Na Princess Asia
MABINGWA watetezi wa michuano ya Copa Coca-Cola, Kigoma
wameng’oka katika michuano ya mwaka huu baada ya kulala mabao 2-1 mbele ya Mara
katika mchezo uliochezwa leo (Julai 7 mwaka huu) Uwanja wa Tanganyika Packers
ulioko Kawe, Dar es Salaam.
Hadi kipindi cha kwanza cha mechi hiyo ya kutafuta tiketi ya
kucheza robo fainali kinamalizika, Mara walikuwa mbele kwa bao 1-0 lililofungwa
dakika ya 21 na George Martime.
Kipindi cha pili kilianza kwa nguvu ambapo Mara walifanikiwa
kupachika bao la pili dakika ya 52 kupitia kwa Israel Daud. Kigoma ilipata bao
lake dakika ya 63 mfungaji akiwa Hassan Ramadhan.
Kwa ushindi huo sasa Mara itacheza mechi ya robo fainali
Julai 10 mwaka huu saa 10 jioni kwenye Uwanja wa Karume na mshindi wa mechi
kati ya Morogoro na Pwani itakayochezwa leo jioni kwenye Uwanja wa Tanganyika
Packers.
Nayo Temeke imepata tiketi ya kucheza robo fainali baada ya
leo kuitoa Ruvuma kwa mikwaju ya penalti katika mechi ya 16 bora iliyofanyika
Uwanja wa Karume. Hadi dakika 90 za kawaida zinamalizika timu hizo zilikuwa
zimefungana mabao 2-2.
Katika mikwaju ya penalti, Temeke ambayo itcheza robo
fainali Julai 10 mwaka huu saa 2 asubuhi kwenye Uwanja wa Karume na mshindi wa
mechi kati ya Mjini Magharibi na Kagera inayochezwa leo jioni kwenye uwanja huo
ilipata penalti 3 dhidi ya moja ya wapinzani wao.
Hatua ya 16 bora inaendelea kesho (Julai 8 mwaka huu) kwa
mechi nne. Asubuhi Kinondoni itacheza na Rukwa (Uwanja wa Karume), na Dodoma
itacheza na Arusha (Uwanja wa Tanganyika Packers, Kawe).
Mechi za jioni itakuwa Kilimanjaro na Mwanza ambazo
zitapambana kwenye Uwanja wa Karume wakati Tabora itaumana na Tanga kwenye
Uwanja wa Tanganyika Packers.
0 comments:
Post a Comment