Juma Nyosso |
Na Princess Asia
BEKI wa Simba SC, Juma Said Nyosso amesaini mkataba wa mwaka
mmoja kuendelea kuichezea klabu hiyo, baada ya mkataba wake awali kumalizika,
hivyo kumaliza tetesi kwamba anaweza kuhamia kwa watani wa jadi, Yanga SC.
Makamu Mwenyekiti wa Simba SC, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’
ameiambia BIN ZUBEIRY mchana wa leo kwamba, Nyosso alisaini mkataba huo
Julai 1, mwaka huu.
Kaburu alisema kwamba Simba ina imani na beki huyo wa timu
ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars na ndio maana imemuongezea mkataba.
Aidha, Kaburu aligusia suala la beki wao, Kelvin Yondan
aliyehamia kwa watani wa jadi, Yanga akisema kwamba bado ni mchezaji wao halali
na wamekwishapeleka malalamiko yao Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), wanasubiri
majibu.
Kaburu pia amesema mshambuliaji wa kimataifa wa Zambia,
Felix Sunzu tayari amejiunga na wenzake kambini visiwani Zanzibar, ambako timu
hiyo inashiriki Kombe la Urafiki.
Kaburu amesema Simba itaendelea kuwa Zanzibar hata baada ya
michuano hiyo, wakijiandaa na Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la
Kagame, ambalo linatarajiwa kuanza kutimua vumbi Julai 14, Simba wakifungua dimba
na URA ya Ugandea Julai 16.
0 comments:
Post a Comment