Simba SC; Imeonyesha nia ya kushiriki |
KATIKA siku ambayo Yanga ilitinga Nusu Fainali ya Klabu
Bingwa ya soka Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame nilikuwa nina mazungumzo
na Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA),
Leodegar Chillah Tenga.
Na Mahmoud Zubeiry |
Mazungumzo yetu yalianzia Uwanja wa Taifa tukiwa kwenye gari
lake kuelekea mjini na yalitosha kwa sababu ya foleni. Tulikuwa wawili tu
kwenye gari na yalidumu kwa zaidi ya nusu saa tukiwa njani, kutokana na foleni.
Tulijadili mambo kadha wa kadhaa, kwanza ni kuhusu timu zetu
na wachezaji chipukizi ambao ndio taswira ya baadaye ya soka ya Tanzania. Tenga
ambaye pia ni rais wa TFF, alisema amefurahishwa na wachezaji vijana wadogo
waliong’ara kwenye mashindano hayo kama Said Bahanuzi ‘Spider Man’, Juma Abdul
wa Yanga, Khamisi Mcha ‘Vialli’, Salum Abubakar ‘Sure Boy Jr’ wa Azam na
wengineo.
Katika timu zetu na ushiriki wao kwenye mashindano hayo, kwa
pamoja tulijiridhisha, hazikuwa na maandalizi ya kutosha kabla ya mashindano na
Tenga akasema ni muhimu kukawa na programu ya taifa ya maandalizi ya kabla ya
msimu na akaniambia tayari amemuagiza Mkurugenzi wa Ufundi wa Shirikisho la
Soka Tanzania (TFF), Sunday Kayuni kulifanyia kazi hilo.
Siku mbili baadaye, TFF ikatangaza mashindano mapya ya Bank
ABC Super 8, ambayo yamepangwa kuanza Agosti 4 hadi 18, mwaka huu yakishirikisha
timu nane, nne za Zanzibar na nne za Bara.
Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah alisema kwamba timu tatu
zilizoshika nafasi za juu katika Ligi Kuu zote mbili zitaingia moja kwa moja,
wakati timu moja kila upande iliyoongoza katika kampeni ya kupanda Ligi Kuu,
zitashirikishwa pia.
Alisema timu hizo zitakuwa katika makundi mawili na
hakutakuwa na mechi ya kusaka mshindi wa tatu zaidi ya kuwepo kwa zawadi kwa
timu itakayotwaa ubingwa tu na tayari wameshaziandikia barua za kuzitaarifu
kuhusiana na michuano hiyo.
“Nadhani hii ni nafasi nyingine kwa timu kuonyesha ushindani
katika michuano hii, pia pamoja na kujiandaa kwa msimu mpya wa ligi, makocha wa
timu shiriki wataweza kujua kiwango kilichopo kwenye timu zao na kama kuna
kasoro warekebishe kabla ya kuanza kwa ligi,”alisema.
Bank ABC ambayo imedhamini michuano hiyo kwa miaka mitatu,
kupitia kwa Mkurugenzi wake Mkuu Boni Nyoni alisema wameamua kuandaa michuano
hiyo ili kuunga mkono jitihada za maendeleo ya soka hapa nchini.
HONGERA TFF KWA MICHUANO HII…
Moja ya sababu za wachezaji wetu kutokuwa fiti kwa angalau
asilimia 70, ni kutokana na kukosa mechi za kutosha za ushindani, kwani wengi
wao zaidi ya Ligi Kuu hawana sehemu nyingine ya kuongeza uzoefu wao kiuchezaji.
Kwa hivyo ujio wa mashindano kama haya, ambayo dhahiri
yatakuwa ya ushindani ni jambo la kufurahia na kwa sababu hiyo hatuna budi
kuipongeza TFF na kuiomba itanue zaidi wigo wa kutafuta udhamini kwa ajili ya
mashindano mengine muhimu.
Muda mrefu sijamuona Mkurugenzi wa Masoko wa TFF, Jimmy
Kabwe akijitokeza kifua mbele, kwa sababu vyombo vya habari vimekuwa
vikimnyooshea sana vidole juu ya utendaji wake, kiasi cha kutilia shaka uwezo wake
na uzoefu katika jukumu alilopewa.
Zaidi ya kumuona katika utiaji saini wa mkataba wa udhamini
wa timu ya taifa, Taifa Stars na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), ndio nilimuona
tena nyota huyo wa filamu ya Secret
katika kutangazwa kwa Super 8 ya Bank ABC.
Nampongeza Jimmy na sasa aelewe kama atatekeleza wajibu wake
vizuri, baadala ya kukaa mezani na kuchati kwenye tweetter na facebook, kila
mmoja atakuwa rafiki yake, kwani shida yetu ni kuona ufanisi.
Kwa sasa tunaona kabisa shirikisho linakabiliwa na mzigo
mzito- mashindano ya Kombe la FA hayapo, yanataka kurudi ha hayana udhamini
hadi sasa, tunahitaji kuwa na Ligi madhubuti ya timu za vijana za klabu za Ligi
Kuu, lakini bila udhamini haiwezekani.
