Simon Msuva, tegemeo la Ngorongoro |
Na Prince Akbar
TIMU ya taifa ya soka Tanzania ya vijana wenye umri chini ya
miaka 20, Ngorongoro Heroes imeahidi ushindi kwenye mechi yake dhidi ya
Nigeria, Flying Eagles kesho Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mechi hiyo ya kwanza ya raundi ya pili kutafuta tiketi ya
kucheza fainali za Afrika kwa vijana wenye umri huo zitakazofanyika mwakani
nchini Algeria itachezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10
kamili jioni.
Akizungumza kwenye mkutano na Waandishi wa Habari
uliofanyika leo (Julai 28 mwaka huu) ofisi za TFF, Kocha Mkuu wa Ngorongoro
Heroes, Jakob Michelsen na nahodha wake Omega Seme wamesema timu yao iko tayari
kwa mechi hiyo itakayochezeshwa na waamuzi kutoka Kenya.
Michelsen amesema timu yake imepata mechi mbili za kujipima
nguvu dhidi ya Rwanda, lakini pia aliishuhudia Flying Eagles ikicheza mechi ya
kirafiki na Rwanda (Young Amavubi) uliofanyika Julai 24 mwaka huu jijini
Kigali.
“Timu iko vizuri na wachezaji kama Frank Domayo, Simon Msuva
na Ramadhan Singano ambao pia wanachezea timu A (Taifa Stars), hivyo uzoefu wao
ni muhimu kwa mechi ya kesho.
“Nigeria ni mabingwa watetezi wa michuano hii kwa hiyo
tunatarajia upinzani mkubwa, lakini tumejiandaa kwa hilo. Nigeria ni nchi yenye
mfumo mzuri wa timu za vijana, na sisi tunaelekea huko huko” amesema Michelsen.
Naye Kocha Mkuu wa Flying Eagles, John Obuh amesema haijui
vizuri Ngorongoro Heroes lakini anaiheshimu kutokana na ukweli kuwa inacheza
raundi ya pili baada ya kuitoa Sudan katika raundi ya kwanza.
“Sina mchezaji yeyote anayecheza mpira wa kulipwa nje ya
Nigeria, lakini tumekuja kushinda ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kucheza
raundi ya mwisho na hatimaye tucheze fainali mwakani,” amesema Obuh
aliyefuatana na nahodha wake Samuel Okan ambaye ni mlinda mlango.
Viingilio katika mechi hiyo itakayochezeshwa na mwamuzi
Moses Osano ni sh. 3,000 kwa viti vya rangi ya chungwa, bluu na kijani wakati
VIP B na C itakuwa sh. 5,000. Kiingilio kwa VIP A ni sh. 10,000.
Osano atasaidiwa na Peter Keireini na Elias Wamalwa wakati
mwamuzi wa mezani (fourth official) ni Thomas Onyango. Kamishna wa mechi hiyo
atakuwa Charles Masembe kutoka Uganda.
Wakati huo huo: Shirikisho la Soka Afrika (CAF) limemteua
refa wa zamani wa kimataifa wa Tanzania, Hafidh Ali kuwa Kamisaa wa mechi kati
ya El Ahly Shandy na Al Hilal zote za Sudan.
Shandy ndiyo mwenyeji wa mechi hiyo namba 98 ya Kombe la
Shirikisho itafanyika Agosti 5 mwaka huu na itachezwa Uwanja wa Shandy ulioko
katika mji wa Shandy.
Refa wa mechi hiyo ni Raj Seechun kutoka Mauritius ambaye
atasaidiwa na Balkrishna Bootun, Jean Daniel Telvar na Parmendra Nunkoo, wote
pia kutoka Mauritius. Mratibu Mkuu wa mechi hiyo ni Paul Bassey wa Nigeria.
0 comments:
Post a Comment