Nurdin Bakari |
Na Prince Akbar
WACHEZAJI 17 wa timu ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya
miaka 17 (Serengeti Boys) wamefanyiwa vipimo vya kubaini umri wao halisi (MRI
Tests) kwenye hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam.
Upimaji huo ulifanyika Julai 14 mwaka huu chini ya usimamizi
wa mjumbe wa Kamati ya Tiba ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Dk. James
Sekajugo kutoka Uganda na Mwenyekiti wa Kamati ya Tiba ya TFF), Dk. Sylvester
Faya.
Dk. Sekajugo alisema vipimo hivyo vya Magnetic Resonance
Imaging (MRI) vinafanya kutokana na maelekezo ya CAF kwa nchi zote ambazo
zitashiriki mashindano ya U17 ambayo fainali zake zitafanyika mwakani nchini
Morocco ili kubaini umri halisi wa wachezaji hao.
Dk Sekajugo amesema vipimo vya MRI havina madhara kama
ilivyo kwa X-ray ambapo vyenyewe vinachunguza uimara wa mifupa ili kubaini umri
halisi wa mchezaji, na uwezo wake ni kubaini watu walio chini ya umri wa miaka
17.
Amesema CAF imeamua vipimo hivyo vifanyike kabla ya
wachezaji kuingia kwenye mashindano kwani Afrika inakabiliwa na tatizo sugu la
kudanganya umri wa wachezaji.
“Naipongeza TFF kwa kuhakikisha upimaji unafanyika kama
ilivyoagizwa na CAF. Wakati mwingine si udanganyifu, unajua katika Afrika
hakuna utaratibu wa watoto kuandikishwa wanapozaliwa. Hivyo inawezekana kabisa
mtoto au mzazi wake hakumbuki au hajui tarahe aliyozaliwa,” amesema Dk.
Sekajugo.
Uamuzi wa CAF kufanya vipimo vya MRI kabla ya wachezaji
kuanza mashindano umelenga kuhakikisha wachezaji wanaoshinda wana umri sahihi,
badala ya vipimo hivyo kufanyika wakati wa fainali.
“Mwaka 2005 CAF iliamua kufanya vipimo hivyo miezi miwili
kabla ya kuanza michuano ya fainali. Kuna timu moja ilikutwa wachezaji wake
wote wamezidi umri, hivyo ikabidi waunde timu mpya,” amesema Dk. Sekajugo na
kuongeza kuwa matokeo ya vipimo vya wachezaji wa Serengeti Boys vitatumwa baada
ya wiki mbili.
Naye Dk. Faya ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya
TFF amesema wachezaji 10 waliobaki watafanyiwa vipimo hivyo baadaye kabla ya
mechi ya michuano hiyo CAF dhidi ya Kenya itakayochezwa Septemba mwaka huu.
Wachezaji tisa wako nchini Burundi kwenye michuano ya
Rolling Stone Multipurpose Acre Foundation wakati mmoja (Dickson Ambundo)
amekwenda Ujerumani na timu ya TASC ya Mwanza.
Walioko Burundi ni Hamad Juma, Mgaya Jaffar, Ismail Gambo,
Mohamed Hussein, Hussein Ibrahim, Mudathir Abbas, Farid Shah, Joseph Lubasha na
Kelvin Friday.
Dk. Faya amesema vipimo vya MRI kupanywa mapema ni vizuri
kwa sababu tatizo la udanganyifu wa umri lipo, lakini pia litaisaidia TFF kwani
inatumia gharama kubwa kuandaa timu, hivyo ni vizuri ikaandaa timu ya wachezaji
wenye umri sahihi badala ya waliodanganya umri ambao hawataruhusiwa kushiriki
mashindano.
Mwaka 2005 Serengeti Boys ilifuzu kucheza fainali za Afrika
zilizofanyika Banjul, Gambia lakini ilinyang’anywa nafasi hiyo baada ya
kubainika kuwa baadhi ya wachezaji wake walikuwa wamezidi umri wa miaka 17.
0 comments:
Post a Comment