Yondan akisaini Yanga na mpunga huo mezani |
KIKAO cha Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji,
kilichofanyika Julai 17, mwaka huu, kupitia mikataba na nyaraka zote
zinazohusiana na mchezaji Kevin Yondani katika kujiridhisha juu ya hadhi yake
ya usajili katika mashindano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la
Kagame kilimhalalisha beki huyo wa kati kuchezea Yanga.
Na Mahmoud Zubeiry |
Taarifa ya Mwenyekiti wa Kamati hiyo ya Shirikisho la Soka
Tanzania (TFF), ilisema;
“1. Kwa mujibu wa
mapitio ya nyaraka zote zilizotajwa hapo juu na kufanyiwa upembuzi yakinifu,
Kamati iliridhika pasi na shaka yoyote kuwa suala zima la mchezaji Kevin
Yondani ni la kiutendaji, hivyo uamuzi wa Sekretarieti ya TFF kuwasiliana na
Klabu ya Simba kwa suala hilo la kiutendaji
kama Sekretarieti ilivyofanya
katika barua yake ya Julai 14 mwaka huu ulikuwa sahihi.
2. Kamati ilibaini
kuwa Mkataba wa mchezaji Kevin Yondani na Klabu ya Simba ulimalizika Mei 31
mwaka huu. Hivyo kwa taratibu za usajili mchezaji Kevin Yondani kuanzia Juni 1
mwaka huu alikuwa ni mchezaji huru.
3. Aidha Kamati
ilibaini kuwa Mkataba uliowasilishwa na Klabu ya Simba TFF ukiwa na maana ya
kuongeza mkataba uliokuwepo TFF baina ya mchezaji Kevin Yondani na Klabu ya
Simba uliwasilishwa TFF, Juni 7 mwaka huu ambapo ni kinyume cha utaratibu wa
kuongeza mikataba ya wachezaji unaozitaka klabu kuwasilisha mikataba ya
kuongeza muda wa mikataba ya wachezaji wao wakati mkataba halisi haujaisha muda
wake. Hivyo mkataba huo kwa jicho la kisheria haupo.
4. Hata kama kamati
ingeuona mkataba huo katika jicho la sheria, bado mkataba huo una tatizo la
kisheria hasa katika tarehe ambazo pande mbili husika ziliingia makubaliano
hayo. Ukiuangalia mkataba huo unabainisha kuwa, wakati mchezaji Kevin Yondani
aliingia makubaliano Desemba 23 mwaka jana, upande wa pili wa kimkataba ambao
ni Klabu ya Simba inaonekana iliingia makubaliano hayo kupitia kwa Makamu
Mwenyekiti wake Geofrey Nyange Kaburu, Desemba 23 mwaka huu.
Mwenyekiti wa Simba SC, Alhaj Aden Ismail Rage, akionyesha Mkataba wa Simba na klabu hiyo, huku akiupitia wa Yanga na kuukosoa |
5. Kisheria utata
huu unaweza kuondolewa na pande husika tu kwa kurekebisha dosari hiyo kwa
maridhiano kuweka saini katika mabadiliko hayo ili kuthibitisha mabadiliko
hayo. Hivyo katika jicho la kisheria mkataba huo hauwezi kutumika kumzuia
mchezaji huyo kwenda katika klabu anayoipenda wakati akiwa huru.
Kutokana na maelezo yote hapo juu, Kamati imeridhia hatua iliyochukuliwa
na Sekretarieti ya TFF ya kumruhusu mchezaji Kevin Yondani kuichezea timu ya
Yanga katika mashindano ya Kombe la Kagame 2012,”
Hiyo ndiyo taarifa ya Mgongolwa, ambayo ilifuatia malalamiko
ya klabu ya Simba dhidi ya Sekretarieti ya TFF kumuidhinisha Yondani kuchezea
Yanga.
Kwa waliokuwa wakifuatilia sakata la mchezaji huyo tangu
mwanzo, wanaweza kuona picha moja kati ya mbili, ama mchezaji huyo ameitapeli
Simba, au Wekundu hao wa Msimbazi wanataka kumfanyia ‘umafia’ beki huyo.
Lakini nani anaweza kuujua ukweli haswa wa sakata hilo,
ikiwa Yondani yupo Yanga na ameikana Simba na wakati huo huo, kila klabu
inaonyesha mkataba iliyosaini naye?
Pagumu hapa. Pendekezo la Kamati ya Mgongolwa kuitaka Simba
iketi chini ya Yondani kurekebisha makosa yaliyopo kwenye mkataba ni sahihi,
lakini je, hilo linawezekana ikiwa mchezaji amekwishaonyesha nia ya kuchezea
Yanga?
