Lino Masombo, beki wa Simba SC |
Na Prince Akbar
KLABU za Simba na Azam zitakazomenyana katika fainali ya
Kombe la Urafiki kesho saa 1:00 usiku Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam tayari
zimerejea Jijini kutoka visiwani Zanzibar walipocheza hatua za awali za
michuano hiyo, inayoandaliwa na Chama cha Soka Zanzibar (ZFA).
Timu zote zilirejea Dar es Salaam saa 12 jioni na kuelekea
kwenye kambi zao, tayari kwa maandalizi ya mchezo huo.
Daktri wa Simba SC, Cossmas Kapinga ameiambia BIN
ZUBEIRY asubuhi ya leo kwamba, amefurahia mechi hiyo kurejeshwa Dar es Salaam,
kwani kwa Uwanja Amaan kutokana na jinsi ulivyo mbovu, kulikuwa kuna hatari ya
wachezaji wake kuumia zaidi.
“Kila mchezaji katika timu yetu, analalamika anaumwa kifundo
cha mguu, ila ni maumivu madogomadogo na wote wanaendelea na mazoezi, lakini
kwa mchezo mkubwa kama huo ilikuwa ni hatari sana, maana kwanza wangecheza kwa woga
na wangeweza kuumia zaidi, ukizingatia kila timu inaingia kwenye Kombe la Kagame,”alisema
Dk Kapinga.
Simba wanatarajiwa kufanya mazoezi mepesi kwenye Uwanja wa
TCC, Chang’ombe, Dar es Salaam jioni ya leo, wakati Azam watajifua uwanjani
kwao, Chamazi.
Fainali ya Kombe la Urafiki baina ya timu hizo, sasa
itachezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Alhamisi na itasimamiwa na kampuni ya
Prime Time Promotions, wamiliki wa Clouds Media Group.
Msemaji wa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA), Munir Zakaria aliiambia
BIN
ZUBEIRY jana kwamba mazungumzo yanaendelea kuhusu mustakabali wa mechi
hiyo, lakini kwa sasa jukumu la promosheni ya mechi wamekabidhiwa Prime Time.
Munir alisema sababu za mechi hiyo kuhamishiwa Dar es Salaam
ni kwamba Simba na Azam zimeukataa Uwanja wa Amaan kwamba ni mbovu na wachezaji
wake wanaumia.
Mapema jana, kocha wa Azam FC, Stewart Hall kutoka Uingereza
alisema ana matumaini ya kuwafunga Simba SC kwenye fainaili, wakati mpinzani
wake Mserbia Profesa Milovan Cirkovick alimjibu kwamba anajidanganya.
Nyota wa Azam; Abdi Kassim 'Babbi' na Abdulhalim Humud |
Stewart alisema baada ya ushindi wa 2-0 jana dhidi ya
mabingwa wa Zanzibar, Super Falcon na kutinga fainali, sasa ni zamu ya mabingwa
wa upande wa pili wa Muungano, Simba SC nao kula kichapo.
Lakini Stewart alikiri kwamba Simba, mabingwa wa Bara ni
timu nzuri na mchezo utakuwa wa ushindani, lakini mwisho wa siku, Azam
watang’ara.
Stewart alisema wachezaji wake aliowapa mapumziko kama
Mrisho Khalfan Ngassa na John Raphael Bocco ‘Adebayor’ wataendelea kuwa
watazamaji, kwani ataendelea na kikosi kile kile kilichomfikisha hapa.
Kwa upande wake, Milovan alisema tangu wanapanda boti kwenda
Zanzibar alijua tu fainali itakuwa kati ya timu yake na Azam kwa sababu hizo
kwa sasa ndizo timu bora Tanzania.
“Sisi mabingwa, wao wa pili kwenye Ligi, hao ndio wapinzani
wetu. Hatuwezi kuukwepa ukweli huo. Ila wataendelea kuwa wa pili hata baada ya
dakika 90,”alisema Milovan.
Milo alisema amewaona Azam wakicheza Zanzibar na anakiri ni
timu nzuri, lakini ya kiwango cha kuisumbua tu Simba SC si kuizuia kushinda.
Azam walikuwa wa kwanza juzi kujikatia tiketi ya kuingia
fainali, baada ya kuifunga Falcon 2-0, mabao yote yakitiwa kimiani na
mshambuliaji wa kimataifa wa Ivory Coast, Kipre Herman Tcheche Uwanja wa Amaan,
Zanzibar.
0 comments:
Post a Comment