// Disable text selection (not fully reliable) function disableSelection(element) { element.setAttribute('unselectable', 'on'); element.style.userSelect = 'none'; element.style.MozUserSelect = 'none'; element.style.webkitUserSelect = 'none'; } // Apply to the entire document body document.addEventListener('DOMContentLoaded', function() { disableSelection(document.body); }); KWA NINI CHUJI ALIKUWA CHUJI LEO... - BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE KWA NINI CHUJI ALIKUWA CHUJI LEO... - BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE
  • HABARI MPYA

    Friday, July 20, 2012

    KWA NINI CHUJI ALIKUWA CHUJI LEO...


    JEZI MPYA, MAVITUZ YA NGUVU; Chuji katika jezi namba 24, badala ya 4 aliyokuwa akivaa awali

    Na Mahmoud Zubeiry
    KIUNGO mkabaji, jukumu lake zaidi ni kusaidia safu ya ulinzi na inapotokea timu imeuteka mchezo ndipo anaonekana naye akisaidia mashambulizi kama ambavyo inaweza kuwa kwa mabeki.
    Athumani Iddi Athumani, anayerudi katika kiwango chake kwa kasi ya kuridhisha baada ya misimu miwili ya kuyumba vibaya, leo katika kikosi cha Yanga kilichomenyana na APR ya Rwanda kwenye mechi ya mwisho ya Kundi C, Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, alipangwa kucheza kama kiungo mkabaji.
    MZUZU; Athumani Iddi 'Chuji' katika staili ya Iddi Cheche
    beki wa zamani wa Sigara, kufuga ndefu chini ya kidevu  'mzuzu'
    Tofauti na mechi mbili zilizopita, dhidi ya Atletico ya Burundi na Waw El Salaam ya Sudan Kusini, ambazo Chuji alikuwa wa kawaida tu, lakini leo mtoto huyo wa mchezaji wa zamani wa CDA ya Dodoma, aling’ara kiasi cha kutosha.
    Alikuwa akichezesha timu vizuri, akigawa pasi muruwa, akitembea na mipira akipokonya mipira. Bila ya kupinda panda kona nyingi, Chuji alifanya kazi nzuri leo.
    Lakini kwa nini? Hilo ndilo swali ambalo tunapaswa kujiuliza. Jibu ni mfumo wa leo wa Yanga, inayofundishwa na kocha Mbelgiji, Tom Saintfiet. Siku zote, baada ya mechi tangu Mtakatifu Tom amekuja Yanga, huwa namfuata kumuhoji maswali, lakini leo ilikuwa tofauti.
    Nilipomfuata, wakati anajiandaa kujibu maswali; alikutana na kitu tofauti, nilimuambia; “Hongera, nimeona timu inabadilika, nimeona mfumo mpya mzuri, nadhani unatakiwa kuutilia mkazo, wachezaji waumudu ipasavyo,”.
    Akasema; “Asante sana, wewe unajua sana na ninapenda sana kusoma blog yako, kila siku,”. Nikamuuliza, unawezaje kusoma Kiswahili? Akaniambia; “Natafsiri kupitia google, nasoma naelewa umeandika nini,”. Mjadala ukaisha.
    Kwa nini nilimpongeza Mtakatifu Tom- ni kutokana na mfumo ambao aliutumia leo. Niwe wazi, kwa jinsi nilivyoiona Yanga iliyocheza na Waw Salaam pamoja na kushinda 7-1, lakini hadi naingia Uwanja wa Taifa leo, kura yangu ilikuwa kwa mabingwa wa Rwanda.
    Niliingia uwanjani, nikiamini Yanga itafungwa, lakini baada ya dakika 90 matokeo yalikuwa tofauti, mabingwa watetezi, walishinda 2-0 kwa mabao safi ya mshambuliaji mpya wa timu hiyo, Said Bahanuzi, yote pasi za Hamisi Kiiza ‘Diego’.
