Na Mahmoud Zubeiry |
FELIX Mumba Sunzu Jr. anaonekana kutokuwa vizuri kwa sasa kutokana
na kiwango chake katika Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame,
inayoendelea Dar es Salaam, kiasi cha kushindwa kuisaidia klabu yake, Simba SC.
Kwa mara nyingine, jana Sunzu aliwadhihirishia wapenzi wa
Simba hayuko tayari kucheza- baada ya kupoteza nafasi nyingi, tena za wazi za
kufunga.
Hayuko fiti? Hapana, yuko fiti ndio maana anamudu dakika 90,
anahaha uwanja mzima, anafungua pembeni, anakimbia, anarudi kusaidia ulinzi-
lakini inaonekana tatizo lipo kichwani mwake na si mwilini.
Kuna matukio matatu jana yanaweza kuwa mfano kama ana
matatizo kichwani; moja ni pasi tatu za mwisho nzuri alizopata kipindi cha
kwanza, baada ya kujiweka mwenyewe kwenye nafasi, lakini akiwa anatazama na
kipa, alishindwa kufunga.
Sunzu katika mechi na Yanga msimu uliopita, alikuwa moto |
Alishindwa kumsoma kipa na lango lake, akajipigia tu kwa
kubahatisha. Hakuiruhusu akili yake kufanya kazi. Kipindi hicho hicho cha
kwanza, alijiweka kwenye nafasi ya kuomba basi akiwa kwenye eneo la hatari la
wapinzani, lakini pasi ilimgonga mguuni na kuondoka, akibaki anasikitika.
Kipindi cha pili kadhalika, Sunzu alipoteza nafasi nyingine
mbili za wazi- kabla ya kufunga kwa penalti. Huyu siye Sunzu tunayemjua,
mfungaji bora wa zamani wa Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati,
Challenge.
Haiingii akilini Sunzu hayuko fiti- hapana ana tatizo labda
linalomuathiri kisaikolojia na unaweza kuwaza mambo mengi, kwa sababu mchezaji
naye ni binadamu. Labda kifo cha marehemu Patrick Mafisango, aliyekuwa rafiki
yake na waliyekuwa wakicheza naye kwa uelewano mkubwa msimu uliopita.
Kumbuka; Sunzu mama yake ni raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia
ya Kongo (DRC) na baba yake ndiye Mzambia na marehemu Mafisango alikuwa Mkongo
pia. Lakini labda inawezekana Sunzu ana tatizo lingine tu kichwani mwake,
ambalo linamuathiri kisaikolojia kwa sasa.
Wangapi miongoni mwetu wapenzi wa soka wanakwenda ofisini
kufanya kazi wakiwa wana matatizo kichwani na matokeo yake ufanisi unakuwa
duni? Wachezaji nao ni binadamu. Kwangu Sunzu ni mshambuliaji hatari- lakini
naamini kwa sasa hayuko sawa kisaikolojia, tatizo ambalo limekuwa likiwaathiri
wachezaji wengi duniani.
Wakati mwingine hata mchezaji kutotimiza ndoto zake,
humuathiri kisaikolojia. Kama kuna mtu aliyekuwa naye kwenye kikosi cha Zambia
katika Fainali za Mataifa ya Afrika mwaka 2008 ambaye kwa sasa anacheza Ulaya,
hilo linaweza likawa linamuumiza kichwa pia Sunzu.
Kumbuka mchezaji huyu wa zamani wa Konkola Blades ya Zambia
na anayeichezea pia timu ya taifa ya nchi hiyo, Chipolopolo, aliachwa na Al
Hilal ya Sudan wakati huo ikiwa chini ya Milutin Sredojevic ‘Micho’ ikiwa ni
miezi sita tu tangu asajiliwe.
Al Hilal waliamua kuvunja mkataba na Sunzu, baada ya
mshambuliaji huyo kudaiwa kuonyesha kiwango kibovu na kuzidiwa ujanja na
Mzimbabwe Sadomba, aliyeonekana kufumania mno nyavu.
Sunzu Jr alionwa na Micho, baada ya kuonyesha kiwango
kikubwa katika michuano ya Kombe la Challenge mwaka 2010, na kuwa mfungaji bora
akiichezea Zambia.
Kwa muda Sunzu, anaonekana kama anayehangaika barabarani na
kushindwa kutulia katika timu moja kwani baada ya kuwemo katika kikosi cha
Zambia 2008, alichukuliwa na Al Masry ya Tunisia, ambako nako alitemwa kwa
sababu kama hizo.
Felix Mumba Sunzu Jr. akiwa na Obadia Mungusa |
Aliporudi Zambia, aliamua kujiunga na timu ya nyumbani kwao
ya Konkola Blades, lakini akaondoka na kwenda kujiunga na Lupopo ya Lubumbashi,
mwaka 2010 na yalipomshinda alirejea tena Konkola Blades kwa mara ya tatu.
Katika michuano ya Kombe la Challenge, Sunzu akaonyesha
kiwango kikubwa na kufanikiwa kufunga mabao matano, hivyo kuivutia Al Hilal
iliyoamua kumchukua.
