Kikosi cha Yanga msimu uliopita |
Na Mahmoud Zubeiry
MICHUANO ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la
Kagame inatarajiwa kufikia tamati leo kwa fainali itakayowakutanisha mabingwa
watetezi, Yanga na Azam FC ya Dar es Salaam, Uwanja wa Taifa.
Yanga wanaodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager, wanaingia
kwenye mechi hiyo wakiwa na matumaini makubwa ya kutetea taji lao, baada ya
kuonyesha soka ya kuvutia katika mechi mbili zilizopita, wachezaji wake
wakicheza kwa ari na kujituma chini ya kocha mpya kutoka Ubelgiji, Thom
Saintfiet.
Yanga ilikaribishwa kwenye michuano ya mwaka huu na kipigo
cha 2-0 kutoka kwa Atletico ya Burundi katika Kundi C, kabla ya kushinda 7-1
dhidi ya Waw Salaam ya Sudan Kusini, na 2-0 dhidi ya APR ya Rwanda, ilishinda
kwa penalti 5-3 dhidi ya Mafunzo katika Robo Fainali, kufuatia sare ya 1-1 na
ikashinda 1-0 dhidi ya APR katika Nusu Fainali ndani ya dakika 120.
Michuano hii, imemuibua kinara mpya wa mabao Yanga, Said
Bahanuzi ‘Spider Man’, ambaye katika mabao 11 iliyofunga Yanga hadi sasa kwenye
michuano ya mwaka huu, yeye amefunga matano, mengine matano Hamisi Kiiza
‘Diego’ na lingine moja Nizar Khalfan,
Washambuliaji hawa wawili, Kiiza na Bahanuzi kwa ‘njaa yao
ya mabao’ wanatarajiwa kuwa chachu ya ubingwa kwa Yanga leo.
SIRI YA JEURI YA YANGA
Yanga inajivunia udhamini wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL),
kupitia bia yake, Kilimanjaro Premeum Lager, ambao ni wa kwanza tangu wapoteze
udhamini wa kampuni ya Shivacom.
Ikumbukwe, Kilimanjaro Premium Lager ilianza kuidhamini
Yanga Agosti 18, mwaka 2008, katika mkataba uliosainiwa kwenye hoteli ya
Movenpick (sasa Serena), mjini Dar es Salaam.
Kilimanjaro Premium Lager, ambao ni wadhamini wakuu wa
wapinzani wa jadi wa Yanga, Simba SC, imekuwa ikihakikisha udhamini wake
unafika maeneo yote muhimu katika shughuli za uendeshwaji wa klabu.
Na inaaminika udhamini huo ndiyo chachu ya mafanikio ya
miaka ya kmaribuni ya klabu hiyo, ikiwemo kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu mara tatu
katika kipindi cha miaka mitano (2008, 2009 na 2011) sambamba na ubingwa wa
Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame mwaka jana.
ILIVYOTWAA KOMBE MWAKA JANA:
Yanga ilifanikiwa kutwaa taji la Klabu Bingwa Afrika
Mashariki na Kati, maarufu kama Kombe la Kagame, baada ya kuifunga Simba bao
1-0, katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Shukrani kwake mshambuliaji wa kimataifa wa Ghana, Kenneth
Asamoah aliyefunga bao hilo, pekee dakika ya 108, akiunganisha kwa kichwa krosi
iliyochongwa kitaalamu na kiungo Rashid Gumbo.
Kabla ya taji hilo walilotwaa Jumapili sambamba na dola za
Kimarekani 30, 000, sawa na Sh. Milioni 45 za Tanzania, Yanga walitwaa tena
Kombe hilo kwa mara ya kwanza mwaka 1975 kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar,
wakiifunga Simba mabao 2-0 na baadaye mara mbili mjini Kampala, Uganda mwaka
1993 na 1999, mara zote wakiifunga SC Villa ya huko.
Ulikuwa mchezo mgumu ambao ulidumu kwa dakika 120, timu
zikionyesha kucheza tahadhari, kabla ya Asamoah kumaliza kazi.
Kikosi kilichoipa Yanga kombe la nne la Kagame kilikuwa; Yaw
Berko, Nsajigwa Shadrack, Oscar Joshua, Chacha Marwa, Nadir Haroub ‘Cannavaro’,
Juma Seif ‘Kijiko’/Rashid Gumbo, Godfrey Taita/Julius Mrope, Nurdin Bakari,
Davies Mwape, Jerry Tegete/Kenneth Asamoah na Hamisi Kiiza.
Yanga iliyokuwa Kundi B la michuano ya mwaka huu, ilifuzu
kama kinara wa kundi baada ya kujikusanyia pointi saba kutokana na kushinda
mechi mbili na kutoka sare moja.
Katika Robo Fainali, Yanga ilikutana na Red Sea ya Eritrea
na kushinda kwa penalti 6-5, kufuatia sare ya bila kufungana ndani ya dakika 90
za mchezo huo.
Katika Nusu Fainali, Yanga ilikutana na St George ya
Ethiopia na kushinda tena kwa penalti 5-4, kufuatia sare ya bila kufungana
ndani ya dakika 120, kabla ya kuiteketeza Simba SC katika fainali.
Ikumbukwe katika michuano ya mwaka huu, Yanga iliingia kama
‘viti maalumu’, kwani Simba SC ndio walikuwa wawakilishi halisi kama mabingwa
wa Bara.
Ili kushiriki mashindano ya mwaka huu, ilibidi Yanga wailipe
CECAFA dola za Kimarekani 20,000 kama faini ya kugomea mechi ya mshindi wa tatu
wa michuano hiyo, mwaka 2008 mjini Dar es Salaam.
