BIN ZUBEIRY na Saintfiet |
Na Mahmoud Zubeiry
“NIMEKUWA nikisikia habari nyingi kuhusu Yanga, ni timu
kubwa. Na ninafurahi kuja hapa, naamini nitafanya vizuri,”.
Ndivyo alivyoanza kuzungumza, Thom Saintfiet katika
mahojiano na BIN ZUBEIRY mchana huu, baada ya kuwasili Dar es Salaam, tayari
kusaini mkataba na kuanza kufundisha klabu hiyo.
Thom amepata mapokezi makubwa baada ya kuwasili na moja kwa
moja alipelekwa makao makuu ya klabu, makutano ya mitaa ya Twiga na Jangwani,
Dar es Salaam. Akiwa hapo, alionyeshwa ofisi na mataji mbalimbali ya klabu hiyo
pamoja na Uwanja wa mazoezi na gym.
“Sifahamu sana kuhusu Yanga au Tanzania kwa ujumla, naamini
mengi nitajifunza hapa, ila mimi kama mwalimu baada ya kukubali kuja Tanzania
kufundisha, nilianza kujifunza kidogo kuhusu nchi hii na hususan Yanga,”alisema
Thom alipoulizwa kama anaifahamu Yanga au soka ya Tanzania.
Kwa nini ameamua kuja kufanya kazi Tanzania, hususan Yanga?
“Imetokea nimekubali, lakini nilikuwa nina ofa nyingine, ila nimetaka
kubadilisha uzoefu wangu kwa sasa, kuwa kocha wa klabu badala timu za
taifa,”alisema.
Thom Saintfiet akiwa na Kombe la Kagame |
Jukumu lake la kwanza Yanga ni nini? “Kwa sasa unaliona Kombe
lile (la Afrika Mashariki na Kati), nataka liendelee kuishi kwenye ofisi hii (ya
Katibu wa Yanga), nina muda mfupi sana, lakini najua Yanga walitwaa Kombe lile
mwaka jana na wanatakiwa kulitetea karibuni, nina uhakika hilo ndilo jukumu
langu la kwanza,”alisema.
Alipoulizwa kuhusu muda, Saintfiet alisema kwamba Yanga
imekuwa chini ya mwalimu msaidizi na ni mwalimu mzuri, hivyo anaamini alikuwa
anafanya kazi yake vizuri. “Nitaungana naye, nianzie pale alipoishia tufanye
pamoja kwa kushirikiana kuhakikisha, kwanza Kombe linabaki hapa.
Na viongozi wamenihakikishia timu ina wachezaji wazuri,
nimeomba DVD za timu za karibuni ili nione wanachezaje katika mechi, na
nikianza kazi naamini kila kitu kitakuwa sawa, Yanga ina wachezaji profesheno
na wanajua wajibu wao, hivyo najua watakuwa vizuri na tutaelewana,”alisema.
Amesikia kuhusu Simba?
“Nimesikia kuhusu Simba, viongozi wangu wameniambia, nchi
yenye timu za aina hii (wapinzani wa jadi), lazima soka yake inakuwa na msisimko
mkubwa. Na upinzani huu ni changamoto kwangu. Lazima Yanga iongoze kila wakati.
Najua kuna timu nyingine inasifika, Azam FC. Lakini mimi ni mpinzani wa kila
timu ninayokutana nayo, na ninataka ushindi kila siku,”anasema.
Ametokea wapi huyu jamaa?
Tom Saintfiet anasema alizaliwa Machi 29, mwaka 1973 mjini
Mol, Ubelgiji na kabla ya kuwa kocha alicheza soka katika nafasi ya kiungo
kuanzia mwaka 1983 hadi 1997 alipostaafu na kuwa kocha akiwa ana umri wa miaka 24,
akiweka rekodi ya kocha kijana zaidi kuwahi kutokea katika soka ya Ubelgiji.
Saintfiet anasema amefundisha nchi kadhaa kuanzia kwao
Ubelgiji, Qatar, Ujerumani, Visiwa vya Faroe, Finland na Uholanzi.
