Dullah Mabao |
Na Princess Asia
MSHAMBULIAJI mpya wa Simba na anayeinukia vizuri, aliyeumia
kwenye mechi ya jana ya mwisho ya Kundi A, dhidi ya AS Vita ya Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Klabu
Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam, Abdallah Juma anaendelea vizuri na anaweza kucheza Nusu Fainali dhidi
ya Azam FC Jumatano.
Dullah Mabao aliumia misuli ya paja la kushoto kwa nyuma
dakika ya 27 na kushindwa kuendelea na mchezo huo ulioisha kwa sare ya 1-1,
nafasi yake ikichukuliwa na Kiggi Makassy.
Daktari wa Simba SC, Cossmas Kapinga ameiambia BIN
ZUBEIRY leo kwamba Dullah
anaendelea vizuri na alipata matatizo kidogo tu ya misuli na kwamba leo anaweza
kufanya mazoezi mepesi kujiandaa na Nusu Fainali ya kukata na shoka dhidi ya
Azam.
Pamoja na kutoa sare ya 1-1 na Vita jana, lakini Simba
ingeweza kuondoka na ushindi, kama mshambuliaji wake Mzambia, Felix Sunzu asingekosa
penalti dakika ya kwanza ya muda wa nyongeza baada ya kutimu dakika 90 za
kawaida, kufuatia beki mmoja wa Vita kuunawa mpira kwenye eneo la hatari,
lakini shuti lake lilipanguliwa na kipa Mcameroon, Lukong Nelson kabla ya
mabeki wake ‘kuosha’.
Hadi mapumziko, Vita walikuwa mbele kwa bao 1-0, lilifungwa
kwa penalti na Etikiama Taddy, dakika ya 35, baada ya Juma Said Nyosso kuunawa
mpira kwenye eneo la hatari.
Simba ilisawazisha bao hilo kupitia kwa Haruna Moshi ‘Boban’
aliyeingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Patrick Kanu Mbivayanya dakika
ya 66.
Kwa matokeo hayo, Simba imemaliza kama mshindi wa tatu
katika Kundi A na itamenyana na Azam katika Robo Fainali, wakati mabingwa
watetezi Yanga watamenyana na Mafunzo Jumanne. Robo Fainali nyingine zitakuwa
kati ya URA na APR na Atletico dhidi ya Vita.
0 comments:
Post a Comment