Thom Saintfiet alipokuwa kazini Namibia |
Na Prince Asia
KOCHA mpya wa Yanga, Thom Saintfiet, raia wa Ubelgiji
anatarajiwa kuwasili leo Dar es Salaam, tayari kuanza kazi ya kukinoa kikosi
cha mabingwa hao wa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame.
Ofisa Habari wa Yanga, Louis Sendeu alisema jana kwamba, Thom
aliyekuwa Mkurugenzi wa Ufundi wa Shirikisho la Soka Nigeria, akiwasili
atakwenda moja kwa moja kufanya mazungumzo na uongozi kwa ajili ya kusaini
mkataba.
Alisema Saintfiet ataanza kazi mara moja atakapowasili na
kumaliza kusaini mkataba, ili kuiandaa timu kwa ajili ya kutetea Kombe la
Kagame, michuano inayotarajiwa kuanza Julai 14, mwaka huu, Yanga ikifungua dimba
na mabingwa wa Burundi, Atletico.
Mbelgiji huyo anakuja kurithi mikoba ya Mserbia, Kostadin
Bozidar Papic aliyetupiwa virago mwishoni mwa msimu.
Tangu kutupiwa virago kwa Papic zikiwa zimesalia mechi tatu
ligi kumalizika, Yanga imekuwa chini ya Kocha wake Msaidizi, Freddy Felix Minziro.
Ujio wa Mbelgiji huyo, unamaliza zama za makocha wa Kiserbia
waliokuwa wakibadilishana uongozi wa benchi la ufundi la Yanga, tangu mwaka
2007, kuanzia Milutin Sredojevic ‘Micho’ aliyewaachia Profesa Dusan Savo Kondic,
Spaso Sokolovoski na Serdan Civojnov, ambao nao walimuachia Papic.
Awali, Papic alipoondoka nafasi yake ilichukuliwa na Mganda,
Sam Timbe aliyeleta mataji mawili, ubingwa wa Ligi Kuu na Kombe la Kagame, lakini
akarudishwa tena Mserbia huyo msimu uliopita kabla ya kutupiwa virago mwishoni
mwa msimu.
0 comments:
Post a Comment