Bondia Francis Cheka usiku wa leo amegoma kuzipiga na mpinzani
wake, Japhet Kaseba katika pambano lililotakiwa kufanyika Uwanja wa Taifa, kwa
visingizio ambavyo haviingii akilini.
Ulipowadia muda wa mabondia hao kupanda ulingoni, Kaseba
alipanda akiwa tayari amevalia vifaa vya michezo kasoro glavu ambazo alizikuta
ulingoni na baadaye MC akamuita Cheka. Ajabu Cheka alipanda kama hahusiki na pambano,
akiwa amevalia kiraia.
Akaomba mic azungumze, lakini MC akanyima naye akaamua
kuteremka ulingoni. Ni kama kuna siri ilikuwa inaendelea, ambayo waandaaji
walikuwa wanaijua. Yaasin Abdallah ‘Ustadh’ rais wa TPBO, alimchongea Cheka kwa
mashabiki kwamba, amefanya kitendo kisicho cha kiungwana kwa kula fedha ya
promota na kugoma kupigana.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kitendo hicho
ambacho hakika si cha kiunamichezo na kingeweza kuhatarisha amani uwanjani kama
mashabiki waliolipa fedha zao kwenda kuwaona wawili wakizipiga, wangeamua ‘kulianzisha’,
hakika Cheka hakuwa na hoja za msingi kukwepa kukipigana.
Alidai mpinzani wake amepigana mapambano matatu, kapigwa
mawili hivyo ni kibonde si sawa yake hawezi kupigana naye na pia walipopima uzito
alikutwa na uzito mdogo, hivyo pia si sawa yake na hawezi kupigana naye. Lakini
swali ambalo hakujibu ni kwa nini alisaini mkataba na kuchukua malipo ya
kupigana, halafu anagoma kupigana. Pichani Kaseba akivaa glavu ulingoni tayari kwa pambano.
|
0 comments:
Post a Comment