Na Prince Akbar
SHIRIKISHO la Soka Tanzania
(TFF) limepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha Mwenyekiti wa Chama cha Soka
Mara (FAM), Fabian Samo kilichotokea leo asubuhi (Julai 10 mwaka huu).
Ofisa Habari wa TFF, Boniphace
Wambura Mgoyo, ameaimbia BIN ZUBEIRY leo mchana kwamba, Samo ambaye Novemba 13
mwaka jana alichaguliwa kwa kipindi cha pili mfululizo kuwa Mwenyekiti wa FAM
katika uchaguzi uliofanyika wilayani Rorya alikuwa amelazwa Hospitali ya Taifa
Muhimbili (MNH), Dar es Salaam akisumbuliwa na maradhi ya figo.
Wambura amesema taratibu za
mazishi ya Samo ambaye alikuwa mjumbe wa Kamati ya Ukaguzi wa Hesabu (Internal
Audit Committee) ya TFF ikiwemo siku atakayozikwa bado zinafanywa na familia
yake.
Amesema Samo alitoa mchango
mkubwa katika maendeleo ya soka mkoani Mara na Tanzania kwa ujumla, vitu
ambavyo vilichangia kuchaguliwa kwake tena kuiongoza FAM.
Amesema msiba huo ni pigo kwa
familia ya Samo, FAM, TFF na mchezo wa mpira wa miguu kwa ujumla nchini
kutokana na mchango na mawazo aliyotoa kwa kipindi chote alichokuwa kiongozi.
Amesema TFF inatoa pole kwa
familia ya marehemu Samo, FAM, jamaa na marafiki na kuwataka kuwa na uvumilivu
katika kipindi hiki cha msiba huo mzito. Pia TFF itatoa ubani wa sh. 200,000
kwa familia ya marehemu kama rambirambi zake.
Mungu aiweke roho ya marehemu Samo
mahali pema peponi. Amina
Wakati huo huo: Wambura amesema
kwamba, wakati wa mechi za Kombe la Kagame Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam
kuanzia Julai 14-28 mwaka huu, screen kubwa iliyoko uwanjani itatumika kwa
matangazo ya biashara na ujumbe mbalimbali kwa washabiki watakaoshuhudia mechi
hizo.
Amesema TFF inakaribisha
kampuni na wadau mbalimbali wanaotaka kuweka matangazo yao wakati wa michuano
hiyo itakayoshirikisha klabu kumi na moja kutoka ukanda huu wa Afrika Mashariki
na Kati.
Amesema muda wa kurushwa
matangazo hayo yanayotakiwa kuwa kwenye mfumo wa DVD ni kabla ya mechi kuanza,
wakati wa mapumziko na baada ya mechi. Matangazo hayo yanatakiwa kuwa ya
sekunde 60 (dakika moja) au sekunde 30 (nusu dakika).
Aidha, Wambura amesema kwamba Kozi
ya makocha wa mpango wa grassroots unaolenga wachezaji mpira wa miguu
(wasichana na wavulana) wenye umri kuanzia miaka 6-12 imeanza leo (Julai 10
mwaka huu) kwenye ukumbi wa Msimbazi Center, Dar es Salaam.
Amesema Wakufunzi kutoka
Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) ndiyo wanaoendesha kozi hiyo
iliyofunguliwa na Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah.
Amesema Kozi hiyo
itakayomalizika Julai 15 mwaka huu inashirikisha washiriki 35, na mwendelezo wa
ile ya awali iliyofanyika Desemba 14-17 mwaka jana jijini Dar es Salaam.
Amemtaja Gouinden Thandoo
kutoka Mauritius ni mmoja wa wakufunzi wa FIFA wanaoendesha kozi hiyo.
0 comments:
Post a Comment