Azam wakijinoa |
Na Prince Akbar
FAINALI ya
Kombe la Urafiki, michuano inayoandaliwa na Chama cha Soka Zanzibar (ZFA),
inachezwa leo kuanzia saa 1:00 usiku Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam
ikizikutanisha bingwa wa Ligi Kuu Simba SC na mshindi wa pili wa ligi hiyo ya
Bara, Azam FC.
Hatua ya awali
ya michuano hii, ilifanyika visiwani Zanzibar, lakini kutokana na timu zote za
Bara kuingia fainali, makubaliano yalifikiwa kwa sababu za msingi, mechi ya
mwisho ya michuano hiyo ifanyike Dar es Salaam.
Timu zote
zililalamikia eneo la kuchezea mpira (pitch) la Uwanja wa Amaan kwamba ni baya
na linasababisha wachezaji kuumia, hiyo ikawa sababu ya leo watu kuelekea
Taifa.
Timu zote
zilirejea Dar es Salaam juzi jioni na kuelekea kwenye kambi zao kwa maandalizi
ya mwisho mwisho kabla ya kuibukia Taifa usiku wa leo.
Kocha wa Azam, Stewart Hall |
Kwa sasa,
upinzani katika soka ya Tanzania upo kwa Simba na Azam ambao waligombea ubingwa
wa Ligi Kuu msimu uliopita na ndio watakaoiwakilisha nchi kwenye michuano ya
Afrika mwakani.
Simba ni
timu kongwe yenye mashabiki mamilioni na leo maelfu ya mashabiki wake watakuwa
uwanjani kuishangilia timu yao, lakini Azam japo ni timu changa na haina
mashabiki wengi, itanufaika na utamaduni wa upinzani wa jadi katika soka ya
Tanzania kwa maelfu ya mashabiki wa Yanga kuwapa sapoti leo.
Kwa sababu
hiyo, suala la msisimko kwenye mchezo wa leo, halina mjadala- utakuwa wa hali
ya juu sana.
Simba iliyoanzishwa
zaidi ya miaka 70 iliyopita, ndio timu bora Tanzania hadi sasa, ikiwa imeweka
rekodi ambazo hazijafikiwa na klabu nyingine nchini, wakiwemo wapinzani wao wa
jadi, Yanga- kufika fainali ya Kombe la CAF 1993 na kufika Nusu Fainali ya
Klabu Bingwa Afrika 1974.
Kocha wa Simba, Profesa Milovan Cirkovick |
Simba pia
inaifuatia Yanga kwa kubeba ubingwa wa Ligi Kuu, ikiwa imetwaa mara 17, katika
miaka ya 1966, 1973, 1976, 1977, 1978, 1979, 1980, 1984, 1990, 1994, 1995,
2001, 2003, 2004 na 2007 (Ligi Ndogo),
2010 na 2012. Yanga imechukua mara 22 katika miaka ya 1968, 1969, 1970, 1971,
1972, 1974, 1981, 1983, 1985, 1987, 1991, 1992, 1993, 1996, 1997, 1998, 2002,
2005, 2006, 2008 na 2009 na 2011.
Hadi sasa,
Azam iliyoanzishwa mwaka 2004 na kupanda Ligi Kuu mwaka 2008, ina taji moja tu,
ambalo ni Kombe la Mapinduzi ililolitwaa Januari 16, mwaka huu kwa kuifunga
Jamhuri ya Pemba mabao 3-1 kwenye fainali, katika michuano ambayo ilivitoa vigogo
Simba na Yanga kabla ya kupata tiketi ya kucheza mechi ya mwisho Uwanja wa
Amaan, Zanzibar.
Simba
iliingia fainali baada ya kuifunga Zanzibar All Stars 1-0, bao pekee la kiungo
wake mpya kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Patrick Kanu
Mbivayanga, wakati Azam iliifunga Super Falcon 2-0, mabao ya mshambuliaji wake kutoka
Ivory Coast, Kipre Herman Tcheche.
Katika mchezo
wa leo, Haruna Moshi ‘Boban’ anaweza kuanzia benchi akitangulia Mbivayanga,
wakati upo uwezekano chipukizi Abdallah Juma akaanza sambamba na Mussa Mudde,
Mwinyi Kazimoto na Salim Kinje.
Kwa Azam,
huenda mfungaji bora wa Ligi Kuu, John Bocco ‘Adebayor’ akapewa jezi kufuatia
Gaudence Mwaikimba kuwa anatumikia adhabu ya kadi nyekundu aliyopewa kwenye
Nusu Fainali, wakati Mrisho Ngassa anaweza kutokea benchi sambamba na Abdulhalim
Humud.
Makocha wa
timu hizo, Muingereza Stewart Hall wa Azam FC na Mserbia Profesa Milovan
Cirkovick wote walitambiana jana kwamba kila mmoja ana matumaini ya kubeba
Kombe hilo, ambalo bingwa atajinyakulia zawadi ya Sh, Milioni 10 na
atakayefungwa atapata kifuta jasho cha Sh. Milioni 5.
Azam na
Simba zitakazocheza pia Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati sambamba na Yanga
kuanzia mwishoni mwa wiki hii mjini Dar es Salaam, zitafungua pia pazia la Ligi
Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kwa kucheza mechi ya Ngao ya Jamii mwezi ujao.
Katika
mchezo wa leo, kikosi cha Simba kinatarajiwa kuwa; Juma Kaseja, Shomary
Kapombe, Amir Maftah, Lino Masombo, Juma Nyosso, Amri Kiemba, Mwinyi Kazimoto,
Mussa Mudde, Abdallah Juma, Kanu Mbivayanga na Salim Kinje.
Azam; Deo
Munishi ‘Dida’, Samir Hajji Nuhu, Ibrahim Shikanda, Said Mourad, Joseph Owino,
George Odhiambo ‘Blackberry’, Ibrahim Mwaipopo, Kipre Michael Balou, Ramadhan
Chombo ‘Redondo’, John Bocco ‘Adebayor’ na Kipre Herman Tcheche.
Simba wakijifua |
REKODI YA SIMBA NA AZAM LIGI KUU:
Februari 11, 2012
Simba SC 2 -
0 Azam FC
Sept 11, 2011
Azam FC 0 -
0 Simba SC
Jan 23, 2011
Simba 2-3
Azam (Dar).
Sep 11, 2010
Azam 1-2
Simba (Tanga).
Machi 14, 2010
Azam 0-2
Simba (Dar)
Okt 24, 2009
Simba 1-0
Azam (Dar)
Machi 30, 2009
Azam 0-3
Simba (Dar)
Okt 4, 2008
Simba 0-2
Azam
0 comments:
Post a Comment