Mtakatifu Tom, akiwa na Kombe la Kagame |
Na Prince Akbar
KOCHA wa Yanga, Mbelgiji Tom Saintfiet amesema kwamba aliwaelekeza
vijana wake kucheza kwa kutotumia nguvu nyingi katika mchezo wa jana dhidi ya
Mafunzo, kwani alijua watakuwa na mechi nyingine ngumu baada ya siku moja
katika Nusu Fainali.
Akizungumza na BIN ZUBEIRY baada ya mechi ya Robo
Fainali dhidi ta Mafunzo ya Zanzibar jana, Mtakatifu Tom alisema kwamba vijana
wake wamecheza kwa kufuata maelekezo yake na hakutaka ushindi mkubwa jana, bali
ushindi tu.
Hata hivyo, anasikitika kuumia kwa kipa wake namba moja,
Mghana Yaw Berko katika mchezo huo, kwani kunaiathiri timu yake.
“Wachezaji wanaumia sana kwa sababu mechi zipo karibu karibu
mno, hakuna jinsi zaidi ya kuendelea kukabiliana na hali hii,”alisema.
Aidha, Tom alisema kwamba hakupenda kabisa kukutana tena na
APR katika Nusu Fainali kwa sababu amekwishakutana nao kwenye kundi lake, C
zaidi alitarajia changamoto mpya kutoka URA ya Uganda.
“Lakini kwa kuwa tupo kwenye mashindano, tunakabiliana na
timu yoyote. Nawaheshimu APR, ni timu nzuri na hatukuwafunga kwa urahisi kwenye
mechi ya kwanza, utakuwa mchezo mgumu sana,”alisema Tom.
Yanga jana imefuzu kuingia Nusu Fainali ya Kombe la Kagame, baada
ya kuifunga Mafunzo ya Zanzibar kwa penalti 5-3, kufuatia sare ya 1-1 ndani ya
dakika 90 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Wawakilishi wa Zanzibar Mafunzo walikuwa wa kwanza kupata bao
lililofungwa na Ali Othman Mmanga, dakika ya 34, akiunganisha kona ya Juma
Othman Mmanga na Yanga wakasawazisha dakika ya 46, mfungaji Said Bahanuzi
‘Spider Man’.
Yanga sasa kesho itamenyana na APR ya Rwanda, ambayo katika
Robo Fainali ya kwanza, iliitoa URA ya Uganda kwa kuifunga mabao 2-1, mabao
yake yakifungwa na Jean Claude Iranzi dakika ya tisa na Suleiman Ndikumana
dakika ya 34, wakati la Watoza Ushuru wa Kampala, lilifungwa na Robert
Ssentongo dakika ya 57.
Kipa wa Yanga Berko aliumia dakika ya 69 na akatibiwa kwa
dakika tatu, kabla ya kutolewa nje dakika ya 72, nafasi yake ikichukuliwa na
Ally Mustafa Barthez ambaye ukaaji wake mazuri langoni wakati wa penalti
ulimfanya Said Mussa Shaaban wa Mafunzo akapiga nje na kuipa Yanga ushindi.
Nyota wa Mafunzo, Juma Othman Mmanga alipoteza
fahamu na kuwaweka roho juu wachezaji wenzake na mashabiki, akatolewa nje
akipepewa na hakuweza kuendelea na mchezo, lakini taarifa za baada ya mchezo
zilisema anaendelea vizuri.
0 comments:
Post a Comment