Nizar Khalfan |
Na Prince Akbar
KIUNGO wa kimataifa wa Tanzania, Nizar Khalfan aliyesajiliwa
na Yanga msimu huu, atakuwa nje ya Uwanja kwa wiki sita baada ya kuumia nyonga katika
mfululizo wa michuano ya Klabu Bingwa ya soka Afrika Mashariki na Kati, Kombe
la Kagame inayofikia tamati leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, tangu ianze
Julai 14, mwaka huu.
Kocha wa Yanga, Mbelgiji Tom Saintfiet ameiambia BIN
ZUBEIRY jana kwamba Nizar alionyesha dalili za kupona mapema awali,
lakini sasa imegundulika anatakiwa kuwa nje ya Uwanja kwa wiki zisizopungua sita.
Kwa masikitiko makubwa, Tom alisema; “Nizar hatacheza
fainali, alionekana kuwa vizuri siku chache zilizopita, sasa atakuwa nje kwa
wiki zisizopungua sita,”alisema.
Tayari Nizar amekosa mechi mbili za Robo Fainali na Nusu
Fainali ya michuano hiyo, licha ya kuanza vizuri katika hatua ya makundi.
Kiungo huyo alisajiliwa na Yanga miezi miwili iliyopita akitokea Philadelphia
Union ya Ligi Kuu ya Marekani (MLS), ambayo alijiunga nayo kutoka Vancouver
Whitecaps ya Canada, ambayo ilikuwa inacheza MLS.
Maana yake, Nizar ambaye tayari ana ofa ya kwenda kucheza
Qatar, atakosa hadi mechi za mwanzoni mwa msimu ujao wa Ligi Kuu ya Bara na
kama Yanga itakubali kushiriki michuano mipya ya timu nane, nne za Bara na nne
Visiwani, Bank ABC Super8 Tournament pia kiungo huyo hatacheza.
Uchunguzi unaonyesha kuumia kwa wachezaji wengi wa klabu za
Tanzania mwanzoni mwa msimu kunatokana na kukosa mazoezi ya kutosha kabla ya msimu
na kucheza mechi za karibu karibu- mfano za Kombe la Kagame.
Mbali na Nizar, kwa Yanga wachezaji wengine ambao ni
majeruhi ni kipa Yaw Berko na beki Juma Abdul, wakati wachezaji wengine
wanaendelea kucheza wakiugulia maumivu.
0 comments:
Post a Comment