Azam FC |
Na Prince Akbar
MABINGWA wa Tanzania Simba SC, leo wanatarajiwa kukata utepe
katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame kwa
kumenyana na URA ya Uganda, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Aidha, Azam FC inayoshiriki mashindano hayo kwa mara ya
kwanza, nao watacheza na mabingwa wa Zanzibar, Mafunzo kwenye Uwanja wa
Chamazi, jioni.
Mechi nyingine itakuwa kati ya Vita
Club ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) dhidi ya Ports ya Djibouti.
Lakini kuna tishio au hatihati ya Simba kutoingia uwanjani
leo, kufuatia kuwepo habari za mabingwa hao wa Kombe la Urafiki kutaka kujitoa.
Habari ambazo ziliifikia BIN ZUBEIRY jana usiku
kutoka ndani ya Simba SC, zilisema kwamba uongozi unajadili juu ya uamuzi wa
kushiriki au kutoshiriki mchuano ya Kagame, iliyoanza jana Uwanja wa Taifa
mjini Dar es Salaam.
Kisa nini? Hawana imani na wenyeji wa michuano hiyo,
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) pamoja na Baraza la Vyama vya Soka Afrika
Mashariki na Kati (CECFA). Kivipi? Ni kutokana na kiteno cha vyombo hivyo kumpa
leseni beki wao, Kelvin Patrick Yondan achezee Yanga SC, ambao ni wapinzani wao
wa jadi.
Habari ambazo BIN ZUBEIRY imezipata kutoka ndani
ya Simba SC, zimesema kwamba kitendo cha Yanga kumchezesha Yondan kwenye mechi
yao na Atletivo ya Burundi jana, kimeikera sana Simba na kinahisi kuna hujuma
wanafanyiwa na TFF na CECAFA.
Ikumbukwe Yondan aliyejiunga na Simba 2006, alijiunga na
Yanga mwezi uliopita ingawa klabu yake inaendelea kudai, ina mkataba naye.
BIN ZUBEIRY ilifanikiwa kuwa chombo cha kwanza cha habari
duniani kuonyesha mikataba yote ya Simba na Yanga dhidi ya Yondan.
Lakini Yondan, beki wa kati hodari nchini, mwenyewe hajawahi
hata siku moja kuukana mkataba wowote kati ya hiyo, zaidi ya kusema kujiunga
kwake na Yanga, Simba watajijua wenyewe.
Mwishoni mwa mwaka jana, Yondan alisusa kuchezea Simba na
kuamua kubaki kwao mjini Mwanza, baada ya mechi dhidi Toto African ya mini humo
ya Ligi Kuu.
Na ndipo hapo zilipoanza kuibuka habari za mchezaji huyo
kuhamia kwa watani wa jadi, hadi Mei mwaka huu alipomwaga wino Jangwani.
Ingawa Yondan kwa sasa yupo kwenye kambi ya timu
mpya, Yanga, lakini klabu yake Simba SC imeendelea kusistiza huyo ni mchezaji
wao halali na sasa inafikiria kujitoa kwenye Kagame baada ya Vidic wa Tanzania
kuchezea Yanga kwenye michuano hiyo. Simba SC |
0 comments:
Post a Comment