Anasema pia ana uzoefu wa kutosha wa kufundisha soka Afrika
akiwa amefundisha Namibia na Zimbabwe kama kocha Mkuu wa timu za taifa za nchi
hizo.
Anasema kabla hajakwenda Namibia, Saintfiet alikuwa kocha wa
klabu ya Ligi Kuu Finland, iitwayo RoPS Rovaniemi na mwaka 2002, alikwenda
kuifundisha B71 Visiwa vya Faroe ambayo aliiwezesha kushika nafasi ya pili
katika Ligi Daraja la kwanza. Anasema kutoka hapo, akaenda kuwa kocha wa Al-Ittihad
Sports Club ya Qatar (sasa inaitwa Al-Gharafa SC) ambako alidumu hadi mwaka 2004
alipochukuliwa kuwa kocha wa timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17
ya Qatar.
Anasema akiwa na U17 ya Qatar, aliiwezesha kushika nafasi ya
tatu katika Kombe la Mataifa ya Asia na hivyo kufuzu kucheza Fainali za vijana
za Kombe la Dunia la FIFA. Kuelekea Fainali za Kombe la Dunia mwaka 2010,
Saintfiet anasema alikuwa kwenye mpango wa kupewa timu ya taifa ya Nigeria,
Super Eagles, wakati huo akiwa Mkurugenzi wa Ufundi wa Shirikisho la Soka la
nchi hiyo.
Anasema katika timu za taifa, mafanikio zaidi alipata akiwa
na Namibia kwanza akiifikisha robo fainali ya michuano ya COSAFA kwa kuzifunga Comoro
na Malawi na kutoka sare na Lesotho katika fainali zilizofanyika Afrika Kusini
Julai mwaka 2008.
Hata hivyo, anasema Namibia ilitolewa na Afrika Kusini
katika robo fainali, ambao mwishowe waliibuka mabingwa wakiwa wenyeji.
Anasema mafanikio yake akiwa na Namibia ni pamoja na
kuifunga Zimbabwe 4-2 katika mechi ya kuwania tiketi ya kucheza fainali za
Kombe la Dunia mwaka 2010 na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) 4-0 katika
mchezo wa kirafiki.
Anasema alipata heshima kubwa akiwa Namibia, kiasi cha
kufikia hadi kuitwa ‘Nabii’ na Mtakatifu.
Anasema sababu ni kwamba, aliifanya Namibia ikawa inacheza
soka nzuri na kupata pia mafanikio, ndiyo maana akawa anatukuzwa mno nchini
humo.
Thom Saintfiet akizungumza na Waandishi wa Habari, makao makuu ya Yanga, Jangwani. Kulia ni Katibu wa Yanga, Celestine Mwesigwa na kushoto mmoja wa wafadhili wa klabu hiyo, Seif Ahmad 'Magari'. |
Anasema moja ya matukio ya kukumbuka ni siku tatu baada ya
kutoka sare 1-1 ugenini na Lebanon Aprili mwaka 2009, Namibia ilipata matokeo
ya kuvutia ya sare ya bila kufungana ugenini na Angola.
Lakini matokeo mazuri zaidi na yaliyomfurahisha ilikuwa ni
mjini Durban, wakati Namibia ilipotoa sare ya 1-1 na Afrika Kusini, baada ya
kuongoza sehemu kubwa ya mchezo huo. Anasema kwa miezi kadhaa, Namibia ilikuwa
imeshinda mechi moja tu kati ya 12 kabla ya kuwasili kwake nchini humo.
“Baada ya mafanikio makubwa, vyombo vya habari Namibia
vilinipa jina la utani The Saint (Mtakatifu) na gazeti moja lilidiriki kuniita The
Messiah (Nabii).
Baada ya hapo alisaini mkataba wa miaka minne na Shirikisho
la Soka Zimbabwe (ZIFA) Oktoba 1, mwaka 2010, lakini anasema kutokana na
matatizo ya kutopewa kibali cha kufanya kazi nchini humo, alifanya kazi katika
mazingira magumu, hadi Desemba mwaka 2010 alipoamua kubwaga manyanga na
kujiunga na Shabab Al Ordon.