Yanga ilitakiwa kucheza na Simba mwaka huo kuwania nafasi ya
tatu, ikiwa chini ya Mwenyekiti aliyekuwa na misimamo mikali, Wakili Imani Omar
Madega, Yanga iligoma kwa sababu hawakukubaliana na TFF juu ya mgawanyo wa
mapato ya milangoni.
ZANZIBAR MWAKA 1975:
Iliingia kama bingwa wa Tanzania baada ya kuifunga Simba SC
katika fainali ya Ligi mwaka 1974 Uwanja wa Nyamagana, Mwanza, wakati watani
wao hao waliingia kama mabingwa watetezi wa michuano.
Yanga ilipangwa Kundi B pamoja na Express ya Uganda na
Mufulira Wanderers ya Zambia. Yanga ilianza kwa kuifunga Express FC mabao 4-0
na baadaye kutoka sare ya 1-1 na Mufulira, hivyo kuongoza Kundi hilo na kukata
tiketi ya kuingia Nusu Fainali.
Katika Nusu Fainali, Yanga iliifunga Gor Mahia ya Kenya
mabao 2-0 na kukata tiketi ya kuingia fainali Janauri 13, mwaka huo ilipokutana
na watani wao wa jadi, Simba SC.
Mabao ya Sunday Manara ‘Computer’ na Gibson Sembuli (sasa
marehemu) yaliipa Yanga ushindi wa 2-0 na taji la kwanza la michuano hiyo.
KAMPALA, UGANDA MWAKA 1993:
Ilikwenda kama bingwa wa Bara na watano wao, Simba
walikwenda kama watetezi wa taji na huko Yanga walipangwa Kundi A pamoja na
wenyeji SC Villa na Malindi ya Zanzibar.
Katika mchezo wa kwanza, Yanga ilifungwa 3-1 na Villa, siku
hiyo kabla ya kuibuka na kuifunga Malindi mabao 2-1, yote yakitiwa kimiani na
Said Nassor Mwamba ‘Kizota’, sasa marehemu, hivyo kukata tiketi ya kuingia Nusu
Fainali.
Katika Nusu Fainali, Yanga ilikutana na Express FC na
kushinda mabao 3-1, hivyo kutinga fainali ambako ilikutana tena na SC Villa.
Kwa kuzingatia matokeo ya mchezo wa awali kwenye Kundi A,
Yanga haikupewa nafasi kabisa ya kufurukuta mbele ya SC Villa, lakini mambo
yalikuwa tofauti, mabao ya Said Mwamba
na Edibily Lunyamila, yaliipa timu hiyo ushindi wa 2-1 pamoja na taji la
pili la michuano hiyo.
Marehemu Kizota aliibuka mfungaji bora wa michuano hiyo.
KAMPALA, UGANDA MWAKA 1999:
Ilikwenda kama bingwa wa Bara, ikiwa mwakilishi pekee na
ilitua huko, huku mashabiki wengi wa soka Uganda wakiwa na kumbukumbu ya kile
kilichofanywa na klabu hiyo mwaka 1993.
Timu zilizoshiriki michuano hiyo ni Vital'O ya Burundi,
Mebrat Hail ya Ethiopia, AFC Leopards ya Kenya, Kiyovu Sport, Rayon Sport za
Rwanda,
Naadiga Dekedaha ya Somalia, KMKM ya Zanzibar, Al Hilal ya
Sudan, Yanga, wenyeji Express na SC
Villa za Uganda wakati Red Sea ya Eritrea ilijitoa dakika za mwishoni.
Kwa matokeo hayo, Kundi D ilimokuwa Yanga lilibakiwa na timu
mbili tu, yaani mabingwa hao wa Bara na mabingwa watetezi.
Mechi ya kwanza, Yanga ilifungwa 3-0 na Rayon Januari 4 na
ziliporudiana siku mbili baadaye, Yanga walilipa kisasi kwa ushindi wa 3-0 pia,
mabao ya
Sekilojo Chambua dakika ya 23 na 57 na Kali Ongala dakika ya
59.
Katika Robo Fanali, Yanga ilikutana na Al Hilal Januari 10
na kushinda mabao 2-1, wafungaji Salvatory Edward dakika ya 14 na Edibily
Lunyamila dakika ya 89 kwa penalti.
Katika Nusu Fainali, Yanga ilikutana na Vital’O ya Burundi
Januari 13 na kushinda mabao 3-2, wafungaji Kally Ongara dakika ya 16, Bakari
Malima dakika ya 78 na Said Mhando dakika ya 90.
Hivyo kwa mara ya pili, Yanga ilikutana na SC Villa kwenye
fainali kukumbushia vitu vya mwaka 1993 na safari hii mambo yalikuwa mazito
zaidi, kwani dakika 120 zilimalizika timu hizo zikiwa zimefungana bao 1-1
Lunyamila akiisawazishia Yanga dakika ya 42, baada ya Hassan Mubiru kutangulia
kufunga dakika ya saba tu ya mchezo huo.
Mchezo ukahamia kwenye mikwaju ya penalti na Manyika Peter
akaingia kwenye orodha ya makipa hodari wa kupangua penalti baada ya kupangua
mikwaju miwili, Yanga ikishinda kwa penalti 4-1, Uwanja wa Nakivubo.
Hivyo ndivyo Yanga ilivyotwaa mataji yake manne ya Kombe la
Kagame- na leo wanacheza fainali ya pili mfululizo nyumbani dhidi ya Azam,
wakijaribu kuifukuza rekodi ya watani wao wa jadi, Simba SC waliotwaa taji hilo
mara sita, je wataweza? Bila shaka dakika 90, 120 au mikwaju ya penalti itatoa
majibu leo.
0 comments:
Post a Comment