Na Mahmoud Zubeiry |
KUNA mawazo potofu ndani ya Simba na sijui yanatokea wapi. Mawazo
potofu, ambayo kama yataachwa yaendelee kufanya kazi yatazidi kuivuruga klabu
hiyo.
Hivi sasa kuna kampeni ya ‘Simba haina washambuliaji’
inaendelea, ambayo unaweza kuona lengo lake ni kuwapiga zengwe washambuliaji
waliopo. Na ukiitazama kwa kina, unaweza kuona kuna mtu ndani ya Simba, kwa
ubinfasi wake hamtaki mshambuliaji Abdallah Juma, ambaye tayari amekwishawadhihirishia
wana Simba ana uwezo.
Kuna mtu anaaminiwa na kuogopgwa hata na viongozi wakuu
ndani ya Simba SC, kiasi huyo sasa ndiye unaweza kumuita mwenye Simba yake. Naye
hutamba hivyo; “Timu yangu….”. kosa kubwa, Simba siyo timu ya mtu, ni timu ya
watu.
Mapema tu Abdallah Juma aliposajiliwa chombo kimoja cha habari
kikamkandia Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ kwamba
kajiamulia mwenyewe kumsajili mshambuliaji huyo kutoka Ruvu Shooting, bila
kushirikisha Kamati ya Utendaji.
Dullah Mabao |
Na kwa kudhihirisha mtu huyo anaogopwa na hadi viongozi
wakuu wa Simba, ilibidi Kaburu ajitetee kwamba mchezaji huyo hajasajiliwa, bali
ameenda kufanya majaribio. Inasikitisha kuona kwamba hadi dunia ya leo Miungo
watu bado wapo!
Kampeni za kumpinga mshambuliaji huyo zimeendelea na unaweza
kujionea pamoja na kuanza kufanya vizuri tangu kwenye mechi za kirafiki, lakini
bado imekuwa vigumu kwake kuaminiwa katika kikosi cha kwanza.
Sitaki kuamini haya ni mawazo ya Profesa Milovan Cirkovick-
naamini ni shinikizo kutoka nje ya benchi la ufundi.
Real Madrid leo wanakwenda mbio kuwania saini ya Luca Modric
kutoka Tottenham Hotspur, lakini huwezi kujua ni chaguo la nani kati ya kocha
Jose Mourinho na rais Florentino Perez- hivyo haiwezi kuwa ajabu hata Tanzania,
Makamu wa Rais wa Simba akisajili.
Hadi wanachama kufikia kumpa kura za kutosha Kaburu kuwa
Makamu wao, walimuamini kwamba ni mtu wa mpira na wakampa dhamana- hivyo yeye
kusajili si kosa.
Na pia mtu anayeweza kuidhinisha au kukwamisha usajili wa
mchezaji ni mwalimu na si Kamati ya Ufundi wala ya Utendaji, labda kuwe kuna
sababu nyingine nje ya mpira.
Lakini kwa nini basi tusikubali amefanya ubinfasi wenye
manufaa, kwa kusajili mchezaji mzuri ambaye leo anaelekea kuwa kinara wa mabao
wa timu?
Namfahamu Salim Kinje, mwaka 1999 alikuwa kwenye kikosi cha
timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20 pamoja na akina Jemedari
Said, Yahya Issa, Simon Butte na wengineo, ambao hivi sasa wamekwishatundika
daluga wote.
Nani kamsajili huyu Simba, ni Kaburu au Milovan? Akina Juma
Kaseja, Haruna Moshi ‘Boban’, ambao hivi sasa wanaitwa ‘wazee’ waliibukia
kwenye kikosi cha timu ya vijana chini ya umri wa miaka 17, mwaka 2000 chini ya
makocha Ernest Mokake na Juma Matokeo, ambao wote hivi sasa ni marehemu.
Tazama Simba inavyojikwaa na kesho wasije kujiuliza
walinguka kwa sababu gani. Mawazo potofu ndani ya Simba yalisababisha akaachwa beki
Haruna Shamte na kiungo Amri Kiemba, ambao unaweza kuona wanacheza vizuri
kikosini hivi sasa, baada ya kurejeshwa kwa shinikizo la kocha.
Sijui haya mawazo potofu yanatoka wapi, lakini kwa haraka
naweza kusema udhaifu unaanzia kwenye Kamati ya Utendaji chini ya Mwenyekiti
Alhaj Ismail Aden Rage, kuwapa watu majukumu mazito kuliko uwezo wao.
Ibrahim Masoud ‘Maesrto’ ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi
ya Simba SC; huu ni mzaha. Simba imeishiwa kiasi gani hadi kuwa na Mwenyekiti
wa Kamati ya Ufundi aina ya huyu?
