Na Mahmoud Zubeiry |
KATIKA mechi za ufunguzi za Klabu Bingwa Afrika Mashariki na
Kati, Kombe la Kagame, timu pekee ya Tanzania iliyofanya vizuri ilikuwa ni Azam
FC, ambayo ilitoka sare ya 1-1 na Mafunzo ya Zanzibar katika mchezo wa Kundi B.
Timu nyingine za Tanzania zilianza vibaya, Simba waliopo
Kundi A walifungwa 2-0 na URA ya Uganda na watani wao wa jadi, Yanga waliopo
Kundi C, walichapwa 2-0 pia na Atletico ya Burundi.
Timu zetu zilizidiwa uwezo kisoka na wapinzani katika mechi
za kwanza na hata mashabiki walikiri, lakini ajabu wanatokea watu wanazilaumu
klabu.
Zilaumiwe kwa nini? Lipo tatizo la msingi ndani ya
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ambalo linasababisha timu za Tanzania
kuonyesha kiwango kibovu katika michuano ya Kagame.
Rejea mwaka jana, michuano hiyo ilifanyika Tanzania pia na
timu zote za nyumbani ziliingia fainali, maana yake Kombe lilibaki, lakini
hazikucheza soka ya kuvutia.
Hii ni kwa sababu TFF, wanapopokea uenyeji wa michuano hii,
wanachojali ni maslahi yao tu na hawajali kama timu za nyumbani ziko tayari kwa
mashindano au la.
Kuingia kwenye mashindano haya, timu nyingine zimetoka moja
kwa moja kwenye ligi zao na nyingine zimetoka kumaliza ligi muda si mrefu,
lakini Tanzania ligi iliisha mwezi wa nne.
Timu zimefanya usajili mwezi Julai na timu zote rasmi
zilianza mazoezi mwishoni mwa Juni na nyingine kama Simba na Yanga Julai
mwanzoni- ndani ya wiki mbili zinatakiwa kucheza Kombe la Kagame.
Ni hatari kwa wachezaji, kuwaingiza kwenye mashindano kabla
hawajawa fiti kwa mazoezi wanaweza kuumia na kukaa nje ya Uwanja kwa muda
mrefu. Wachezaji kuanza msimu kwa kuzomewa inawavunjia kujiamini na kujenga hatari
ya kutofanya vizuri msimu mzima.
Inashusha thamani ya soka yetu; mashindano yanaonyeshwa na Super
Sport TV, watu nchi mbalimbali wanaona jinsi Yanga walivyokuwa wakiutafuta
mpira kwa tochi mbele ya Atletico au Simba mbele ya URA, tunadharaulika.
Umefika wakati sasa, TFF wajiulize, kwa nini wasishirikiane
kikamilifu na klabu zetu kuelekea katika michuano hiyo, ili wakubaliane kupeana
muda wa kutosha wa maandalizi kabla ya mashindano, ili badala ya kuingia
gharama za kuwaagiza marefa wazipendelee Simba na Yanga, tuwekeze kwenye
maandalizi mazuri?
Ukirejea historia ya michuano ya Kombe lenyewe la Kagame
tangu inatambulika kama Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati tu, ilikuwa
inafanyika mwanzoni mwa mwaka.
Kama inavyofahamika, michuano hii hushirikisha klabu bingwa
za nchi za ukanda huu, ambazo kwa mujibu wa kanuni hushiriki pia michuano ya
Ligi ya Mabingwa Afrika.
Kwa hakika kufanyika kwa michuano hii mwanzoni mwa mwaka
kulikuwa kunasaidia mno maandalizi ya klabu zetu kwenye michuano ya Afrika,
kwani zikitoka kwenye michuano hiyo tu huhamia katika mashindano ya CAF.
Kutokana na uzembe au uvivu wa viongozi wa klabu zetu, Kombe
la Kagame kufanyika Januari ilikuwa inazisukuma klabu kuanza mapema maandalizi
ya msimu, ikiwemo michuano ya Afrika.
Simba SC |
Kwa kawaida raundi ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika
hufanyika kuanzia Februari, ambayo inakuwa siku kadhaa tangu kumalizika kwa
Kagame enzi hizo za kuanza mwanzoni mwa mwaka.
