Na Prince Akbar
BENKI ya CRDB PLC imeibuka mshindi wa tenda ya kutengeneza
tiketi za elektroniki za kuingilia uwanjani iliyotangazwa na Shirikisho la
Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Kampuni saba zilijitokeza katika hatua ya awali ya kuonesha
nia (Expression of Interest) kwa ajili ya tenda hiyo ambapo Aprili 19 mwaka huu
Kamati ya Mipango na Fedha ya TFF ambayo ndiyo Bodi ya Tenda ya shirikisho
ilipitia maombi hayo na kupitisha nne kati ya hizo.
Baadaye kampuni hizo nne; CRDB Bank PLC, Prime Time
Promotions, Punchlines (T) Limited na SKIDATA People Access Inc. zilitakiwa
kuwasilisha rasmi tenda zao zikionesha jinsi zitakavyofanya shughuli hiyo
pamoja na gharama ya utengenezaji kwa tiketi moja.
Bodi ya Tenda ya TFF ilikutana Julai 13 mwaka huu kwa ajili
ya kupitia tenda hizo ambapo kampuni zote nne zilifanya uwasilishaji
(presentation) wa jinsi zitakavyofanya shughuli hiyo, na baadaye kuipa kazi
hiyo benki ya CRDB.
Uamuzi huo wa Bodi ya Tenda uliwasilishwa mbele ya Kamati ya
Utendaji ya TFF. Kamati ya Utendaji ya TFF katika kikao chake kilichofanyika
Julai 14 mwaka huu iliridhia uteuzi huo wa benki ya CRDB.
Baadhi ya vigezo ambavyo Bodi ya Tenda ya TFF iliangalia na
kuipa CRDB tenda ni uwezo wa kufanya kazi hiyo (capacity), hadhi yake mbele ya
jamii (credibility) katika shughuli inazofanya na teknolojia ya kisasa
itakayotumika kutengeneza tiketi hizo.
Uamuzi wa TFF kutangaza tenda hizo ulilenga kuimarisha
udhibiti wa mapato ya milangoni na kurahisisha mtiririko mzima wa washabiki
kupata tiketi na kuingia viwanjani.
Rais wa TFF, Leodegar Tenga amesema: “Hatua hii ni muhimu
sana, kwani tulikuwa tukiisubiri kwa muda mrefu. Si tu itaimarisha udhibiti wa
mapato, bali pia itaondoa matatizo ya tiketi na kuendelea kujenga credibility
(kuaminika) ya TFF. Mafanikio haya si kwa TFF pekee bali mpira wa miguu kwa
ujumla.”
CRDB imeanza mara moja mchakato wa shughuli hiyo ambapo
tiketi hizo zinatarajia kuanza kutumika rasmi katika kipindi cha kati ya miezi
miwili na mitatu kuanzia sasa.
0 comments:
Post a Comment