KATIKA siku za karibuni, Tanzania imeanza kufaidika kwa kupata vijana wadogo wenye vipaji vya soka kupitia taasisi na timu mbalimbali. Kama ilivyo kawaida ya klabu zetu kubwa, Yanga imezoa yosso kadhaa walioko kwenye timu za taifa za vijana na Taifa Stars, mmoja wao ni Simon Happygod Msuva. Msuva (19) si mdogo tu wa umri, hata umbile lake ni la saizi ya kati lakini anatajwa kuwa miongoni mwa watakaoking'arisha kikosi hicho katika Kombe la Kagame na Ligi Kuu Bara. Yanga imemsajili kwa mkataba wa miaka miwili akitokea Moro United aliyong'ara nayo msimu uliopita kwa uhodari wake wa kupachika mabao. Umahiri wake ndiyo ulioisukuma Mwanaspoti kumtafuta ili kuzungumza naye. Ilimkuta nyumbani kwao Ubungo, jijini Dar es Salaam akiwa na wazazi wake, Happygod na Suzan James. Sababu ya kujiunga Yanga "Nimejiunga Yanga kwa sababu mimi ni mchezaji. Kazi yangu ni kucheza soka na ninaangalia maslahi," anasema Msuva ambaye amefurahia kupata nafasi ya kucheza kikosi kimoja na Mnyarwanda, Haruna Niyonzima. "Pia naipenda Yanga na naamini mambo yataenda vizuri nitakaposhirikiana vizuri na wenzangu, kikubwa naomba waniunge mkono, anasema Msuva ambaye pia ni shabiki wa Manchester United anayevutiwa na Cristiano Ronaldo wa Real Madrid. "Hii ni kwa wachezaji wenzangu, viongozi na wadau wa Yanga kwa ujumle, tuwe kitu kimoja." Anasema, anaamini alifanya jambo sahihi kujiunga na Yanga licha ya baadhi ya wadau kumpinga. "Sijafanya mapema, kama Yanga wenyewe wameniamini na kunisajili, nafikiri huu ndiyo muda wangu mwafaka wa kufanya kazi Mtaa wa Jangwani," anaeleza na kutolea mfano wa kiraka wa Simba, Shomari Kapombe, ambaye naye alijiunga akiwa mdogo lakini amecheza kwa mafanikio. Akizungumzia ushindani wa namba, Msuva, anajua ushindani ni mkubwa, lakini anaamini ataimudu changamoto hiyo. Nje ya soka Mbali na soka, Msuva ana kipaji kingine cha kucheza dansi kama wanavyofanya vijana wa Nyumba ya Vipaji Tanzania (THT). Anakiri kuupenda mno muziki na anavutiwa na Ally Kipa na Chriss Brown. Akizungumzia tabia, alisema kuwa yeye ni mtu mtaratibu na kudokeza chakula anachokipenda ni wali na kuku. Alivyoibuka Kipaji cha Msuva kilitambulika akiwa mdogo wakati akisoma katika Shule ya Msingi ya Lions ya Magomeni ambako alicheza nafasi ya kipa. "Nilianza kucheza kama kipa wakati nasoma elimu ya msingi, lakini nilibadilisha nafasi nilipojiunga na Academy ya Wakati Ujao ambayo hufanya mazoezi yake Chuo Kikuu, hapo ndiyo nilianza kucheza ndani," anasema. Akiwa hapo alifanya vizuri na kuchukuliwa timu ya Mkoa wa Kinondoni kucheza Copa Coca Cola mwaka 2009 na alishika nafasi ya pili kwa ufungaji bora. Kutokana na kufanya kwake vizuri, Azam ilimchukua akawa katika kituo chao na aliwachezea michuano ya Kombe la Uhai mwaka 2010 na kuwa Mfungaji Bora. Aliamua kujiunga na Moro United mwaka 2011 baada ya kuondoka Azam kutokana na kukosa mkataba. Akiwa na Moro United, alingara kutokana na uhodari wake wa kufunga mabao na ndipo Yanga ilipomwona na kumsajili na hasa baada ya kuitwa Taifa Stars. Msuva alisema kwa sasa anapiga moyo konde ili aitwe acheze katika kikoso cha kwanza cha Taifa Stars. Mama yake alimkataza soka Msuva anasema, awali mama yake (Suzan) alimpinga kabisa mwanaye huyo katika suala la kucheza soka kwa kuamini huo ulikuwa ni uhuni tu. Alimtaka ajikite katika kusoma. "Mama yangu ni mlokole, alijua soka ni mambo ya kihuni," anasema Msuva ambaye hucheza nafasi za kiungo mshambuliaji na winga. "Alipata matumaini na kuniruhusu alipoona nimechaguliwa kwenda Sudan na timu ya taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 17. "Kitendo hicho ndicho kimemfanya aungane nami na sasa ananiunga mkono kwa asilimia 100." Anasema baba yake amechangia mafanikio ya soka yake kwani alikuwa akimnunulia viatu na jezi. Historia Msuva anatoka katika familia ya soka, baba yake alikuwa akisakata kabumbu. Baba huyo Happygod anasema: "Mimi nilicheza soka enzi za ujana wangu, nilicheza na akina Jamhuri Kihwelo, Idd Cheche wa Azam, Ubwa Zuberi na Edward Chumila, ilikuwa kati ya 1977 na 1982. "Lakini sikufanikiwa kucheza soka ya klabu kubwa kwani wazazi wangu walitaka nisome na nisiwe mbali nao, nilitakiwa na Majimaji ya Songea sikwenda, lakini pia Black Fighters ya Zanzibar ambayo nilikwenda pamoja na Ubwa (baba wa Zuberi na Abuu wa Yanga) nayo sikuichezea kwani baada ya muda wazazi walinitaka nirudi." Msuva ni wa pili kati ya watoto wa nne, anamfuata dada yake, Mary na wadogo zake ni James na Gabriel ambao nao wanacheza soka. Alisoma Shule ya Msingi ya Lions ya Magomeni na kumalizia Shule ya Sekondari ya Middlend High School 2008. SOURCE: GAZETI LA MWANASPOTI |
Buffalo Bills WAG sends one-word message to Brittany Mahomes after rivalry
showdown with Chiefs
-
Paige Buechele sent a message to fellow NFL WAG Brittany Mahomes after the
two saw each other at Sunday's mega-AFC matchup between the Buffalo Bills
and th...
36 minutes ago
0 comments:
Post a Comment