Thom Saintfiet akiongoza mazoezi ya Yanga, Uwanja wa Kaunda jioni hii. Picha zote na Mahmoud Zubeiry |
Na Mahmoud Zubeiry
KOCHA mpya wa Yanga, Thom Saintfiet amesema kwamba sera yake
ni ushindi na mataji na hahofii mpinzani yeyote katika soka ya Tanzania, ikiwemo
watani wao wa jadi, Simba SC.
Akizungumza katika Mkutano na Waandishi wa Habari jioni ya leo,
makao makuu ya klabu makutano ya Mitaa ya Twiga na Jangwani, Dar es Salaam,
Saintfiet alisema kwamba yeye ni muumini wa ushindi na mataji, hivyo anachotaka
ni ushindi tu.
“Nikishinda 5-0 ni vizuri, lakini hata nikishinda 1-0 si mbaya,
mimi ni mshindi na ndio maana nimekuja hapa kushinda,”alisema.
Thom alisema kwamba akili yake hapo kwa Simba tu, bali wapinzani
wote katika Ligi Kuu na akasema anataka kurejesha ubingwa wa Ligi Kuu, ambao
msimu uliopita klabu hiyo ilipokonywa na watani wao hao wa jadi.
“Upinzani ni mkubwa, nasikitika mwaka jana timu imepoteza
ubingwa wa Ligi Kuu, lakini si mbaya, si lazima timu bora kila mwaka iwe na
taji. Hata Barcelona ni timu nzuri, lakini haikuchukua ubingwa wa Ligi ya
Mabingwa wala La Liga.
Timu (Yanga) ilibeba nafasi ya tatu msimu uliopita, siyo
nzuri sana. Nataka nishirikiane na wenzangu kurejesha heshima,”alisema.
Saintfiet alisema kwamba ameona wachezaji ni wazuri na
anamuamini kocha anayemkuta Freddy Felix Minziro ni mzuri na amefanya kazi
nzuri. “Timu ilicheza mechi na Express wiki iliyopita, nimeambiwa ilicheza soka
nzuri na kushinda, naamini naikuta timu ikiwa vizuri,”alisema.
Mbelgiji huyo alisema kwamba ana wiki moja kabla ya kuanza
kwa Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame na hana wasiwasi atafanya
vizuri kwa sababu timu ina wachezaji wazuri na Minziro alianza kuwaandaa mapema.
Saintfiet alikataa kuzungumzia falsafa yake akisema hataki
wapinzani wake wajue siri zake, ila akasistiza sera yake ni ushindi na kubeba mataji.
Tom Saintfiet alizaliwa Machi 29, mwaka 1973 mjini Mol, Ubelgiji
na kabla ya kuwa kocha alicheza soka katika nafasi ya kiungo kuanzia mwaka 1983
hadi 1997 alipostaafu na kuwa kocha akiwa ana umri wa miaka 24, akiweka rekodi
ya kocha kijana zaidi kuwahi kutokea katika soka ya Ubelgiji.
Saintfiet amefundisha nchi kadhaa kuanzia kwao Ubelgiji,
Qatar, Ujerumani, Visiwa vya Faroe, Finland na Uholanzi.
Pia ana uzoefu wa kutosha wa kufundisha soka Afrika akiwa
amefundisha Namibia na Zimbabwe kama kocha Mkuu wa timu za taifa za nchi hizo.
Anasema kabla hajakwenda Namibia, Saintfiet alikuwa kocha wa
klabu ya Ligi Kuu Finland, iitwayo RoPS Rovaniemi na mwaka 2002, alikwenda
kuifundisha B71 Visiwa vya Faroe ambayo aliiwezesha kushika nafasi ya pili
katika Ligi Daraja la kwanza. Anasema kutoka hapo, akaenda kuwa kocha wa Al-Ittihad
Sports Club ya Qatar (sasa inaitwa Al-Gharafa SC) ambako alidumu hadi mwaka 2004
alipochukuliwa kuwa kocha wa timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17
ya Qatar.
Saintfiet ana leseni Shirikisho la Soka Ulaya (UEFA) ya
kufundisha soka ya kulipwa popote barani humo, ambayo aliipata mwaka 2000.
Kati ya mwaka 2006 na 2007 alikuwa Mkurugenzi wa Ufundi wa FC
Emmen ya Daraja la Kwanza Uholanzi na pia amewahi kufanya kazi kama Mshauri wa
Ufundi wa Shirikisho la Soka la Kazakhstan.
Amewahi kuwa
Mchambuzi wa soka katika Televisheni katika nchi za Ubelgiji, Afrika Kusini na
Namibia na alifanya kazi kama mkalimani DFB. Amesomea Saikolojia ya Michezo na
Uchumi.
Anazungumza lugha kibao na kwa ufasaha zaidi ni Kiholanzi, Kiingereza,
Kifaransa, Kijerumani, Kifaroe na ‘ana jua jua’ Kiarabu, Kiafrikana na Kispanyola
na sasa tayari ameanza kujifunza Kiswahili.
Baada ya kumaliza kusaini mkataba majira ya 9:47 jioni,
Saintfiet aliyewasili jana mchana nchini, aliteremka Uwanja wa Kaunda kuanza kufundisha
timu. Kwanza alianza kuzungumza na wachezaji kuwaelezea falsafa zake na kisha akaanza
kazi.
0 comments:
Post a Comment