Sunzu akajumuishwa katika ziara ya timu ya taifa katika nchi
za Misri na Israel kabla ya kuchukuliwa na Al Hilal, huku kukiwa na madai TP
Mazembe nayo ilikuwa inamtaka, timu ambayo anachezea pia ndugu yake, beki, Stopilla.
Baada ya Al Hilal kumtema, Simba ikaingia kati na kuanzia
kumfuatilia mshambuliaji huyo na kumtwaa.
Msimu uliopita alianza vizuri na alikuwa ana mchango mkubwa
katika mataji matatu iliyotwaa Simba, kuanzia Ngao ya Jamii, Ligi Kuu na hata Kombe
la Urafiki, lakini sasa dalili za kile kilichofanya atemwe El Hilal zinaanza
kuonekana katika Kagame.
Sunzu anaboronga uwanjani, wakati mshambuliaji mpya Abdallah
Juma anafanya vitu.
Sunzu wa Kagame 2012; Hapa ni baada ya kukosa bao la wazi akiwa anatazama na nyavu |
SIMBA WAFANYE NINI?
Klabu zetu katika mfumo wake wa utawala, zinakosa mtu mmoja
muhimu sana- mtaalamu wa saikolojia. Huyu ndiye anayeweza kumrudisha uwanjani
Sunzu kwa sasa.
Mtu mwenye tatizo la kisaikolojia kumfokea, kumkaripia
kumuadhibu ni kuzidi kumwathiri- mtu wa aina hiyo ni wa kuzungumza naye
taratibu, ili kujua kinachomsibu.
Unaketi naye, unazungumza naye kirafiki- kwa kumteka
unamsimulia mambo yako- hata matatizo ya kifamilia, au matukio yoyote yanayohusu
maisha- ili kumteka na kumfanya naye akusimulie ya kwake.
Hapo unaweza kugundua tatizo lake, na mwisho wa siku ikawa rahisi
kumsaidia. Kumuwakia mtu wa aina hiyo, ni kuzidi kumchanganya- alilonalo
kichwani hajajua atalitatua vipi, unamuongeza linguine, tena ambayo yote yanahusu
mustakabali wa maisha yake.
Kuna wakati niliwahi kuandika nikiwa pale DIMBA, kuhusu
Haruna Moshi Shaaban ‘Boban’, kwamba kumsimanga si kumsaidia- wakati huo kocha
wa timu ya taifa alikuwa Jan Poulsen.
Boban anajiamini ana uwezo na ndio maana anachezea Simba Dar
es Salaam hadi Setif- Jan Poulsen akamuomba achezee U23 ili aone kiwango chake
kama anastahili jezi ya timu ya taifa, akagoma akidhani amedharauliwa.
Wachambuzi wetu wa kibongo, walimkandia kinoma- mi nikasema
lazima tutafute njia mbadala ya kumkabili Boban na si kumsusa, kwani kijana
anaonekana ana tatizo la kisaikolojia.
Vipi sasa Stars ikiwa chini ya Kim Poulsen, Boban alifanyiwa
majaribio wapi ili kupewa jezi? Tazama kijana anavyobadilika taratibu, jana
nimemshuhudia Boban anakwenda kukaba na hadi kupokonya mpira baada ya kupoteza.
Kwa hiyo nachowaambia Simba, walifanyie kazi suala la Sunzu.
Huyo bado ni mchezaji mzuri na kijana mdogo, kwani alizaliwa Mei 2, 1989 katika
mji wa Chingola nchini Zambia..
Sunzu alianza maisha ya soka kwa kuichezea Afrisport F.C na
mwaka 2005 alijiunga na timu aliyoichezea baba yake ya Konkola Blades, lakini
baada ya mwaka mmoja wa kuichezea timu ya vijana mwaka 2007 akapandishwa hadi
timu ya wakubwa.
Katika msimu wake wa kwanza aliichezea Konkola Blades mechi
25 na kufunga mabao 15, lakini Februari 2007 akachukuliwa kwa mkopo na timu ya
AS Marsa, ambapo alicheza mechi 16 na kufunga mabao mawili katika Ligi Kuu ya
Tunisia.
Lakini Juni 2008 akarudi Konkola Blades lakini Septemba 2,
2008 akapelekwa kwa mkopo katika timu ya LB Chateauroux inayoshiriki Ligi
Daraja la Pili Ufaransa kwa muda wa mwaka mmoja.
Julai 2009 akarudi AS Marsa ambaye alicheza Oktoba 29, kabla
ya timu hiyo kuamua kuachana naye, ambapo akiwa hapo alicheza mechi mbili tu. Na
si kwa Simba, klabu zetu zote, hasa zile kubwa, Azam na Yanga pia, wawe na
wataalamu wa saikolojia kwa ajili ya wachezaji wao. Kituo.
Sunzu baada ya kuwaliza Yanga mechi ya Ngao, msimu uliopita |
0 comments:
Post a Comment