Timu zetu zote za taifa hazina udhamini, ukiondoa ule wa timu
ya wakubwa. Bado soka haitumiki ipasavyo hapa nchini katika kampeni za
kibiashara kama ilivyo nchi za wenzetu- tunataka kuona wachezaji wa timu ya
taifa wanaingia mikataba mikubwa ya madau makubwa ya matangazo ya biashara. Kwa
kweli Jimmy anatakiwa kujua, ana kazi kubwa bado ya kufanya ili kutimiza wajibu
wake vema.
MICHUANO HII IMEKUJA WAKATI
SIYO…
Ingawa ujio wa michuano hii ni habari njema kwa soka ya
Tanzania, lakini kwa sababu moja au mbili, imepokewa vibaya na klabu nchini.
Kocha wa Yanga, Tom Saintfiet raia wa Ubelgiji alikuwa wa
kwanza kuonyesha hayuko tayari kuingiza timu yake kwenye michuano hiyo kwa
sababu anaamini itawaumiza wachezaji wake.
Alisema kwamba baada ya mashindano ya Klabu Bingwa ya soka
Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame jana klabu yake ikitetea taji, ni
vema wachezaji wakapewa muda wa kupumzika, badala ya kupewa adhabu nyingine.
“Tunahitaji kupumzika, tunawaumiza wachezaji wetu, bado
sijaambiwa rasmi, nimekamilisha programu yangu ya mazoezi(ya Kagame) na baada
ya mechi na Azam, lazima wachezaji wangu wapumzike hadi Alhamisi. Ijumaa
(Agosti 3) tunaanza upya programu ya mazoezi kwa ajili ya Ligi Kuu,”alisema
Saintfiet.
Wakati kocha wa Yanga, washindi wa tatu wa Ligi Kuu ya Bara,
Mtakatifu Tom akitoa msimamo huo, BIN ZUBEIRY inafahamu mabingwa wa
Ligi Kuu ya Bara, Simba SC, baada ya kutolewa wamewapa mapumziko wachezaji wake
na watakutana wiki ijayo kuanza maandalizi ya tamasha lao la kila mwaka, Simba
Day, litakalofanyika Agosti 8, mwaka huu na tayari wamekwishatoa ratiba yao
kuanzia Agosti 5 hadi 11, mwaka huu.
Agosti 5, Simba itakuwa na Mkutano Mkuu wa mwaka katika
ukumbi wa Polisi Oystrebay na siku hiyo hiyo watazindua Wiki ya Simba na Jamii,
kuelekea Simba Day Agosti 6, watatembelea watoto yatima katika kituo cha Maungu
Orphanage, Kinondoni Mkwajuni, Agosti 7, watatembelea wagonjwa katika hospitali
ya Mwananyamala na Agosti 8, watafanya tamasha la Simba Day Uwanja wa Taifa, likitanguliwa
na burudani kadhaa kabla ya mechi dhidi ya klabu moja kubwa barani.
Agosti 9, Simba watatembelea shule ya msingi Mgulani
kuhamasisha michezo mashuleni na Agosti 10, watatembelea kiwanda cha Kampuni ya
Bia Tanzania (TBL) Ilala, ambao ni wadhamini wao wakuu, kupitia bia ya
Kilimanjaro Premium Lager.
Tayari wadhamini wakuu wa Simba SC, kupitia Meneja wa bia ya
Kilimanjaro Premium Lager, George Kavishe wamekwishakabidhi fedha, Sh. Milioni
20 kwa ajili ya Mkutano Mkuu na fedha nyingine za tamasha zitatolewa wiki
ijayo.
Na jana Mwenyekiti wa Simba, Alhaj Ismail Aden Rage alisema atakuwa
tayari kuiruhusu timu yake kushiriki mashindano hayo, iwapo Simba wataonyeshwa
mikataba ya mashindano hayo ambayo TFF wameingia na wadhamini, Bank ABC.
Hapa Rage yupo kimaslahi zaidi na si kuhusu mustakabali wa
timu. Mara baada ya Simba kutolewa na Azam katika Kombe la Kagame, Kocha Milovan
Cirkovick alisema aliwaambia mapema viongozi wake kwamba timu haina maandalizi
ya kutosha na hakutaka iingie kwenye mashindano hayo, ila viongozi
wakalazimisha.
Sasa katika kipindi hiki ambacho Milo yuko kwa Serbia kwa
mapumziko ya wiki moja, akirudi tu atafikia michuano hiyo, je saa ngapi atakuwa
amewaandaa wachezaji wake?
Ni kweli Rage alishauriana na kocha Milovan kabla ya kutoa
tamko lake? Sijui, lakini nasema soka ya Tanzania kwa aina ya viongozi
tulionao, tuna safari ndefu sana kufikia mafanikio. Sasa huyu ndiye Rage, ambaye
angalau kidogo ameucheza mpira, ana uzoefu wa uongozi wa soka na hata kielimu
si haba- Mhasibu huyo bwana, je wale wenzangu na mie akina Iddi Godi Godi
tutarajie nini kutoka kwao?