Hii ni klabu kubwa yenye wachezaji wengi wastaafu wenye
taaluma ya ukocha na wazoefu, weledi wa masuala ya soka- lakini kwa kile ambacho nakiita udhaifu
unaoanzia kwenye Kamati ya Utendaji ndio chanzo cha yote haya.
Ndiyo maana sasa anasimama mtu anasema Simba ina tatizo la
washambuliaji, kisa imewafunga vibonde Ports ya Sudan mabao matatu tu, lakini
mtu huyu anashindwa kuurejea mchezo ulivyokuwa na kujiuliza timu ilitengeneza
nafasi ngapi za kufunga mabao na ikatumia ngapi?
Miguuni mwa Felix Sunzu pekee, Simba ilipoteza mabao sita ya
wazi, kama angefunga angalau matatu- ingekuwaje? Dullah Mabao pamoja na kufunga
mara mbili, lakini alikosa bao moja la wazi sana kipindi cha pili. Na hapa
tunaiweka wapi kauli ya wenye soka yao, Football is the game of chance?
Tunapenda kufanya mambo kwa mazoea, kwa sababu Ports ilifungwa
saba na AS Vita, basi Simba nayo ilistahili kushinda saba- hapana soka haiko hivyo.
Juni 1, mwaka 2002, Ujerumani iliitandika Saudi Arabia mabao
8-0 katika Fainali za Kombe la Dunia, Korea Kusini na Japan, lakini Cameroon
iliyoonekana kutopishana sana makali na Wajerumani, tena wakiongozwa na Samuel
Eto’o bado kijana mdogo, walishinda 1-0 kwa mbinde. Hii ndiyo soka.
Lakini kwa nini uwadanganye wana Simba timu ina tatizo la
washambuliaji wakati kuna Felix Sunzu, Danny Mrwanda, Haruna Moshi na Dullah
Mabao?
Mfumo unaotawala katika dunia ya soka ya leo ni kutumia viungo
wengi na mshambuliaji sana mmoja tu- je hadi hapa bado unaweza kusema Simba ina
washambuliaji wachache?
Simba ina viungo wa kutosha kabisa, akina Uhuru Suleiman,
Mussa Mudde, Kanu Mbivayanga, ‘Babu’ Kinje, Kiggi Makassy, Christopher Edward, Mwinyi Kazimoto, Jonas Mkude, Amri Kiemba na sijui nimemsahau nani hapa. Bado Emmanuel Okwi yuko
mguu nje ndani, anaweza kufeli majaribio (simuombei hivyo) na akarudi Simba
kama alivyoahidi.
Mwenyekiti wa Simba Alhaj Ismail Aden Rage kulia, akishuhudia kocha Milovan Cirkovick anavyosaini mkataba mwaka jana, kushoto ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi ya Simba SC, Ibrahim Masoud 'Maestro'. |
NINI TATIZO LA SIMBA?
Alichosema Milovan kwenye Mkutano na Waandishi wa Habari
leo, kwamba timu bado ni mpya wachezaji hawajazoeana ndicho ambacho hata mimi
naunga mkono. Matatizo madogo madogo ya kufunga mabao yataisha timu itakapozoeana.
Soka ina wigo mpana sana na inahitaji muda wa kutosha
kujifunza kabla ya kuanza kujiona wajuaji, kisa tu tunapewa pewa nafasi ya kuandika
andika kwenye kurasa za magazeti au kuzungumza kwenye vipindi vya Radio na
Televisheni. Hapana.
Mshauri wa Ufundi wa Enyimba FC International anaitwa Abdu
Maikaba, ambaye wakati fulani mwaka jana alikuwa kocha wa muda wa timu, baada
ya kufukuzwa kwa Evans Ogenyi kutokana na matokeo mabaya.
Huyu jamaa ana umri wa miaka 46, alizaliwa mwaka 1965, na alianza
ukocha katika klabu ya Kano Pillars, kabla ya kwenda Buffalo FC, badaaye, FC Abuja alikokuwa Kocha Mkuu hadi anaingia
Enyimba mwaka 2009, kwanza kama kocha Msaidizi.
Naomba wasifu wa Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi ya Simba SC,
halafu niambie kwa nini asiwe Zamoyoni Mogella, Khalid Abeid, au Abdallah ‘King’
Kibadeni, aliyeitwa Chifu Mputa Songea?
Namaliza kwa kuweka msistizo, Simba haina tatizo la
washambuliaji, bali timu haijakaa sawa na inahitaji muda wa kutosha wa maandalizi.
Hizi ni salamu zangu kwa wana Simba wote. Alamsiki.
Danny Mrwanda, mshambuliaji hatari hadi taifa linajua, unasemaje Simba haina washambuliaji? |
0 comments:
Post a Comment