    Chuji aling’ara kwenye kiungo kama nilivyoelezea hapo juu, ingawa kidogo aliangushwa na kiungo aliyekuwa akicheza juu yake, Haruna Niyonzima ‘Fabregas’, ambaye nadhani kutokana na kusumbuliwa na maumivu bado hajacheza kwa kiwango chake kwenye michuano hii.
    Pongezi kwa Nizar Khalfan, aliyekuwa akicheza kama kiungo wa kulia, kwa kuingia katikati kumsaidia kazi Niyonzima.
    Hadi hapo, bado sijasema kwa nini Chuji aling’ara leo. Ni kwamba, mfumo wa kutumia mabeki watatu wa katikati alioutumia Mtakatifu Tom ndio siri ya kung’ara kwa Chuji leo. Oscar Joshua Fanuel alipangwa kama beki wa kushoto, lakini juu yake alikuwa anacheza beki mwingine wa kushoto, Stefano Mwasyika.
    Mtakatifu Tom, akiwa na kocha wa APR,
    Ernest Brandy kulia leo Taifa, kabla
    ya mechi baina ya timu zao
    Yanga inapokuwa inashambuliwa, Mwasyika anashuka chini na Hamisi Kiiza anakwenda kumsaidia, wakati Oscar anaingia katikati kuongeza idadi ya mabeki wa katikati- hivyo Chuji anabaki huru akiusoma mwelekeo wa mpira na inakuwa kazi rahisi kwake kwenda kupokonya na kuanza kupandisha timu.
    Nadhani nimeeleweka. Lakini pia, upande wa pili, mbele Yanga ilianza na mshambuliaji mmoja kama wawili- yaani Said Bahanuzi na Kiiza walicheza kama washambuliaji pacha, ambao wanaelekea kuelewana vizuri katika mechi ya pili sasa na hii inaweza kufanya uone nafasi ya Jerry Tegete kuendelea kuwa mshambuliaji namba moja, Yanga inazidi kuwa finyu.
    Kumbuka, kuna kifaa kingine, Simon Msuva hakimo kwenye mashindano haya, kipo timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20, inayojiandaa na mechi dhidi ya Nigeria, Julai 29, mwaka huu kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Mataifa ya Afrika kwa vijana.
    Kiiza alikuwa anaingia katikati, Yanga inaposhambulia, lakini mpira ukiwa kwenye himaya ya wapinzani anakwenda pembeni na ndiyo maana leo pasi zote za mabao ya Bahanuzi, zilitoka kwake. Na bado na yeye alikosa mabao kama mawili ya wazi.
    Nimewahi kusema soka ni mchezo wenye wigo mpana na unahitaji muda wa kutosha kujifunza kabla ya kukimbilia majukumu. Tom amekuwa mwepesi kubadili mfumo aliotaka kuanza nao Yanga na kutambulisha mfumo mpya mara moja, ambao unaonekana kuleta tija ndani ya timu. Hiyo ndiyo soka na bila shaka hadi hapo unaweza kujua kwa nini Chuji alikuwa Chuji leo. Wasalaam. Waislamu wenzangu, nawatakiwa mfungo mwema wa mwezi mtukufu wa Ramadhani inshaallah. Natambua taifa, lipo katika kipindi kigumu wakati huu, kutokana na ajali mbaya ya meli ya MV Skaget, iliyosababisha vifo vya mamia juzi. Tunapswa kuwa wavumilivu na wenye subira, tukimuomba Mwenye Mungu, pamoja na kuziweka pema peponi roho za marehemu, kuwajaalia ahueni walonusurika, lakini pia aliepushe taifa letu na majanga zaidi. Atujaalie amani na salama inshaallah amin. Alamsiki, Ramadhan Karim.   
    Chuji anapokonya, anapasua

    Chuji anaenda kupokonya

    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KWA NINI CHUJI ALIKUWA CHUJI LEO... Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top