Pagumu. Lakini tukumbuke hili si suala geni katika soka ya
Tanzania na Yondani si mchezaji wa kwanza kufanya hivyo- mwaka 1993 kama
sikosei, Mohamed Mwameja akiwa Simba, alisaini Yanga na Kenny Mkapa akiwa Yanga
alisaini Simba, huku kila mchezaji akiwa ndani ya mkataba na klabu yake.
Mwisho wa siku, klabu hizo ziliafikiana kila timu ibaki na
mchezaji wake na yakaisha hivyo na hadi wanstaafu soka wote, hakuna kati yao aliyevaa
jezi ya upande wa pili.
Mwaka 2000, Ephraim Makoye alisaini Simba na kupewa fedha
Sh. Milioni 1.5 wakati huo, mbele ya aliyekuwa Katibu Msaidizi wa klabu hiyo,
Amin Bahroon, sasa marehemu, lakini mwisho wa siku alibaki Yanga, ingawa
baadaye alichezea Wekundu wa Msimbazi.
Victor Costa mwaka 2005 pia alichukua fedha Yanga akaenda
hadi kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi Zanzibar, lakini aliporejea akaenda
kwenye klabu yake, Simba SC.
Athumani Iddi ‘Chuji’ mwaka 2007 alisaini Yanga, huku Simba
ikidai bado ina mkataba naye, na mwisho wa siku akachezea Yanga.
Unaweza kuona haya si mambo mageni na kwa jinsi ambayo
yamekuwa yakimalizwa ‘kwa ujanja ujanja’ imekuwa sababu yanaendelea hata katika
dunia ya soka ya leo, ambayo inalindwa na kanuni, sheria na mifumo madhubuti.
Sasa Simba wanaambiwa wakutane na Yondani kurekebisha
mkataba wao, jambo ambalo TFF wanajua kwa wakati huu haliwezekani na
itakapofika Desemba, muda ambao mkataba wa Yondani na Simba utaanza kufanya
kazi, mchezaji huyo atakuwa bado yupo kwenye mkataba na Yanga.
Saini mbili tofauti za Yondani katika fomu za Simba na Yanga, kwa nini afanye hivi? |
Sasa nani atakuwa na kosa au ile ya kanuni ya kuizuia klabu
kufanya mazungumzo na mchezaji ambaye yupo ndani ya mkataba itatafsiriwa vipi?
Mkataba wa Simba na Yondani unaonyesha mchezaji huyo alisaini kabla ya kwenda
Yanga, lakini utaanza kazi Desemba akiwa ndani ya mkataba na Yanga. Bonge la
sinema.
Lakini swali ambalo tunatakiwa kujiuliza, upuuzi huu
utaendelea kuendekezwa katika soka ya Tanzania hadi lini?
Kwa nini sasa isifike wakati suala hili lichunguzwe kwa kina
na vyombo vya dola vuhusishwe, ili kutafuta ukweli wa jibu sahihi kati ya
mawili, ambayo yanaingia kwenye vichwa vya wengi hivi sasa, yaani aidha Yondani
ametapeli au Simba inaleta ujanja ujanja?
Kama nilivyosema hapo, awali Costa alichukua fedha Yanga,
akabaki Simba kadhalika na Makoye na leo tena Yondani- na bado inaonekana suala
hili litaisha hivi hivi, maana yake desturi hii itaendelea.
Naona kabisa, umefika wakati TFF ikomeshe tabia hii, nidhamu
katika suala la usajili na mikataba izingatiwe. Ili tuondoe uhuni katika soka
ya Tanzania. Kama tutataka kuendekeza ushabiki au kutumia madaraka yetu vibaya,
hakika soka ya Tanzania itaendelea kuwa kichekesho.
Mambo mengi ya kihuni yanazungumzwa kufanyika katika soka ya
Tanzania na inaonekana hata wakubwa wanasikia, lakini wanayachukulia poa tu.
Nini matokeo yake? Tulicheza Fainali za Mataifa ya Afrika kwa mara ya kwanza na
ya mwisho 1980 na mafanikio makubwa katika ngazi ya klabu ni Simba kucheza
fainali ya Kombe la CAF mwaka 1993.
Hivi sasa, tayari hatuna ndoto za kucheza Fainali za Afrika
za mwakani- baada ya kutolewa na Msumbiji na hata tiketi ya Kombe la Dunia
Brazil 2014 unaweza kuona ni ngumu kulingana na hali halisi ya soka yetu kwa
sasa.
Tukifanikikwa kujenga misingi imara ya nidhamu katika soka
yetu, tutangeneza msingi mzuri ya kutafuta mafanikio kama wenzetu. Sasa, je
tuache upuuzi huu uendelee, au tuanze sasa kuufanyia kazi ili kuutokomeza?
Wasalam.
0 comments:
Post a Comment