Kaburu akiwaonyesha Waandishi mkataba wa Okwi na Simba |
Mkataba wa Okwi na Simba |
Soma vipengele hapo |
Kaburu akizungumza na Waandishi wa Habari |
Kaburu akiwasikiliza sauti ya Okwi waandishi |
Hapa anafunguka kwa hisia kali |
Na Prince Akbar
WAKATI Mshambuliaji Emmanuel Okwi amekanusha kusaini Yanga, uongozi wa klabu yake, Simba umesikitishwa na habari
zilizovumishwa kwenye vyombo vya habari kuhusu mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Uganda kujiunga na wapinzani wa jadi, Yanga SC.
Akizungumza na Waandishi wa Habari mchana wa leo, makamo
makuu ya klabu Mtaa wa Msimbazi, Dar es Salaam, Makamu Mwenyekiti wa Simba,
Geoffrey Nyange ‘Kaburu’, alisema kwamba habari hizo hazina ukweli wowote, ni
kinyume cha maadili ya taaluma ya uandishi wa habari na zina lengo la kupotosha
ukweli na kuwanyima raha wale wote wenye mapenzi mema na Simba.
“Gazeti kama la Spoti STAREHE limekwenda mbali zaidi kwa
hatua yake ya kutaka kuufitinisha uongozi na wapenzi na wanachama wake kwa
kudai kuwa uongozi unafikiria tu kumuuza Okwi bila ya kuangalia mkataba wake.
Kwa mujibu wa gazeti hilo, mkataba wa Okwi umemalizika leo
na ndiyo maana ameamua kusaini Yanga akiwa mchezaji huru,”alisema Kaburu na
kuongeza;.
“Ukweli ulivyo. Emmanuel Okwi alisaini mkataba mpya wa
kuichezea Simba mnamo mwaka jana na mkataba huo unamfanya kuwa mchezaji halali
wa klabu yetu hadi mwaka 2013. Baada ya mkutano huu, nitawaonyesha waandishi
nakala ya mkataba wa Okwi na Simba. Hivyo taarifa kwamba mchezaji huyo hana
mkataba na Simba ni za uongo, uongo mtupu,”alisema.
“Hivi ninavyozungumza nanyi, Okwi yuko kwao nchini Uganda
akishughulikia viza ya kwenda nchini Italia ambako anatarajiwa kufanya
majaribio ya kucheza soka la kulipwa katika moja ya vilabu vya Ligi Kuu ya
Italia (Serie A),”alisema Kaburu.
Okwi |
Aidha, alisema uongozi wa Simba SC unavitaka vyombo vya
habari vilivyoripoti kuhusu Okwi kuhamia Yanga (gazeti la Bingwa na lile la
Spoti STAREHE) kuomba radhi katika kipindi cha siku saba kuanzia leo la sivyo
uongozi utachukua hatua kali za kisheria dhidi yao.
“Tayari tumewasiliana na mwanasheria wa klabu ambaye
ameelekeza kwamba ni lazima vyombo hivyo viombe radhi na viuambie umma kwamba
vilisema uongo na vinajutia kosa hilo la kimaadili na habari hiyo itoke katika
ukurasa wa mbele katika namna ileile ambayo habari ya leo ilitoka.
Pia, uongozi wa Simba unaviomba vyombo vya dola vichunguze
ni nani anahusika na usambazwaji wa taarifa hizi kwenye simu na vyombo vya
habari kwani zina hatari ya kuchafua hali ya amani na utulivu nchini,”alisema.
Aidha, Kaburu alimpigia simu Okwi na kuzungumza naye huku akiwasikilizisha
Waandishi wa Habari. Katika mazungumzo hayo, alisema hana mpango wa kusaini
Yanga na kwa sasa yuko kwao Uganda akifuatilia visa ya kwenda Italia ndani ya
siku mbili hizi, ambako anatakiwa na klabu ya Parma ya Serie A.
“Akili yangu kwa sasa ni kucheza Ulaya, na hata kama
nitakosa nafasi Italia, basi kama ni kurudi Tanzania, basi nitaendelea kucheza
Simba siyo Yanga,”alisema Okwi katika mazungumzo yake na Kaburu kwa simu kutoka
Uganda.
Mbali na Parma, Okwi pia anatakiwa na Etoile du Sahel ya
Tunisia, Mamelodi Sundown na Orlando Pirates za Afrika Kusini.
0 comments:
Post a Comment