Kifaa kipya Azam, George Odhiambo 'Blackberry' |
Na Princess Asia
SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limepokea Hati ya Uhamisho
wa Kimataifa (ITC) ya mchezaji George Odhiambo ‘Blackberry’, raia wa Kenya
aliyejiunga na klabu ya Azam.
Ofisa Habari wa TFF, Boniphace Wambura Mgoyo ameiambia BIN
ZUBEIRY mchana huu kwamba, Hati hiyo imetolewa na Chama cha Soka
Denmark (DBU) ambapo Odhiambo alikuwa akicheza nchini humo kabla ya kutua Azam
kwa ajili ya msimu wa 2012/2013.
Wambura alisema klabu nyingine zinazosajili wachezaji kutoka
nje ya Tanzania zinatakiwa kuhakikisha zinakamilisha uhamisho wao (transfer)
kabla ya Julai 30 mwaka huu ambayo ndiyo siku ya mwisho kufanya hivyo.
Alisema Kanuni ya 41 ya Ligi Kuu kuhusu ITC inasema: “(1)
Maombi ya ITC kwa wachezaji wa kigeni wa kulipwa yatawasilishwa kupitia mtandao
wa kompyuta kwa kutumia program ya ‘Transfer Matching System-TMS’ baada ya
klabu zinazohusika na mchezaji huyo au wachezaji hao kukubaliana nje ya
mtandao.
Alisema Maombi ya ITC kwa wachezaji wa kigeni wasio wa
kulipwa yatawasilishwa kwa barua TFF baada ya klabu zinazohusika na mchezaji
huyo au wachezaji hao kukubaliana. Chama cha Soka kinachotoa ITC kwa njia hii
kitapeleka nakala FIFA. (3) ITC haihitajiki kwa mchezaji mwenye umri chini ya
miaka kumi na mbili (12).”
“Tunapenda kuzikumbusha klabu kuwa kwa mujibu wa Kanuni ya
53 ya Ligi Kuu, wachezaji wa kigeni ni lazima wawe wanachezea timu ya Taifa au
klabu za Ligi Kuu huko wanakotoka,”alisema.
Alisema Kanuni hiyo inasema: “Klabu inaruhusiwa kusajili
wachezaji wa kigeni wa ngazi ya kimataifa ambao ni wa timu za Taifa na Ligi Kuu
kutoka nje ya nchi wasiozidi watano (5). Wachezaji kutoka Ulaya na Marekani ya
Kusini wanweza kuwa wa daraja la pili na kuendelea, na klabu inaruhusiwa
kuchezesha wachezaji walioorodheshwa wasiozidi watano (5) wa kigeni katika
mchezo mmoja. Wachezaji hao watasajiliwa baada ya TFF kuhakikisha usahihi wa
taarifa zao na kukamilika kwa taratibu za uhamisho wa kimataifa.”
0 comments:
Post a Comment