Anasema alisaini mkataba wa miezi minne na mabingwa hao wa
Ligi ya Mabingwa Asia mwaka 2007, Shabab Al Ordon na alifanya kazi nzuri ya
kutukuka huko, akijenga ukuta imara ambao katika mechi tano uliruhusu bao moja
tu.
“Baada ya mechi sita, tukishinda tatu na kutoka sare tatu, nilitosheka
na nikaiacha timu ikiwa katika nafasi ya pili na haijafungwa,”alisema.
Anasema baada ya kupokea ofa kutoka timu tatu za taifa za
Afrika, aliikubali ya Ethiopia na mwishoni mwa Mei mwaka 2011 akaanza kazi.
Baada tu ya kusaini mkataba, Saintfiet anasema ndani ya siku
10 alikuwa ana mtihani mzito wa kucheza na Nigeria kuwania tiketi ya kucheza
Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika 2012.
“Nigeria ilikuwa imetoka kuifunga Argentina 4-1 siku nne
kabla ya mechi yetu na wao na pia iliifunga Ethiopia 4-0 katika mechi ya kwanza
ya AFCON nyumbani, lakini hadi mapumziko niliiongoza timu kumaliza kwa
kufungana 1-1. Tulifanikiwa kupata bao la kuongoza kipindi cha pili, lakini kwa
bahati mbaya beki Joseph Yobo akasawazisha ikawa 2-2 mwisho wa mchezo,”anasema.
Kwa mara nyingine, Saintfiet anasema akajizolea sifa kemkem
kwa staili yake ya ufundishaji baada ya kuifanya Ethiopia kuwa timu ya
ushindani yenye kucheza soka maridadi hata dhidi ya vigogo kama Nigeria.
“Baada ya mechi, kocha wa Nigeria, Samson Siasia alisema
amestaajabishwa mno na soka ya kitaalamu na nidhamu ya hali ya juu ya Ethiopia
na Nigeria hawakupata majibu. Licha ya kukubalika sana, lakini Oktoba 28, mwaka
jana nilijiuzulu, baada ya kupata ofa ya Nigeria” anasema.
Machi 28, mwaka huu, Mbelgiji huyo anasema alipewa mkataba
wa miaka minne wa kuwa Mkurugenzi wa Ufundi wa Nigeria, lakini Juni, mwaka huu
akaamua kuvunja mkataba huo baada ya kuvutiwa na ofa ya Yanga.
NONDOZ ZA ‘MTAKATIFU’
THOM
Saintfiet anasema ana leseni Shirikisho la Soka Ulaya (UEFA)
ya kufundisha soka ya kulipwa popote barani humo, ambayo aliipata mwaka 2000.
Anasema kati ya mwaka 2006 na 2007 alikuwa Mkurugenzi wa
Ufundi wa FC Emmen ya Daraja la Kwanza Uholanzi na pia amewahi kufanya kazi kama
Mshauri wa Ufundi wa Shirikisho la Soka la Kazakhstan.
Anasema amewahi kuwa
Mchambuzi wa soka katika Televisheni katika nchi za Ubelgiji, Afrika Kusini na
Namibia na alifanya kazi kama mkalimani DFB. Anasema amesomea Saikolojia ya
Michezo na Uchumi.
Anasema anazungumza lugha kibao na kwa ufasaha zaidi ni
Kiholanzi, Kiingereza, Kifaransa, Kijerumani, Kifaroe na ‘ana jua jua’ Kiarabu,
Kiafrikana na Kispanyola.
Naam huyo ndiye Thom Saintfiet, ambaye anatarajiwa kusaini mkataba
wa kuinoa Yanga, akiwa tayari amekuja nchini kikamilifu. Je, Yanga imepata
mwalimu? Je, watadumu naye? Je, hayatajirudia yale yale? Bila shaka hayo ni
mambo ya kusubiri na kuona, ila kwa mujibu wa wasifu wake, huyu ni mwalimu wa
uhakika.
0 comments:
Post a Comment