Amir Maftah |
Na Prince Akbar
BEKI wa kushoto wa Simba SC, Amir Maftah ameuvunjika kidole
cha mwisho cha mkono wa kulia na sasa hataweza kuendelea na michuano ya Klabu
Bingwa ya soka Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, kwani anatakiwa kuwa
nje ya Uwanja kwa wiki mbili.
Ofisa Habari wa Simba SC, Ezekiel Kamwaga ameaimbia BIN
ZUBEIRY mchana huu kwamba, beki huyo anayeweza kucheza kama kiungo pia,
aliumia kwenye mechi ya Kundi A, Kombe la Kagame jana dhidi ya Ports ya
Djibouti, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kuumia kwa beki huyo ni pigo kwa Simba SC katika kampeni
zake za kuwania taji la saba la michuano hiyo, kwani amekuwa tegemeo la timu mbele
ya kocha Mserbia, Milovan Cirkovick, kiasi cha kufikia kutemwa kwa beki
mwingine wa nafasi hiyo, Juma Jabu.
Pamoja na kuumia wakati mchezo ukiendelea, lakini Amir,
aliyejiunga na Simba miaka mitatu iliyopita akitokea kwa watani wa jadi, Yanga
alionyesha ujasiri kwa kumaliza dakika zote 90, mabingwa hao wa Tanzania Bara, wakiichapa
Ports mabao 3-0 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Shujaa wa Simba katika mchezo huo, alikuwa mshambuliaji mpya
kutoka Ruvu Shooting ya Pwani, Abdallah Juma aliyeingia kuchukua nafasi ya Amri
Kiemba mwanzoni mwa kipindi cha pili aliyefunga mabao mawili dakika za 60 na 73
na Felix Mumba Sunzu Jr. aliyefunga moja kwa penalti dakika ya 64
Dakika 45 za kipindi cha kwanza zilimalizika bila nyavu za
Ports kutikisika, na katika kipindi hicho Sunzu, mshambuliaji wa kimataifa wa
Zambia, alipoteza nafasi tatu za wazi mno, za kufunga mabao akiwa amebaki yeye
na kipa, Kalid Ali Moursal.
Mabadiliko yaliyofanywa na kocha Mserbia, Milovan Cirkovick
kipindi cha pili kuwaingiza Juma Nyosso kuchukua nafasi ya Haruna Shamte,
Abdallah Juma aliyechukua nafasi ya Kiemba na baadaye Uhuru Suleiman kuchukua
nafasi ya Haruna Moshi ‘Boban’ yaliisaidia Simba.
Kwa matokeo hayo, Simba imefikisha pointi tatu baada ya
kucheza mechi mbili na sasa inashika nafasi ya tatu kwenye Kundi A, nyuma ya
URA yenye pointi sita na AS Vita yenye pointi tatu na wastani mzuri wa mabao.
Simba itamaliza na AS Vita ya DRC, mechi ambayo itakuwa kali kwa sababu timu
zote zina pointi sawa.
Kikosi cha Simba jana kilikuwa; Juma Kaseja, Haruna
Shamte/Juma Nyosso, Amir Maftah, Shomary Kapombe, Haruna Moshi ‘Boban’/Uhuru
Suleiman, Mussa Mudde, Felix Sunzu, Amri Kiemba/Abdallah Juma, Mwinyi Kazimoto,
Lino Masombo na Kanu Mbivayanga.
Katika mchezo wa awali uliotangulia wa kundi hilo, URA ya
Uganda, ilikuwa timu ya kwanza kufuzu Robo Fainali ya baada ya kuichapa mabao
3-1, AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam jioni hii.
Mabao ya URA yaliwekwa kimiani na Sula Bagala mawili na
Robert Ssentongo, wakati la kufutia machozi la Vita, inayofundishwa na kocha w
zamani wa Yanga, Raul Jean Pierre Shungu lilifungwa na Mutombo Kazadi.
MSIMAMO WA KUNDI A
ULIVYO SASA:
P W D L GF GA GD Pts
URA 2 2 - - 5 1 4 6
AS Vita 2 1 - 1 8 3 5 3
Simba 2 1 - 1 3 2 1 3
Ports 2 - - 2 - 7 -7 -
0 comments:
Post a Comment