Azam kama klabu, hawajatoa tamko rasmi, lakini wachezaji wake
wamesema wanataka kupumzika na hawako tayari kucheza michuano ya Bank ABC Super
8 na wamependekeza labda, wacheze wachezaji wa timu ya Academy michuano hiyo.
Wakizungumza na BIN ZUBEIRY kwa masharti ya
kutotajwa majina yao kukwepa kuingilia uhuru wa viongozi, wachezaji hao walisema
kwamba tangu kumalizika kwa Ligi Kuu Aprili mwaka huu hawajapumzika, hivyo
wanataka kupumzika japo kwa wiki moja kabla ya kuanza rasmi kwa msimu mpya.
“Ligi imeisha tumengia kwenye kambi ya timu ya taifa,
tumecheza na Ivory Coast, tumecheza na Gambia, tumecheza na Msumbiji na baada
ya hapo tumerudi hapa, tunaingia kwenye Kombe la Urafiki. Tunatoka huko,
tunaingia moja kwa moja kwenye Kombe la Kagame, jamani tena tutoke hapa tuingie
kwenye mashindano mengine! Na sisi ni binadamu jamani,”alisema mchezaji mmoja
wa klabu hiyo tegemeo.
Lakini pia, BIN ZUBEIRY inatambua Azam ambao ni washindi
wa pili wa ligi hiyo, Azam watakuwa na ziara ya wiki mbili nje ya nchi
kujiandaa na msimu mpya.
MASHINDANO HAYA
YAFANYIKE DESEMBA
Tumeuona ugumu wa mashindano haya kufanyika mwezi ujao na kama
TFF itataka kulazimisha, lazima wajue kabisa hatutakuwa na mashindano bora na
hayatakuwa na tija.
Timu tatu za Bara, Simba mabingwa, Azam washindi wa pili na
Yanga wa tatu wametoka kwenye Kombe la Kagame wamechoka na wachezaji wao wengi
wameumia kwenye mashindano hayo, kutokana na kuingia kwenye michuano hiyo
wakiwa hawako fiti kimazoezi.
Tenga amecheza mpira, atakuwa anajua. Hata Angetile huwa anasema
alicheza na marehemu Saidi Mwamba Kizota huko Tabora, basi atakuwa anajua pia-
lakini Sunday Kayuni ni mwalimu anajua nina hakika na kwa kuwa ninamjua ni mtu wa
misimamo sijui ingekuwaje kama yeye ndiye angekuwa kocha wa Simba, halafu TFF
inataka kumburuza namna hii.
Kosa moja kubwa ambalo TFF wamefanya ni kutozishirikisha klabu
katika mjadala wa ujio wa mashindano haya, kwani kama wangewashirikisha basi,
leo kauli zisingepishana. Wote wangeongea lugha moja. Na ndiyo maana kuna
wakati huwa namstaajabu sana Angetile, anakuwa kama mtu ambaye hajatokea
newsroom.
TFF wanawezaje kukaa na kuamua hadi kupanga bila kuwasiliana
na wadau, klabu ambao wao ndio wanacheza mashindano hayo? Hii haijakaa sawa na
huko tunapoelekea, lazima Angetile abadilike, maana anaonekana siku hizi hata sura
yake, amekuwa mchungu mno na japokuwa hajasema, lakini inaonekana sasa anachukia
sana Waandishi wenzake, tena kuliko Rage alivyokuwa anamchukia yeye enzi zake
Nipashe.
Mimi nawashauri TFF, waanze upya taratibu za mashindano
haya, wakutane na klabu, wawaonyeshe hiyo mikataba na wapange tarahe mpya ya
mashindano yenyewe.
Ligi yetu inaanza mwezi ujao na Novemba tutamaliza mzunguko
wa kwanza- Desemba kutakuwa kuna Kombe la Challenge kabla ya kurejea kwa Ligi
Kuu Januari na Februari klabu nne kati ya nane zinazotarajiwa kushiriki
mashindano hayo zitaingia kwenye michuano ya Afrika.
Sasa tuangalie kuanzia Desemba, wapi tuyachomeke mashindano
haya, ili yawe na maana halisi ya maandalizi ya msimu mpya. Maana japokuwa sisi
ligi yetu inaanza Agosti, lakini utaona tunahitaji kuwekeza zaidi katika
maandalizi ya mwishoni mwa mwaka, kwa sababu ndio tunaelekea kwenye mashindano
makubwa, yakiwemo ya Afrika na lala salama ya Ligi Kuu.
Nimalizie tu kwa kuwapongeza tena TFF na hasa Mkurugenzi wa
Masoko bwana Jimmy Kabwe kwa kutuletea Super 8 ya Bank ABC, ila tu nawaambia
kosa moja walilofanya ni kubwa sana. Warekebishe, mambo yaende sawa. Ramadhan Karim.
0 comments:
Post a Comment