Ibrahim Rajab Jeba |
Na Prince Akbar
SIMBA SC wanalo mwaka huu. Walimsajili Ibrahim Rajab Jeba wa
Azam na akajiunga nao, lakini hivi unaposoma habari hii, mchezaji huyo jana
ameongeza mkataba wa mwaka mmoja kuendelea kuwachezea ‘Watoto wa Chamazi’ na
tayari amerejea rasmi kwenye klabu hiyo, inayomilikiwa na Said Salim Bakhresa
na familia yake.
Hii inakuja katika wakati ambao, Simba ina machungu ya
kupokonywa beki wake, Kevin Yondan aliyehamia Yanga, wakati inadai bado ina
mkataba naye.
Msemaji wa Azam FC, Jaffar Iddi Maganga ameiambia BIN
ZUBEIRY leo asubuhi kwamba, Jeba alikwenda kuzungumza na uongozi wa
Azam jana akaomba radhi kwa kitendo chake cha kuukiuka mkataba wake na kuomba
kurejeshwa kundini.
“Kwa kweli uongozi umemsamehe kabisa na amerejeshwa kundini
na hivi navyozungumza na wewe yuko kwenye himaya ya Azam. Mkataba wake wa sasa
unaisha Desemba mwaka huu, lakini jana hiyo hiyo ameongeza mkataba na Azam hadi
2013,”alisema mtangazaji huyo wa zamani wa Radio One na ITV, aliyewahi
kuandikia pia gazeti la Nipashe.
Jeba aliibukia katika akademi ya Azam FC na msimu uliopita
alitolewa kwa mkopo Villa Squad ya Kinondoni, ili akapate uzoefu wa Ligi Kuu,
hata hivyo kwa bahati mbaya aliumia na hakucheza ligi, lakini mwishoni mwa
msimu, Simba SC wakamsajili.
Hata hivyo, uliibuka mvutano mkubwa baina ya klabu hizo
mbili, Azam ikilalamika kupokonywa mchezaji kimabavu na Simba SC, lakini ajabu
mchezaji huyo Wekundu wa Msimbazi hawakumtumia kabisa hata kwenye mechi za
kirafiki hadi jana anarejea Chamazi.
0 comments:
Post a Comment