Messi wa Msimbazi; Rama Singano |
Na Princess Asia
KIUNGO chipukizi wa Simba
SC, Ramadhani Singano ‘Messi’ anatarajiwa kuondoka nchini wakati wowote kwenda
Austria kwa majaribio ya soka ya kulipwa, imeelezwa.
Chanzo cha habari cha
uhakika kutoka ndani ya Simba SC, kimeiambia BIN ZUBEIRY jana kwamba, Messi amepata ofa hiyo ya majaribio
kupitia wakala mmoja wa wachezaji Tanzania, anayetambuliwa na Shirikisho la
Soka la Kimataifa (FIFA), anayefanya kazi na klabu hiyo.
“Kuna wakala mmoja ambaye
anafanya kazi na sisi, ameleta ofa hiyo na kama kijana atafuzu, Simba itapata
kama dola za Kimarekani 300,000 hivi,”kilisema chanzo kutoka Simba SC.
Messi huyo alipandishwa
kutoka timu ya vijana ya Simba msimu uliopita na pamoja na kuingia mara chache
akitokea benchi, lakini amewavutia wengi kwa soka yake na kwa sasa ni miongoni
mwa wachezaji tegemeo wa timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20,
Ngorongoro Heroes.
Tayari mshambuliaji wa
Simba, Emmanuel Okwi, anaendelea na majaribio katika klabu ya FC Red Bull
Salzburg ya Austria yenye maskani yake Wals-Siezenheim, nchini humo na baada ya
hapo ndipo majibu yatatoka.
Klabu hiyo inayotumia Uwanja
wa Red Bull Arena, ikiwa zaidi inafahamika kama SV Austria Salzburg kabla
haijanunuliwa na kampuni ya Red Bull mwaka 2005, imewahi kufika Fainali ya
Kombe la UEFA mwaka 1994 na inacheza Ligi Kuu ya Austria, iitwayo Bundesliga
kama Ligi Kuu ya Ujerumani.
Timu hiyo ni kama timu
ambayo Okwi, anachezea kwa sasa, Simba SC, kwani nayo inavaa jezi za rangi ya
nyeupe na nyekundu na imewahi kutwaa taji la Bundesliga ya Austria mara saba na
pia ilicheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu wa 1994–1995 kama Casino Salzburg, na
kuwa timu pekee, ambayo haikufungwa na mabingwa wa wakati huo, Ajax Amsterdam.
Awali, Okwi aliikosesha
Simba Sh. Bilioni 2 kwa kukataa kujiunga na klabu ya Mamelodi Sundown ya Afrika
Kusini na kuamua kwenda Austria, ambako inaelezwa klabu hiyo iko tayari kutoa
Euro 600,000 akifuzu.
Awali Orlando Pirates ya
Afrika Kusini ilimuomba Okwi akafanye majaribio huko kama angefuzu wangemsajili
dau la dola 550,000 kabla ya kuibuka kwa taarifa za kutakiwa Italia na klabu ya
Parma.
Hata hivyo, Simba SC ilisema
imeshindwa kumshawishi Okwi kwenda kucheza Afrika Kusini kwa kuwa mwenyewe
anataka kucheza Ulaya tu. Wakala aliyeiunganisha Simba na Pirates akawasilisha
ofa nyingine kutoka Mamelodi, ambayo ni Euro 600,000 na kupanda hadi Sh.
Bilioni 2, lakini bado mabingwa hao wa Tanzania, walishindwa kumshawishi Okwi
kwenda Ligi Kuu ya Afika Kusini (PSL).
0 comments:
Post a Comment