Sure Boy Jr. |
Na Prince Akbar
KIUNGO wa Azam FC, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, amesema kwamba
anasikitishwa na tuhuma zilizozagaa kwamba yeye ni miongoni mwa wachezaji waliocheza
chini ya kiwango katika Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe
la Kagame dhidi ya Yanga, timu yao ikilala 2-0.
Sure Boy Jr. ameiambia BIN ZUBEIRY kwamba tuhuma hizo
zinamnyima raha na kwa mara ya kwanza tangu aanze kuchezea Azam, hivi sasa
anajisikia mnyonge.
Sure amekana tuhuma hizo hazina ukweli wowote ndani yake na
kwamba wanazungumza dhana tu, kitu ambacho ameonya si kizuri na kitaivuruga
timu yao.
“Ukiutazama ule mchezo, utaona sisi tulijituma sana, siwezi
kusema nani hakucheza kwa uwezo wake wote, muda mwingi tulikuwa kwenye lango
lao na tulitengeneza nafasi nyingi kuliko wao. Ila tu bahati haikuwa yetu.
Kuna bao moja Yanga waliokoa mpira ukiwa unaelekea nyavuni
na mimi ndiye nilitoa pasi ya mwisho, sasa unasemaje tulihujumu timu? Au kwa
kuwa tumefungwa? Mimi kwa kweli sipendi haya maneno.
Sisi tulitaka hilo Kombe, lakini bahati haikuwa yetu. Sisi ndio
tumeumia zaidi. Mimi nawashauri viongozi wetu, wayachukulie haya kama matokeo
ya kawaida ya mchezo, tusianze kuvurugana saa hizi mapema, tuanze kujipanga kwa
ajili ya mechi ya Ngao ya Jamii na Ligi Kuu,”alisema kiungo huyo bora kwa sasa
Afrika Mashariki na Kati.
Jumamosi Azam ilifungwa mabao 2-0 na Yanga katika fainali ya
Kagame, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kushindwa kutimiza ndoto zake za kuwa
timu ya kwanza nje ya Simba na Yanga kutwaa Kombe hilo.
Lakini wengi wanaamini, Sure anakuwa miongoni mwa wanaotuhumiwa
kwa sababu baba yake mzazi, Abubakar Salum ni kocha wa timu ya vijana ya Yanga
ni pia mchezaji wa zamani wa klabu hiyo.
0 comments:
Post a Comment