21 Julai, 2012 - Saa 14:46 GMT
Mabingwa watetezi wa Ligi ya mabingwa barani Afrika, Esperance ya Tunisia wamesalia kileleni mwa kundi A, baada yua kujinyakulia ushindi wa dakika ya mwisho kwa kuikandika AS Chlef 3-2 siku ya Ijumaa.
Esperance ilipiga hatua kupitia mkwaju wa peneti ya Khaled Mouelhi kabla ya Farid Mellouli kurudisha bao hilo dakika chache kabla ya kipenga cha mapumziko.
Mohamed Messaoud akaongezea bao la ugenini mnamo dakika ya 85, kabla ya Mouelhi kutikisa nyavu kupitia mkwaju wa peneti.
Yannick Ndjeng kutoka Cameroon akaondoa ubishi kwa kufunga bao la dakika ya 90 na kuwawezesha Watunisia pointi zote tatu mjini Tunis.
Hivi sasa Esperance ina jumla ya pointi sita kutoka mechi mbili kufuatia ushindi wake dhidi ya Sunshine Stars 2-0 nchini Nigeria mapema mwezi huu.
AS Chlef kwa hiyo inavuta mkia wa kundi A, bila kuwa na pointi yoyote baada ya kuchapwa bao 1-0 na Etoile du Sahel nyumbani kwao katika michuano ya duru ya kwanza.
Etoile ilitazamiwa kuchuana na Sunshine katika mchuano wa baadaye jumamosi kwenye uwanja ulio pwani ya Bahari Mediterranean huko Sousse.
Ushindi kwa Etoile utaleta uwezekano wa klabu mbili za Tunisia kuingia nusu fainali.
Jumapili kuna mechi za kundi B ambapo TP Mazembe kutoka DR Congo itaipokea Berekum Chelsea kutoka Ghana wakati Zamalek itapambana na Al Ahly katika kinyanganyiro cha Derby ya Misri. Mechi hiyo itachezwa ndani ya uwanja usio na mashabiki kutokana na sababu za kiusalama.
SOURCE: BBC SWAHILI
0 comments:
Post a Comment