Na Princess Asia
MWILI wa kiungo wa zamani wa Simba SC, Issa Kihange aliyefariki
dunia jana maeneo ya nyumbani kwake, Mbezi Jogoo, Dar es Salaam baada ya
kuanguka uwanjani wakati akicheza mechi za maveterani, unatarajiwa kusafirishwa
kesho asubuhi kuelekea Dodoma kwa mazishi.
Kipa aliyecheza pamoja na Kihange Simba 1991 na 1992, Iddi
Pazi ‘Father’, ameiambia BIN ZUBEIRY jioni hii kwamba, mama wa
marehemu amewasili leo Dar es Salaam na taratibu za mazishi zinaendelea na
imeamuliwa kiungo huyo mchezeshaji wa zamani wa Wekundu wa Msimbazi mwili wake
ukastiriwe Dodoma.
Vyanzo vilisema jana kwamba, Kihange alianguka wakati
akishangilia bao alilofunga mazoezini uwanjani hiyo jana na baada ya hapo,
alikimbizwa hospitali ya IMTU, Mbezi Interchick ambako umauti ulimfika.
Issa Kihange alikuwamo na aling’ara kwenye kikosi cha Simba
kilichotwaa taji la pili Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame
mwaka 1991 mjini Dar es Salaam, hiyo ikiwa ni mara ya kwanza tangu walipotwaa
mwaka 1974 Dar es Salaam.
Marehemu Issa alijiunga na Wekundu wa Msimbazi mwishoni mwa mwaka
1990, akitokea CDA ya Dodoma ambako aling’ara katika msimu wa Ligi Daraja la
Kwanza (sasa Ligi Kuu) Tanzania Bara mwaka 1990.
Aliichezea Simba kwa misimu miwili mfululizo na kwa
mfanikio, 1991 na 1992 kabla ya kutemwa mwaka 1993 na hakuna uhakika kama
aliendelea soka baada ya kuondoka Msimbazi.
Aliondoka Simba na Medali mbili za Dhahabu za Kombe la
Kagame, mbali na ile aliyovalishwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam (sasa Uhuru)
1991, wakiifunga SC Villa ya Uganda kwenye fainali mabao 3-0, pia alivalishwa
Medali nyingine mwaka 1992, Uwanja wa Amaan, Zanzibar walipoifunga Yanga kwa penalti
5-4 kufuatia sare ya 1-1 ndani ya dakika 120.
0 comments:
Post a Comment