Hivyo kwa timu ambazo zinapigana hadi kufika angalau hatua
ya Nusu Fainali katika Kombe la Kagame, hakika huingia kwenye michuano ya
Afrika zikiwa zimepata maandalizi ya kutosha kidogo.
Mifano iko wazi, mabingwa wengi wa Kagame au wana fainali,
ndio ambao hufika mbali kwenye michuano ya Afrika.
Mfano mabingwa wa mwaka 2002 wa Kagame, Simba SC na wana
fainali wa mwaka 2003 waliofungwa na SC Villa ya Uganda 1-0 mjini Kampala,
mwaka huo, walifanya makubwa kwenye michuano ya Afrika 2003.
Waliivua ubingwa Zamalek ya Misri na kukata tiketi ya
kucheza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Hata miaka ambayo timu
zetu zilikuwa hazifiki mbali, lakini zilikuwa zinaonyesha ushindani kwenye
michuano ya Afrika.
Hakika michuano hii kufanyika mwanzoni mwa mwaka ilikuwa ina
manufaa mno kwa klabu za ukanda wetu zinazoingia kwenye michuano ya Afrika,
lakini kwa sasa ukweli ni kwamba mabadiliko ya kalenda ya michuano hiyo kutoka
kufanyika mwanzoni mwa mwaka hadi katikati, hayana tija tena.
Michuano hii inafanyika wakati ambao kwa mfano ligi ya
Tanzania imemalizika, hivyo wachezaji wanaitwa kutoka mapumziko kwa maandalizi
ya muda mfupi ili waende kwenye michuano hiyo.
Angalau mwaka juzi Simba waliingia kwenye michuano hiyo
wakitoka kutolewa kwenye raundi ya Pili ya Kombe la Shirikisho Afrika na Haras
El Hodoud ya Misri, hivyo kikosi chao kilikuwa bado kipo tayari kwa mashindano.
Yanga SC |
Lakini mwaka jana, Simba walikuwa wamekwishavunja kambi na kuanza
kujenga upya timu yao chini ya kocha mpya, Moses Bassena aliyemrithi Patrick
Phiri. Basena tayari amefukuzwa na sasa Simba inafundishwa na Mserbia, Milovan
Cirkovick.
Ndiyo, Simba ilifika fainali na kufungwa na watani wa jadi,
Yanga 1-0, lakini kwa ujumla timu zetu zilizidiwa viwango na timu za nje na
mechi nyingi za mtoano matokeo yake yalikuwa ya utata.
Hii ni kwa Tanzania, lakini hatujui nchi nyingine ratiba hii
ya Kagame kuwa katikati ya mwaka inawaathiri vipi.
Lakini kikubwa ni kwamba CECAFA ambayo Mwenyekiti wake ni
Leodegar Chillah Tenga, pia ni Rais wa TFF, inapaswa kulifikiria mno suala la
kalenda ya Kagame kuwa katikati ya mwaka badala ya mwanzoni mwa mwaka.
Lakini hoja ya msingi hapa, CECAFA inaelekea kama kuyafanya
mashindano haya yawe ya kudumu katika ardhi ya Dar es Salaam- sasa kama
mashabiki wataamini kwamba, mashindano haya yapo kwa ajili ya kuzibeba Simba na
Yanga, yatakosa msisimko na yatapoteza maana.
Bora timu zetu zitolewe mapema, zikiwa zimecheza soka nzuri,
kuliko kufika fainali kwa kucheza soka mbovu mbovu- unajua hapa ni nini? Tunajidanganya
wenyewe.
Nina wasiwasi, dhuluma walizofanyiwa mwaka jana timu za
Sudan na Ethiopia zimesababisha mwaka huu wasilete timu, kwa visingizio walivyotoa.
Sudan kwa mfano, timu zao tatu zinashiriki michuano ya Afrika,
wameshindwa kuleta hata timu ya nne? Mbona ile nchi ina timu nyingi imara? Hili
linawahusu CECAFA, ila TFF nawaambia wafikirie namna ya kuziwezesha Simba na
Yanga kushiriki kwa ufanisi, kuliko hivi wanavyotuaibisha. Watu hawajiamini na
timu zao bana!
Azam FC |
0 comments:
Post a Comment