MUINGEREZA; Stewart Hall wa Azam |
Na Prince Akbar
WAKATI kocha wa Azam FC,
Stewart Hall kutoka Uingereza amesema ana matumaini ya kuwafunga Simba SC
kwenye fainaili ya Kombe la Urafiki kesho, Uwanja wa Amaan, Zanzibar, mpinzani
wake Mserbia Profesa Milovan Cirkovick amemjibu kwamba anajidanganya.
Stewart amesema mjini hapa,
baada ya ushindi wa 2-0 jana dhidi ya mabingwa wa Zanzibar, Super Falcon na
kutinga fainali, sasa ni zamu ya mabingwa wa upande wa pili wa Muungano, Simba
SC nao kula kichapo.
Lakini Stewart amekiri kwamba
Simba, mabingwa wa Bara ni timu nzuri na mchezo utakuwa wa ushindani, lakini
mwisho wa siku, Azam watang’ara.
Stewart amesema wachezaji wake
aliowapa mapumziko kama Mrisho Khalfan Ngassa na John Raphael Bocco ‘Adebayor’
wanaweza kuja Zainzibar kesho, ila kama watazamaji, kwani ataendelea na kikosi
kile kile kilichomfikisha hapa.
Kwa upande wake, Milovan
amesema tangu wanapanda boti Zanzibar alijua tu fainali itakuwa kati ya timu
yake na Azam kwa sababu hizo kwa sasa ndizo timu bora Tanzania.
“Sisi mabingwa, wao wa pili
kwenye Ligi, hao ndio wapinzani wetu. Hatuwezi kuukwepa ukweli huo. Ila wataendelea
kuwa wa pili hata baada ya dakika 90 za kesho,”alisema Milovan.
Milo alisema amewaona Azam
wakicheza Zanzibar na anakiri ni timu nzuri, lakini ya kiwango cha kuisumbua tu
Simba SC si kuizuia kushinda.
Azam walikuwa wa kwanza jana
kujikatia tiketi ya kuingia fainali, baada ya kuifunga Falcon 2-0, mabao yote
yakitiwa kimiani na mshambuliaji wa kimataifa wa Ivory Coast, Kipre Herman
Tcheche Uwanja huo huo wa Amaan, Zanzibar.
MSERBIA; Profesa Milovan Cirkovick wa Simba SC |
Tcheche alifunga bao la kwanza
dakika ya 67, akiunganisha krosi ya Hamisi Mcha wakati bao la pili, alifunga
kwa penalti, dakika ya 77, baada ya Samir Haji Nuhu kuangushwa kwenye eneo kla
hatari na Samir Said dakika ya 77.
Katika mechi hiyo, Azam ilipata
pigo dakika ya 54, baada ya mshambuliaji wake Gaudence Exavery Mwakimba
kutolewa nje kwa kadi nyekundu dakika ya 54 kwa kumpiga kiwiko Abdul Ally.
Simba nayo ilijikatia tiketi
yake baadaye hiyo jana kwa ushindi wa 1-0 dhidi ya Zanzibar All Stars, bao
pekee la kiungo wa kimataifa wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Patrick
Kanu Mbivayanga.
Kanu, aliyeletwa kwa mabingwa
hao wa Ligi Kuu na Mkongo mwenzake, marehemu Patrick Muteesa Mafisango,
alifunga bao hilo dakika ya 57, akiunganisha krosi ya mshambuliaji wa kimataifa
wa Zambia, Felix Mumba Sunzu Jr., aliyeingia kipindi cha pili kuchukua nafasi
ya Salim Kinje.
Dakika ya 85, Sabri Ramadhan
‘China’wa All Stars, alikwamisha mpira nyavuni, lakini refa akasema alikuwa
ameotea.
0 comments:
Post a Comment