Kipa wa Express, Didi Mahmoud akidaka mpira Uwanja wa Taifa jana. |
Kumekuwa na malalamiko juu ya kuharibika kwa miundo mbinu mbalimbali licha ya uongozi wa uwanja kuchukua mapato makubwa mechi.
Wadau wa soka wanakumbuka kukatika kwa umeme wakati wa mechi ya fainali ya Kombe la Kagame kati ya Simba na Yanga mwaka jana.
Tukio lile lilitokea mbele ya aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Dk. Emmanuel Nchimbi.
Haikuwa mara ya kwanza kwa matukio ya kufedhehesha kutokea wakati wa mechi zinazochezwa katika Uwanja wa Taifa.
Kuna matukio ya aibu yalishatokea tena mbele ya Rais Jakaya Kikwete. Kila mdau wa soka anakumbuka jinsi wimbo wa Taifa wa Tanzania ulivyokwama kupigwa kwenye mechi dhidi ya timu ya taifa ya Morocco, mbele ya Rais Kikwete.
Pia wimbo wa Taifa ulipigwa kwa matatizo wakati wa mechi za kirafiki dhidi ya Brazil na New Zealand.
Matatizo mengine ya uwanja huo ni pamoja na udhibiti mbovu wa mapato na pia hakuna hata sehemu ya kukaa waandishi wa habari.
Ukiangalia hali ya vyoo ni mbaya, kuna mabomba kadhaa ya maji yamevunjwa na baadhi ya viti navyo vimevunjwa.
Haya yote yanatokea wakati timu zinapochezea katika uwanja ule zimekuwa zikilia na makato makubwa yanayochukuliwa na viongozi wa uwanja wakati utunzaji wake ni mbovu.
Kwa ujumla usimamizi wa uwanja ni dhaifu kiasi ambacho kama serikali isipokuwa makini utachakaa muda si mrefu.
Haya yanasababishwa na ombwe la uongozi la uwanja huo na cha kushangaza serikali imekuwa ikifumbia macho suala hilo wakati wale waliopewa dhamana ya kusimamia uwanja ule wamefeli.
Lilipotokea tatizo la Wimbo wa Taifa iliundwa tume ya kuchunguza na ikaja na mapendekezo yake.
Pia Waziri Nchimbi aliunda tume nyingine baada ya tatizo la umeme, ambayo pia iliomba masuala kadhaa kufanyiwa kazi.
Serikali inapaswa kufanya tathmini ya kisayansi juu ya uendeshaji kwa ufanisi wa uwanja huu.
Usimamizi wa uwanja sio suala la kuteuana kwa kujuana, bali linahitaji utaalamu katika utendaji wake na ndiYo maana tunasema watafutwe watu wenye ujuzi wa kusimamia uwanja.
Unahitajika utaalamu wa masuala ya maeneo ya kuchezea, kuna vipimo vya mchezo wa riadha, mpira wa wavu, mpira wa kikapu n.k.
Katika miaka ya nyuma serikali ilikuwa na utaratibu wa kusomesha wataalamu wa fani za michezo.
Kwa mfano katika miaka ya 1970, serikali ilimsomesha mtaalamu wa viwanja, ambaye anatambuliwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), Mohammed Ali Madenge, ambaye kwa sasa anasaidia kusimamia Uwanja wa timu ya Azam.
Sasa tangu serikali imeacha kusomesha wataalamu wa fani mbalimbali za michezo na kusababisha kutokea kwa ombwe la wasimamzi wa viwanja, matokeo yake tunashuhudia kuchakaa kwa viwanja mbalimbali kama vile vya Sokoine mjini Mbeya, Majimaji mjini Songea na Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora.
Ndiyo maana wito wetu ni kuwa kama serikali haina watu waliobobea kusimamia uwanja basi itafute mkandarasi mwenye sifa na uzoefu ili kuepusha uwanja huo kuchakaa haraka.
SOURCE: GAZETI LA MWANASPOTI
0 comments:
Post a Comment