Na Princess Asia
BINGWA wa Ligi Kuu ya Bara, Simba SC leo atakuwa na mtihani
mzito mbele ya washindi wa pili wa ligi hiyo, Azam FC katika mchezo wa Robo
Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, Uwanja wa
Taifa, Dar es Salaam.
Mchezo huo wa Robo Fainali, unazikutanisha timu hizo wiki
mbili tangu zikutane kwenye Fainali ya Kombe la Urafiki, ambayo Simba ilishida
kwa penalti 3-1, kufuatia sare ya 2-2 ndani ya dakika 90.
Katika mchezo huo, mshambuliaji wa kimataifa wa Zambia,
Felix Sunzu alitangulia kuifungia Simba dakika ya 29 kabla ya Hamisi Mcha
‘Vialli’ kusawazisha dakika ya 45 na ushei.
Kipindi cha pili mchezo ulichangamka zaidi na dakika ya 81,
John Bocco ‘Adebayor’ aliyetokea benchi aliifungia Azam bao la pili, kabla ya
Kazimoto kuisawazishia Simba kwa penalti dakika ya 87, baada ya Danny Mrwanda
kuangushwa kwenye eneo la hatari.
Penalti za Simba zilikwamishwa nyavuni na Mwinyi Kazomoto,
Amir Maftah na Kiggi Makassy, wakati Haruna Moshi Boban alipaisha na kwa upande
wa Azam FC, aliyefunga ni Hamisi Mcha ‘Vialli’ pekee, wakati Samir Hajji Nuhu,
Ibrahim Mwaipopo na Himid Mao walikosa.
Katika siku za karibuni, Simba na Azam zinaonekana kuchuana
vikali, kwani mbali na Azam kuwa wa pili ya nyuma kwenye Kombe la Urafiki, hata
kwenye Ligi Kuu walifuata hivyo hivyo
Simba imefuzu Robo Fainali kama mshindi wa tatu kwenye Kundi
A, ikivuna pointi nne, kutokana na kufungwa mechi moja (2-0 dhidi ya URA),
kushinda moja dhidi ya Ports ya Djibouti na sare moja dhidi ya AS Vita ya
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Azam yenyewe imefuzu kama kinara wa Kundi B, lakini herufi
tu, kwani timu zote za Kundi hilo zililingana kwa pointi, mbili kila moja na
kutokana na sare katika mechi zote (1-1 Azam na Mafunzo, 0-0 Mafunzo na Tusker,
0-0, Azam Tusker na 0-0 Mafunzo na Tusker).
Mchezo wa leo, utatanguliwa na Robo Fainali nyingine kati ya
Atletico ya Burundi AS Vita ya DRC.
Habari za ndani kutoka Azam zinasema kwamba viongozi wa
klabu hiyo wametoa angalizo kwa TFF (Shirikisho la Soka Tanzania) na CECAFA
(Baraza la Vyama Soka Afrika Mashariki) wanataka haki itendeke kwenye mechi
hiyo.
Kiongozi mmoja wa juu wa Azam, ambaye hakupenda kutajwa
jina, alisema kuna desturi ya Simba na Yana kubebwa kwenye mashindano ili
zicheze fainali na CECAFA na TFF watimize ndoto zao za kukusanya mapato mengi milangoni, lakini wanaomba
desturi hiyo leo iwekwe kando.
“Sisi Azam tuko tayari kuaga kwenye mashindano bila ya
malalamiko na kuchukua ilikuwa hali mchezo, lakini kama tutaona dalili zozote
za wapinzani wetu kupendelewa, tutachukua hatua,”alisema.
0 comments:
Post a Comment