpigia sana kelele Tegete, lazima awe na
malengo ili apambane kuyatimiza badala ya kujichezea tu. Mbona anafunga kwenye
mechi za Simba? Si kwa sababu ana malengo hayo, basi akiamua angalau kila mechi
afunge bao moja, ataweza na mwisho wa msimu atavaa kiatu cha dhahabu.
Tazama John Bocco ‘Adebayor’, miaka miwili iliyopita tayari nilijua
siku moja atakuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu, na kweli baada ya kuzidiwa na Boniphace
Ambani, msimu wa kwanza, Mussa Mgosi msimu wa pili, Mrisho Ngassa msimu wa
tatu, hatimaye msimu uliopita ametimiza malengo yake.
Tegete malengo yake yanaishia kuifunga Simba na ataendelea
kuwafunga. Lakini kwa nini wachezaji wetu wawe na mitazamo finyu? Naamini umefika
wakati wachezaji wetu wawe na mitazamo ya mbali zaidi.
Mrwanda na mwanawe, Jr. |
Wawe na ndoto za kuishi maisha mazuri ya kifahari kupitia
vipaji vyao. Leo Bocco amekwishakuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu, sasa akijiwekea
malengo, kwamba ndani ya misimu mitatu nataka niwe nacheza Ulaya, kama ataamua
kupambana kuyatimiza, naamini atafanikiwa.
Tegete niseme nini, alipata nafasi Ulaya, akafanya majaribio
akafuzu, lakini hayo hayakuwa malengo yake, malengo yake yalikuwa kucheza
Yanga, hivyo akarudi Yanga.
Miaka ya 1990, kulikuwa kuna wachezaji wawili, Ally Yussuf ‘Tigana’
na Mwanamtwa Kihwelo, hawa hawakupenda kabisa kucheza Tanzania, ila kama Nizar
na Mrwanda ilikuwa wakimaliza mikataba yao, wanaporudi nyumbani kusaini Simba
au Yanga, basi wamerejea kujipanga na muda si mrefu wanaondoka tena.
Katika siku zijazo nitazungumzia pia, kwa nini baadhi ya
wachezaji wa Tanzania hushindwa kucheza nje, ila kwa leo ili nieleweke vizuri
naomba mada iwe hii tuu, wachezaji wetu wanaishia mwisho wa malengo yao na kama
watapanua wigo wa malengo yao, basi watasonga mbele pia. Wasalam!
0 comments:
Post a Comment