Danny |
DANNY Davis Mrwanda na
Nizar Khalfan wanafaa kuwa kioo cha wachezaji wa Tanzania. Hawa jamaa ni
wapiganaji, hawasiti kurudi nyuma kujipanga upya, mara wanapopoteza nafasi.
Sasa Danny amesaini Simba, akitokea Hoang Anh Gia Lai, aliyoichezea kwa msimu mmoja akitokea Dong Tam
Long An, zote za Vietnam.
Ni huyu Danny ambaye mwaka 2004 alikwenda kufanya majaribio
katika klabu ya Yanga, lakini pamoja na kufanya vizuri, enzi hizo akiitwa Okocha,
akatemwa dakika za mwishoni, kocha wa Yanga wakati huo, Kenny Mwaisabula.
Danny alipotemwa Yanga dakika za mwishoni, akaenda Arusha
kujiunga na AFC ya huko na msimu wa 2005 alicheza soka baab kubwa, hata
akasajiliwa na Simba SC msimu uliofuata.
Alicheza Simba SC kwa mafanikio na msimu wake wa kwanza tu,
aliitwa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars.
Mwaka 2008, Danny alinunuliwa na klabu ya Tadhamon ya Kuwait
kwa pamoja na kiungo Nizar Khalfan. Mchongo waliupataje? Stars ilikwenda ziarani
Saudi Arabia na ikiwa huko ndipo soka yao ikamvutia kiongozi mmoja wa klabu
hiyo, akawanunua wote.
Lakini baada ya msimu mmoja, Danny hakuongezewa mkataba na
klabu hiyo, hivyo akarejea nyumbani na kujiunga tena na Simba SC. Hakurudi kama
amefika, au aliyekata tamaa, bali aliendelea na mikakati yake ya kutoka.
Nizar |
Alicheza Simba hadi 2010 alipopata ofa tena ya kwenda Vietnam
ambako amecheza hadi msimu huu anarudi. Sitaki kuamini Danny amekuja kumalizia
soka yake Simba SC. Naamini kama ilivyokuwa awali, amerudi kucheza nyumbani,
baada ya kumaliza mkataba Vietnam, huku akitafuta nafasi nchi nyingine.
Kuna kitu Danny amepost kwenye page yake ya facebook leo,
kinachonifanya niamini huyu ni mchezaji anayejitambua na mwenye malengo. “U-superstar
huwa ni feki...hung'arisha tu ukiwa na market, open your mind bongo superstars,”
ameandika.
Kwa mtazamo huu, Danny anatembea akijua ana deni. Ana deni
la kuhakikisha anakuwa na soko wakati wote. Na kama ni hivyo, Danny hawezi kubweteka,
lazima atahakikisha siku zote anakuwa vema.
Kama mchezaji, Danny anatakiwa kuwa fiti wakati wote ili
acheze vizuri. Na kucheza vizuri ndiko kutamfanya
aendelee kuwa supa star na kupamba kurasa, kuanzia za blogs hadi magazeti. Kama
mimi BIN
ZUBEIRY, nafungua moyo wangu. Nampenda sana wakati wote kama mchezaji
wa Kitanzania kioo cha wachezaji wengine. Nampenda Nizar Khalfan, ingawa
sijamuelezea kwa undani hapa, lakini naye ana fikra sawa na za Danny.
Amekatishiwa mkataba Marekani, karudi Yanga kujipanga upya,
kama tu alivyomaliza mkataba Kuwait, akarudi Moro United kujipanga. Maisha ukiyaonea
noma, yanakutoa nishai kweli kweli.
Najua, kuna wachezaji walikwenda nje kucheza, ama wamekosa
timu au wametemwa, lakini wanaona noma kurudi nyumbani kujipanga upya. Danny na
Nizar hawana akili hiyo. Na watarudi tu juu. Safi sana vijana.
0 comments:
Post a Comment