HONGERENI; Mwenyekiti mpya wa Yanga, Manji akiwa Makamu wake Clement Sanga |
Na Prince Akbar
SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limeupongeza uongozi mpya
wa Yanga uliochaguliwa katika uchaguzi mdogo uliofanyika Julai 15, mwaka huu
ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam.
Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniphace
Wambura Mgoyo, ameiambia BIN ZUBEIRY mchana huu kwamba, ushindi
waliopata wajumbe wapya sita waliochaguliwa kuingia kwenye Kamati ya Utendaji
unaonesha jinsi ambavyo wanachama wa Yanga waliohudhuria uchaguzi huo walivyo
na imani kwao.
Mume huyo wa Mwandishi wa gazeti la Mwanaspoti, Ndaya
alisema, TFF inaahidi kuendeleza ushirikiano wake kwa Kamati ya Utendaji ya
Yanga ambayo hivi sasa ina vinara wapya, na kwamba wana changamoto kubwa ya
kuhakikisha wanaendesha shughuli za klabu hiyo kwa kuzingatia katiba na kanuni.
Pia tunatoa pongezi kwa Kamati ya Uchaguzi ya Yanga chini ya
Jaji Mkwawa na Kamati ya Uchaguzi ya TFF inayoongozwa na Deogratias Lyatto kwa
kuhakikisha uchaguzi huo unafanyika kwa utulivu na kwa kuzingatia katiba na
kanuni.
Katika uchaguzi huo, Yussuf Manji alishinda Uenyekiti,
Clement Sanga, Makamu na Aaron Nyanda, Abdallah Bin Kleb, George Manyama na
Mussa Katabaro nafasi za Ujumbe wa Kamati ya Utendaji.
Uchaguzi huo, ulifuatia Wajumbe wengi wa Kamati ya Utendaji
katika uongozi uliochaguliwa miaka miwili iliyopita, wakiwemo Mwenyekiti Wakili
Lloyd Baharagu Nchunga na Makamu wake, Davis Mosha kujiuzulu.
0 comments:
Post a Comment