Na Prince Akbar
MABINGWA watetezi wa Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati,
Kombe la Kagame, Yanga SC leo wanashuka Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam
kumenyana na timu ya Jeshi la Rwanda, APR katika mchezo wa mwisho wa Kundi C
kutafuta mpangilio wa nafasi ya kwanza, ya pili na ya tatu kwenye kundi hilo.
Yanga yenye pointi tatu, katika nafasi ya tatu, inaweza
kumaliza mechi za kundi hilo katika nafasi ya pili, iwapo itashinda mechi ya
leo, lakini sare au kufungwa itabaki katika nafasi hiyo hiyo.
APR yenye pointi nne, inaweza kupanda hadi nafasi ya kwanza
kwenye kundi hilo na kuongoza kwa wastani wa mabao, iwapo itaifunga Yanga,
kwani hadi sasa timu hiyo ya jeshi la Kagame, inalingana kwa wastani wa mabao
(GD) na vinara wa kundi hilo, Atletico ya Burundi, saba kila timu.
Katika mchezo wa leo, Yanga iko hatarini kuwakosa nyota wake
wawili, kipa wake namba moja, Mghana Yaw Berko, ambaye ni majeruhi sawa na
kiungo wa zamani wa APR, Haruna Niyonzima, wakati kipa Ally Mustafa ‘Barthez’
yuko fiti kwa asilimia 100 sawa na beki Juma Abdul aliyeumia kwenye mechi ya
kwanza dhidi ya Atletico, timu yake ikilambwa 2-0.
Safu ya ushambuliaji ya APR inaweza kuongozwa na wakali
wawili, Mrundi Suleiman Ndikumana na Olivier Karekezi ambao wote wana miili
mikubwa ni hatari kweli sambamba na kiungo mshambuliaji, Mganda Danny Wagaluka,
wakati Yanga bila shaka Said Bahanuzi na Hamisi Kiiza wataendelea kumpumzisha
kwenye benchi Jerry Tegete na Nizar Khalfan ataongoza safu ya kiungo.
Kihistoria mechi kati ya Yanga na APR huwa ni kali na za
kusisimua tangu zianze kukutana mwaka 1995 katika Klabu Bingwa Afrika Mashariki
na Kati na mara nyingi watoto wa Jangwani hunyanyaswa na timu hiyo ya jeshi la
Rwanda.
Mechi hiyo itatanguliwa na mchezo wa Kundi A, kati ya Ports
ya Djibouti na URA ya Uganda.
JE WAJUA?
1.
Klabu ya Armee Patriotique Rwandaise, maarufu
kama A.P.R., ilianzishwa mwaka 1993 na inamilikiwa na Jeshi la Rwanda na katika
kipindi cha uhai wake, mafanikio yake makubwa ni kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya
Rwanda mara 12 (1995, 1996, 1999, 2000, 2001, 2003, 2005, 2006, 2007, 2009,
2010 na 2011), Kombe la Kagame mara mbili (2004 na 2007) na kufika Nusu Fainali
ya Kombe la Washindi mwaka 2003.
2.
Young Africans SC maarufu kama Yanga
iliyoanzishwa rasmi mwaka 1935, hadi sasa mafanikio yake makubwa ni kutwaa
ubingwa wa Ligi Kuu ya Bara mara 23, (1968, 1969, 1970, 1971, 1972, 1974, 1981,
1983, 1985, 1987, 1989, 1991, 1992, 1993, 1996, 1997, 1998, 2002, 2005, 2006,
2008, 2009 na 2011), Kombe la Kagame mara nne (1975, 1993, 1999 na 2011),
kufika Robo Fainali ya Klabu Bingwa Afrika mara tatu (1969, 1970 na 1998) na
Kombe la Washindi 1996.
3.
Wakati Yanga, kocha wake ni Mbelgiji Tom
Saintfiet, APR inafundishwa na kocha Mholanzi, Ernie Brandts- na wakati Yanga
Mwenyekiti wake ni mfanyabiashara milionea, Yussuf Manji, APR Mwenyekiti wake
ni mdogo wa rais wa Rwanda, Paul Kagame aitwaye Alex Kagame.
4.
Nembo ya Yanga ina alama ya Mwenge, ramani ya
Afrika na mpira- ikimaanisha kushiriki harakati za Uhuru wa Tanganyika, ambayo
baadaye iliungana na Zanzibar na kuwa Tanzania (Mwenge), timu halisi ya Afrika
(ramani) na timu ya mpira (mpira), wakati nembo ya APR ina alama ya mnyama
Simba na mpira- vikimaanisha, ni wafalme kama mnyama Simba porini (Simba) na
timu ya mpira (mpira).
5.
Wakati Yanga huvalia jezi za rangi ya kijani na
njano, APR wao huvalia jezi za rangi nyeupe na nyeusi siku zote, mara nyingi zikiwa
za mistari ya punda milia.
6.
Wakati wapinzani wa jadi wa Yanga, nchini
Tanzania ni Simba SC kwa APR wapinzani wao wa jadi Rwanda ni Rayon Sport.
0 comments:
Post a Comment