Sure Boy |
Na Prince Akbar
SALUM Abubakar ‘Sure Boy Jr’ amesema kwamba kama wapo watu wanasema anacheza soka ya nguvu kwa sasa, wanajidanganya, kwani yeye anajiona hajafikia kabisa kiwango anachotaka.
Akizungumza na BIN ZUBEIRY leo, baada ya kuiwezesha Azam kutinga Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, Sure Boy alisema kwamba anashukuru Mungu ndoto zake za awali zimetimia na sasa anafungua ukurasa mpya ili kutimiza ndoto zake zaidi.
“Tangu niko mdogo, nilisema nataka kucheza Ulaya nikikua, lakini kwanza nilitaka nichezee klabu kubwa hapa nyumbani na timu ya taifa. Nadhani utakubaliana nami Azam si timu ndogo, sasa hivi pia mimi ni mchezaji wa timu ya taifa.
Ni wakati mzuri sasa kuanza kufikiria kucheza Ulaya au hata nchi nyingine ya Uarabuni inayolipa vizuri kama Qatar au Saudi Arabia,” alisema mtoto huyo wa winga machachari wa zamani wa Yanga, Abubakar Salum ‘Sure Boy’.
Kwa sasa inaaminika Sure Boy ndiye kiungo bora Afrika Mashariki, ingawa kiwango kilichoonyeshwa na Haruna Niyonzima katika mechi kati ya Yanga na APR jana kinarudisha swali nani bora kati ya wawili hao.
Sure jana aliiongoza Azam kukata tiketi ya kucheza Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame baada ya kuifunga AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kobgo (DRC) mabao 2-1.
Mfungang Alfred alitangulia kuifungia Vita dakika ya 34, baada ya kuunasa mpira uliopigwa na Ibrahim Shikanda na kuichambua ngome ya Azam kabla ya kufumua shuti kali lililomshinda kipa Deo Munishi ‘Dida’.
Vita walipata pigo dakika ya 41, baada ya mchezaji wao, Issama Mpeko kutolewa nje kwa kadi nyekundu ya moja kwa moja.
Azam ilisawazisha bao hilo, kupitia kwa John Bocco ‘Adebayor’ dakika ya 68 aliyeunganisha kwa kichwa krosi ya Kipre Tchetche kutoka wingi ya kulia.
Mrisho Khalfan Ngassa aliyeingia kutokea benchi kipindi cha pili aliifungia Azam bao la ushindi dakika ya 89, akimalizia pasi ya Salum Abubakar ‘Sure Boy’. Baada ya kufunga bao hilo, Mrisho alikwenda moja kwa moja kwan mashabiki wa Yanga na kushangilia nao, badala ya mashabiki wa Azam.
0 comments:
Post a Comment