Kocha wa Simba SC, Mserbia Milovan Cirkovick kushoto, akiwa na bosi wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi ya Simba SC, Ibrahim Masoud 'Maestro' |
Na Prince Akbar
MABINGWA wa Tanzania Bara, Simba SC leo wanafungua dimba na
mabingwa wa Zanzibar, Mafunzo kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar katika michuano
ya Kombe la Ujirani Mwema, inayoandaliwa na Chama cha Soka Zanzibar (ZFA).
Aidha, washindi wa Medali ya Fedha ya Ligi Kuu ya Bara, Azam
FC nao watacheza mechi yao ya ufunguzi dhidi ya timu ya taifa ya vijana chini
ya umri wa miaka 23 ya Zanzibar (U23) kwenye Uwanja huo huo wa Amaan.
Kinara wa mabao wa Azam FC, John Bocco 'Adebayor' |
Mechi kati ya Azam na U23, maarufu kama Karume Boys ndio
itatangulia na mechi ya Simba itafuatia usiku kwenye Uwanja huo huo.
Tayari Azam wapo visiwani Zanzibar tangu jana, wakati
Wekundu wa Msimbazi watapasua mawimbi mchana wa leo kuelekea visiwani humo.
Timu nyingine ya Bara iliyoalikwa kushiriki mashindano hayo,
Yanga SC washindi wa Medali ya Shaba ya Ligi Kuu ya Bara walijitoa, kwa kuhofia
wachezaji wake kuumia kabla ya kuanza Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati,
Kombe la Kagame.
“Mara nyingi tunapokwenda kwenye michuano ya Zanzibar,
wachezaji wetu huumia, hivyo tunahofia hilo lisijitokeze tena wakati tuna wiki
mbili tu kabla ya kuanza kutetea Kombe la Kagame,” alisema wiki iliyopita,
Ofisa Habari wa Yanga, Louis Sendeu akitoa tamko la klabu hiyo kujitoa.
Wakati michuano ya Ujirani Mwema ilianza jana visiwani
Zanzibar, Kombe la Kagame linatarajiwa kuanza Julai 14, Yanga ikifungua dimba
na Atletico ya Burundi.
Timu nyingine katika Kundi A mbali na Simba ni Azam, Mafunzo
na U23.
0 comments:
Post a Comment